Nora Damian-Dar Es Salaam
ZIKIWA zimesalia wiki mbili wakristo duniani wote duniani kuungana kuadhimisha sikukuu ya Pasaka, uhakika wa waumini wa kanisa katoliki nchini kufanya ibada makanisani upo shakani kutokana na hofu ya kusambaa virusi vya corona.
Hatua inakuja baada ya kutolewa mwongozo unaoelekeza namna ibada zitakavyokuwa kuanzia Jumapili ya Matawi, Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na siku ya Pasaka.
Tayari makao makuu ya kanisa hilo yaliyopo Vatican – Italia yametangaza Papa ataongoza misa kupitia mitandaoni bila waumini kufika makanisani.
Kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) ambao MTANZANIA Jumapili imeuona, unaelekeza maadhimisho ya sikukuu ya Pasaka mwaka huu yatafanyika bila waumini kukusanyika (kukongamana) kutokana na tishio la visuri vya corona.
“Kutokana na kusambaa kwa kasi kwa ugonjwa wa covid – 19 wa corona virus na kwa kuzingatia tahadhari kutoka mabaraza ya maaskofu, ‘kongregasio’ hii inatoa mwongozo wa jumla na ushauri kwa kuzingatia ule wa awali wa tarehe 19 Machi.
“Ikitiliwa maanani kuwa tarehe ya maadhimisho ya Pasaka haiwezi kuhamishwa, katika nchi ambazo zimeathirika kwa ugonjwa na makatazo yahusuyo mikusanyiko na safari yanayotolewa, maaskofu na mapadri wanaweza kuadhimisha ibada za juma kuu katika sehemu zinazofaa bila uwepo wa waamini, pia wakiepuka maadhimisho ya pamoja na ishara ya kutakiana amani.
“Waamini wanaweza kufahamishwa muda wa kuanza maadhimisho hayo ili waweze kujiunga kwa sala wakiwa nyumbani. Matangazo mubashara kwa njia za kisasa za mawasiliano zaweza kutumika.
Kwa ujumla ni muhimu kutenga muda wa kutosha kwa sala hususani sala ya kanisa. Mabaraza ya maaskofu ya majimbo yaendae miongozo itakayosaidia familia na watu binafsi katika sala,” ilieleza sehemu ya mwongozo huo.
JUMAPILI YA MATAWI
Mwongozo huo unaelekeza kukumbuka kuingia kwa bwana Yerusalemu kuadhimishwe kwenye majengo ya ibada na kwamba katika makanisa ya kiaskofu yatatumia kanuni ya pili kadiri ya misale ya kirumi wakati kwenye makanisa ya parokia na sehemu nyingine itatumika kanuni ya tatu.
ALHAMISI KUU
Mwongozo huo ulifafanua kuwa tukio la kuoshwa miguu halitafanyika na kwamba baada ya misa maandamano ya kuhamisha ekaristi takatifu hayatafanyika na badala yake sakramenti takatifu itahifadhiwa kwenye kifaa maalumu (Tabernako).
“Katika siku hii ruhusa maalumu inatolewa kwa mapadri wote (mahali penye katazo la mikusanyiko) kuadhimisha misa sehemu inayofaa bila uwepo wa waumini,” ilieleza sehemu ya mwongozo huo.
IJUMAA KUU
Katika ibada ya Ijumaa Kuu mwongozo huo unaelekeza kwenye sala kwa ajili ya watu wote maaskofu wataweka nia maalumu kwa ajili ya wenye taabu, wagonjwa na waliofariki na kwamba tendo la kubusu msalaba litafanywa na kiongozi wa ibada tu.
PASAKA
Maadhimisho yatafanyika kwenye makanisa ya kiaskofu na parokiani tu na kuhusu litrujia ya ubatizo itafanyika ibada ya kurudia ahadi za ubatizo tu.
Mwongozo huo utafanyika pia kwenye seminari zote, nyumba za mapadri na jumuiya zote za watawa wa kike na kiume.
Mwongozo huo umefafanua kuwa maandamano na ibada pekee ambazo hufanyika kwenye juma kuu na siku tatu kuu za Pasaka, yanaweza kuhamishiwa katika siku nyingine za mwaka, mfano tarehe 14 na 15 Septemba kadiri ya maamuzi ya askofu wa mahali husika.
RAIS BARAZA LA MAASKOFU
MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Gervas Nyaisonga, ambaye alikiri kuufahamu mwongozo huo na kwamba waliutoa wakati wa kumuapisha Askofu wa Jimbo la Moshi.
“Ile tuliyetoa tuliisoma Moshi wakati wa kumsimika Askofu wa Moshi, ndiyo ‘standard’ lakini kila askofu anaweza kuiboresha zaidi. Yaani ile ni ‘guideline’ ya kitaifa lakini kila askofu anaweza akaiboresha kwa kuona kwamba asisitize kitu gani zaidi. Kuna mengine waamini wasikilize mwongozo wa askofu wa jimbo,” alisema Askofu Nyaisonga.
Alisema wamechukua taratibu mbalimbali kuepusha watu wasije wakapata maambukizi huku wakizingatia pia miongozo iliyotolewa na Serikali.
“Kuna masuala ambayo tumesisitiza sisi yanayotuhusu kiibada kwa mfano, kuna kupeana amani, kuoshana miguu, wanaokunywa ile damu ya Yesu kuna kitu tuna – shea kikombe kimoja, na ile mikusanyiko ya pamoja hayo tumepeana mwongozo.
“Mengine tutafuata kwa heshima zote tunayoagizwa na Serikali, kwa hiyo wakitangaza kitu kingine leo hatutapinga tutafuata ‘guidline’ ya Serikali kwa sababu ina jopo la wataalamu wanaoelewa.
“Unaweza ukawauliza baadhi ya maaskofu kwenye jimbo lake anasemaje, usishangae mwingine ukakuta amesema kitu zaidi ya hiki tulichosema.
“Lakini pia Serikali isichelewe kutoa maagizo kwa uhakika pale ambapo inajua hili ni kwa manufaa ya wananchi, tungependa tufanye kazi pamoja na Serikali,” alisema.
JIMBO LA NGARA
MTANZANIA Jumapili lilizungumza na Askofu wa Jimbo Katoliki la Ngara, Severine Niwemugizi, ambaye alisema huenda sikukuu hiyo ikaadhimishwa bila kuwapo waumini.
“Kwa kweli zitaadhimishwa kwa namna ya pekee kidogo huenda bila waumini, kwa hiyo huenda mapadri tutakaokuwemo makanisani tutasali wenyewe na labda waumini wachache sana,” alisema Askofu Niwemugizi.
MGONJWA MWINGINE ZANZIBAR
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed, alisema mgonjwa mmoja amebainika visiwani humo ambaye ni mwanamke raia wa Tanzania.
Alisema mwanamke huyo mwenye miaka 57 alitokea safarini nchini Uingereza na anafanya idadi ya wagonjwa wa corona visiwani humo kufikia watatu huku Tanzania Bara ikiwa na 11 na hivyo wagonjwa wote nchini kufikia 14.
CHINA YASITISHA VISA ZOTE
China imesitisha vibali vya kuingia nchini humo (visa) kuanzia jana na kwamba Watanzania na wanafunzi wenye hati za ukazi wasitishe mipango ya kurejea nchini humo hadi itakapotangazwa.
Taarifa iliyochapishwa kupitia ukurasa wa Twitter wa Ubalozi wa Tanzania – China, imeeleza hatua hiyo ni mwendelezo wa kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo.
“Katika kudhibiti kuenea kwa Covic-19, kuanzia Machi 28, 2020 Serikali ya China imesitisha visa zote za kuingia nchini China na hati za ukazi (residence permit), Watanzania wenye Visa na wanafunzi wenye hati za ukazi wasitishe mipango ya kurejea China hadi itakapotangazwa tena” ilieleza taarifa hiyo.
MINADA YA MIFUGO ISIFUNGWE
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amewataka wakurugenzi katika mamlaka za Serikali za Mitaa kutofunga minada ya mifugo na mialo ya samaki badala yake shughuli ziendelee huku watu wakichukua tahadhari.
Alitoa maelekezo hayo jana baada ya kutembelea Soko la Kimataifa la Samaki Feri na Mnada wa Mifugo uliopo Pugu.
Alisema baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali wameanza kuzuia minada na kuwatisha wafanyabiashara licha ya kuwapo jitihada za kuudhibiti ugonjwa huo.
“Minada ya mifugo na masoko ya uvuvi yasifungwe, naelekeza wakurugenzi wote wasifunge masoko ya mifugo wala samaki bila kutueleza, tunataka biashara iendelee isipokuwa wafanyabiashara wachukue tahadhari. Hakikisheni ninyi wenyewe (wafanyabiashara) bila kuchungwa mchukue tahadhari,” alisema Ulega.
Mmoja wa wafanyabiashara wa mifugo kutoka Nzega, Masese Samson, alilalamikia kufungwa kwa mnada uliopo Ndala na kusababisha kuathiri biashara hiyo.
“Kule Ndala – Nzega walikuwa wanasema hakuna mnada sasa tukajiuliza mbona hatujatangaziwa,” alisema Samson.
Mfanyabiashara mwingine alidai kuwa juzi watu waliokuwa kwenye mnada katika eneo la Chumbi- Muhoro mkoani Pwani walifukuzwa na kusababisha wengine kupoteza fedha na ng’ombe.
Akiwa katika soko la Feri, Ulega aliwataka wafanyabiashara kutumia fursa ya corona kuhifadhi shehena za samaki kwani baadhi ya nchi hivi sasa hazina kitoweo hicho kutokana na kuwa kwenye karantini.
Pia alisema tayari Serikali imetenga Sh bilioni moja kwa ajili ya kuboresha maeneo mbalimbali ya soko hilo na kulifanya liwe la kisasa zaidi.
Awali Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri, alisema soko la Feri linategemewa na wafanyabiashara zaidi ya 3,000 na kwamba wamechukua tahadhari kujikinga na corona kwa kupuliza dawa, kuongeza maofisa afya na kuhakikisha kila anayeingia na kutoka ananawa mikono.
“Asilimia kubwa ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanategemea kupata kitoweo katika soko la Feri, tukisema tufunge wananchi wengi watakosa kitoweo na wafanyabiashara wataathirika.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, katika kipidi kama hiki mwaka jana walikuwa wamekusanya Sh milioni 96 lakini mpaka sasa wamekusanya Sh milioni 94.