Catherine Sungura – Mwanza
HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC), ipo mbioni kuanzisha taasisi ya moyo ili kuweza kuhudumia wananchi wa kanda ya ziwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa hospitali hiyo Profesa Abel Makubi, alisema kuwa wapo mbioni kuanzisha taasisi hiyo itakayokuwa na majengo mawili yenye ghorofa kumi na kumi na tano.
Profesa Makubi alisema kuwa hadi kukamilika kwa majengo hayo wanatarajia kutumia Sh bilioni 59 .
“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kutoa huduma zote za kibingwa na bobezi hapa nchini,hii itapunguzia mzigo serikali na wizara kupeleka wagonjwa nje ya nchi vilevile wananchi wa kanda hii kunufaika na huduma za moyo huku huku,” alisema
Kwa upande wa watumishi, Prof. Makubi alisema wameweza kuongeza wataalam wa fani mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wakiwepo wauguzi, madaktari, madaktari bingwa na bobezi na hivyo kufanya kazi ya utoaji huduma katika idara zote bila kuteleleka.
Hata hivyo aliishukuru Serikali kwa kusomesha madaktari bingwa na bobezi kutoka hospitali hiyo na hivyo kuifanya hospitali hiyo kutoa huduma za kibingwa ikiwemo matatizo ya tumbo, mifupa, koo, pua na ndomo, macho, mfumo wa mkojo, meno, ubongo na mishipa ya fahamu pamoja na matatizo ya akina mama.
“Huduma za upasuaji kiujumla zimeboreka sana katika awamu hii kwa upande wa upasuaji mkubwa wa kawaida pia,upasuaji maalumu wa midomo sungura, kichwa maji na mgongo wazi pamoja na upasuaji wa fistula,” alisema Prof. Makubi
Aidha, aliishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Mifupa MOI kwa, ushirikiano wa karibu katika kutoa huduma za kibingwa za upasuaji katika mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa.