25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Idadi ya vifo vya jengo Kariakoo yafikia 29, uchunguzi kuendelea

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Idadi ya vifo vilivyosababishwa na jengo la ghorofa tatu lililoporomoka katika eneo la Kariakoo imeongezeka na kufikia 29 baada ya kukamilika kwa zoezi la uokoaji leo. Miongoni mwa miili iliyopatikana, mitatu bado haijatambuliwa, na juhudi za kuitambua kwa kutumia teknolojia ya vinasaba zinaendelea.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba, alisema kuwa zoezi la uokoaji limekamilika huku kifusi kikubwa kikihifadhiwa sehemu salama kwa uchunguzi zaidi.

“Tumehakikisha tumemaliza zoezi la uokoaji na sasa tunakabidhi eneo hilo kwa usimamizi maalum wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na mamlaka za mkoa,”alisema Makoba.

Aliongeza kuwa Serikali imeanza kushirikiana na wafanyabiashara waliokuwa katika eneo hilo kutambua mali zilizookolewa na kuweka taratibu za urejeshaji.

Makoba alieleza kuwa serikali imechukua hatua tatu muhimu baada ya kukamilika kwa uokoaji ambazo ni kusaidia wafanyabiashara ambapo serikali inashirikiana na mamlaka za biashara kuanza mchakato wa kuchambua mali zilizookolewa.

Hatua nyingine ni huduma kwa wahanga ambapo serikali itahakikisha wahanga wanapata mazishi yenye heshima na kwamba majeruhi wanapata matibabu ya kina na usimamizi mealum wa Eneo: Eneo lililoathirika, ikiwemo Mtaa wa Mchikichi na Congo, litabaki chini ya usimamizi maalum kwa siku mbili hadi tatu wakati uchunguzi unaendelea.

Jengo hili lililoanguka pia limeathiri majengo mawili ya jirani, na uchunguzi unafanyika kuhakikisha usalama wa majengo hayo,” aliongeza Makoba.

Makoba alithibitisha kuwa mmoja wa wamiliki wa jengo hilo tayari amekamatwa na jeshi la polisi. Alisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea, na kamati maalum inayoshughulikia suala hilo itatoa ripoti itakapokamilika.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alitangaza kuwa shughuli zote za biashara katika Kariakoo zimeanza kurejea isipokuwa katika eneo dogo lililoathiriwa.
“Kuanzia jana mchana, wafanyabiashara wameanza shughuli zao kama kawaida isipokuwa kipande cha Mtaa wa Mchikichi na Congo ambacho kinabaki chini ya usimamizi wa mamlaka,”alisema Chalamila.

Makoba pia aliwataka Watanzania wote waliojiandikisha kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambao idadi yao ni milioni 31, kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
“Huu ni uchaguzi muhimu kwa maendeleo ya maeneo tunayoishi. Kila mmoja ajitokeze kupiga kura,” alisema.

Tukio la kuanguka kwa jengo hilo limeibua maswali kuhusu ubora wa majengo na usimamizi wa sekta ya ujenzi nchini, huku uchunguzi ukiwa hatua muhimu kwa uwajibikaji na kuhakikisha usalama wa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles