KwaZulu – Natal, Afrika kusini
Idadi ya vifo vimezidi kuongezeka na kufika 72 huku Zaidi ya watu 800 wamekamatwa na polisi kufuatiwa ghasia zinazoendelea nchini Afrika kusini zidi ya kupinga kwenda jela kwa Rais wa zamani Jacob Zuma.
Waandamanaji waligeuza maandamano hayo na kuwa ghasia mwishoni mwa wiki, wakichoma moto, kufunga barabara kuu na kuvamia na kupora maduka.
Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, amelaani vikali vurugu hizo ambazo zimesababisha vifo vya raia na matukio mabaya ya uporaji wa mali ya umma na kibinafsi, uharibifu wa miundombinu, ikiwemo kusitishwa kwa huduma muhimu katika eneo la Kwazulu-Natal, Gauteng na maeneo mengine ya Afrika Kusini.
Mamia ya wanajeshi yalitumwa kusitisha ghasia na uporaji nchini Afrika Kusini na kudhibiti machafuko hayo yaliyoibuka siku tano zilizopita.
Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika ametoa wito wa jitihada za haraka kufanyika ili kurejesha amani na utulivu katika taifa hilo kwa kuzingatia utawala wa sheria.
Pia alifafanua kuwa kushindwa kufanya hivyo athari itakuwa kubwa si kwa taifa hilo pekee bali kwa ukanda wote.