LONDON, ENGLAND
UWANJA wa soka wa klabu ya Arsenal, Emirates, umeweka historia mpya ya kuingia mashabiki wachache kwenye mchezo wao wa juzi dhidi ya Doncaster Rovers, huku kikosi hicho cha kocha Arsene Wenger kikishinda bao 1-0.
Katika mchezo huo jumla ya watazamaji 44,064 waliingia uwanjani na kuifanya idadi ndogo ya mashabiki kuingia uwanjani hapo, huku mara ya mwisho ilikuwa Septemba 20, 2011 kwenye mchezo dhidi ya Shrewsbury Town ambapo waliingia watazamaji 46,539 katika Kombe la Ligi.
Katika mchezo wa juzi, viti vingi vilionekana kuwa wazi kwenye uwanja huo wa Emirates japokuwa uongozi wa Arsenal uliamua kupunguza gharama za tiketi na kufikia pauni 10 kwa watu wazima ambayo ni sawa na 30,068 ya Kitanzania, wakati huo wadogo wakitakiwa kulipa pauni 5 sawa na 15,034.
Nyota wa klabu ya Arsenal, Theo Walcott, alipeleka furaha kwa mashabiki wa Arsenal waliojitokeza uwanjani hapo kwa kupachika bao moja la ushindi katika dakika ya 25.
Michezo mingine ambayo ilipigwa juzi ni pamoja na Everton waliokuwa kwenye uwanja wa nyumbani na kufanikiwa kushinda mabao 3-0 dhidi ya Sunderland, hivyo Everton wameweza kuingia hatua ya 16 bora.
Chelsea walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani na kufanikiwa kushinda mabao 5-1 dhidi ya Nottm Forest, wakati huo kwenye uwanja wa Old Trafford wenyeji Manchester United waliweza kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Burton.
West Brom walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani lakini walipokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Manchester City. Klabu hizo ambazo zimepoteza michezo hiyo zimeshindwa kusonga mbele kwenye hatua ya 16 bora, lakini zile ambazo zimeshinda zimeweza kuingia hatua hiyo.
Hatua ya 16 bora ya michuano hiyo inatarajia kuanza kutimua vumbi Oktoba 25, mwaka huu kwenye viwanja mbalimbali.