27.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali Sekou Toure yakabidhiwa vyoo

BENJAMIN MASESE-MWANZA

HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure imekabidhiwa matundu nane ya vyoo yaliyogharimu Sh milioni 20.3 huku ikiahidiwa kujengewa mengine 12 na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TD & CF).

Taasisi hiyo tawi la Tanzania, imejenga matundu hayo ya choo chini ya ufadhili wa Charty Walfare Aid ya Australia.

Akikabidhi vyoo hivyo kwa uongozi wa hospitali hiyo jana, Mwenyekiti wa TD & CF, Alhaji Sibtain Meghjee, alisema taasisi inafanya shughuli za kijamii kwenye sekta za maji, elimu na afya.

Alisema taasisi iliguswa na changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo unaoikabili hospitali hiyo, baada ya kupokea maombi kuhusu tatizo hilo na wameahidi kuendelea kujenga matundu mengine 12 ili kufikia 20.

Meghjee alisema hospitali hiyo iliyojengwa miaka ya 1970 ilikuwa na matundu ya vyoo manne idadi ambayo inapaswa kuwa katika kituo cha afya.

Alisema Sekou Toure ni hospitali kubwa ambayo inahudumia watu zaidi ya 600 kwa siku.

 “Tunatambua umuhimu wa afya bora kwa jamii na tunaahidi kujenga matundu 12 mengine ili kufikia 20, haya manane tuliyokamilisha tumekabidhi, lakini baada ya wiki sita tutakabidhi mengine.

“Katika ujenzi huo tunazingatia makundi yote yakiwamo ya watu wenye ulemavu, watumishi na wazee wa jinsia zote.

“Tumedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha afya za wananchi ili kuwaepusha na maradhi ya kuambukiza,” alisema.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou Toure, Dk. Bahati Msaki, akizungumza baada ya kupokea msaada huo wa vyoo, alisema hospitali hiyo inahudumia watu 500 hadi 700 kwa siku, hivyo msaada huo umekuja muda mwafaka kwa sababu namba ya wahitaji ni kubwa.

“Kwa niaba ya bodi na uongozi wa hospitali, tunashukuru sana The Desk & Chair kwa msada huu wa vyoo matundu manane ambayo yamegharimu fedha nyingi.

“Bado taasisi hii inaendelea kujenga mengine 12 kukamilisha matundu 20 ili kukidhi mahitaji makubwa ya wagonjwa na wasindikizaji pamoja na watumishi,” alisema Dk. Bahati.

Alisema kuna changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo kwa wagonjwa wa nje na kuongeza kuwa wodi nyingi zina changamoto hiyo na kuomba watu wengine wenye kuguswa na hali hiyo kuiga mfano wa The Desk & Chair ili kusaidia kujenga miundombinu ya vyoo hospitalini hapo.

Wakati huo huo, uongozi wa hospitali hiyo umemkabidhi cheti cha kutambua mchango wake, Mwenyekiti wa TD & CF, Alhaji Meghjee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles