Chupa za maji hatari

0
1827

*Kwa wanaotumia zaidi ya mara moja kupata saratani

*Vikombe vya plastiki navyo vyatajwa, mtaalamu aonya

Bakari Kimwanga-DAR ES SALAAM

MATUMIZI ya chupa za maji kwa zaidi ya mara moja na vikombe vya plastiki  ni hatari kwa afya ya binadamu imeelezwa.

Tahadhari hiyo, imekuja wakati jamii ikitumia chupa  za maji kwa kuendelea kuhifadhia maziwa, juisi na hata maji mengine kwenye majokofu.

Tahadhari hiyo, ilitolewa mwishoni mwa wiki Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Joshua Matiko alipokuwa akizungumza na wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Alisema hatua ya kutumia chupa ya maji kwa zaidi ya mara moja, ni hatai kwa afya kwani chupa hizo watu hushindwa kuzielewa kwa kuwa zipo za daraja la kwanza na pili.

“Matumizi ya chupa za maji zaidi ya mara moja ni hatari kwa afya ya binadamu. Ukiangalia chupa tunazotumia za kawaida ambazo hutakiwa kutumika si zaidi ya mara moja.

“Kwa mfano wapo wanaozitumia kwa ajili ya kujaza maji, kuweka maziwa,kisha kuhifadhi kwenye majokofu. Hili ni jambo la hatari kwa afya na ukitumia kwa matumizi tofauti kuna hatari ya kupata saratani.

“Lakini pia kwa jamii zetu, wapo ambao pia hupenda kutumia vikombe vya plastiki nalo ni jambo la hatari. Ukiangalia vizuri kikombe cha plastiki kama utaweka kitu cha moto, kinalainika, kama utakitumia kwa muda mrefu hutoa kama nyuzinyuzi ina maana ile plastiki iliyokuwapo imeshaunguzwa, sasa unakwenda kuzalisha sumu,kisha watu huingiza mwilini kwa kuila.

 “…si hilo tu nimetembelea maeneo mbalimbali na kufanya mahojiano, hata viti wanavyokalia wanahabari kwenye majukumu yao ni hatari kwa afya.

“Wengi tunakumbuka kuangalia maelekezo ya vinywaji mfano maji ya chupa ila hatujali kuangalia ni aina gani ya plastiki iliyotunza hayo maji. Aina za plastiki zinaonyeshwa kwa kitu kinachojulikana kama resin identification code.

“Katika kila plastiki unakuta alama ya pembe tatu yenye namba kati ya moja hadi saba au maneno  Pete, HDPE, PVC katikati ya alama hiyo ya pembetatu.  Alama hii ndiyo inakujulisha ni aina gani ya plastiki iliyotumika. mara nyingi inakua chini kwenye kitako cha chupa au kifungashio.

“Ila kwa ufupi unashauriwa kuepuka plastiki aina ya namba 3, 7 na 6. Wakati huo aina namba 1, 2,4 na 5 ni salama japo zinahitaji uangalifu unapowekea kitu cha moto au kupigwa na jua,” alisema

Kutokana na hali hiyo, alisema wao kama OSHA wana wajibu pia katika ukaguzi wao mahali pa kazi kuhakikisha kama mwajiri anatoa chai kwa watumishi basi ahakikishe kuna kuwa na vikombe vyenye ubora ili kulinda afya ya mfanyakazi wakati wote.

Alisema wakala huo, umekuwa wakifanya tafiti mbalimbali na umefanikiwa kuajiri wataalamu wa fani mbalimbali kama lengo la kulinda jamii  hasa mahali pa kazi kwenye taasisi za serikali, viwandani na hata makampuni binafsi.

“Si hilo tu, kwa mfano ninyi  ni wanahabari mnapokuwa vyumba vya habari tunaangalia usalama wenu, ikiwamo mwanga je hauna madhara pindi unapoona hilo huwa tunachukua hatua pia.

Alisema katika kutekeleza malengo na dira ya Serikali, ilikuja na mkazo katika suala la kuimarisha uchumi ili kuwaondoa Watanzania kutoka katika kipato cha chini na kuwapeleka katika kipato cha kati kupitia uchumi wa viwanda.

“Ujenzi wa miundombinu na miradi mikubwa ya umeme kama Kinyerezi na mradi wa umeme wa Nyerere ambao unajengwa katika maporomoko ya Mto Rufiji pamoja na kuimarisha miundombinu katika viwanja vya ndege nchini.

“OSHA imekuwa ikiisaidia Serikali  kutoa huduma ya mafunzo na vifaa kinga kwa wajasiriamali wadogo na wa kati bila kuchangia gharama yoyote. Kwa mfano mwaka 2015/16, tulitoa mafunzo kwa wadau 3,494, lakini idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia 4,005 na 6,477  miaka 2016/17 na 2017/18,” alisema

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alisema suala la kuangalia suala mahali pa kazi wamekuwa wakiifanyakazi hiyo kwa lengo la kulinda afya za watumishi wa umma na sekta binafsi.

Alisema wanatambua sasa yapo mazingira ambayo si salama kwa wafanyakazi jambo ambalo wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa kushtukiza .

KAULI ZA WATALAAMU

Mhadhiri na Mtafiti wa Chuo Kikuu Cha Tiba Muhimbili (MUHAS), Hussein Mohammed, hivi karibuni alinukuliwa akisema plastiki ina madhara mengi katika afya ya binadamu.

“Tatizo ni kwamba plastiki inachukua muda mrefu kuonekana madhara yake katika mwili wa binadamu. Ukiingiwa na athari za plastiki ukiwa mtoto unakutana na madhara yake ukiwa mtu mzima,” alisema

Aliyataja baadhi ya madhara ya kiafya yatokanayo na plastiki kuwa ni pamoja na kusababisha saratani, matatizo katika mfumo wa hewa na kusababisha matatizo katika mfumo wa uzazi.

Alisema matatizo mengine huwezi kusema moja kwa moja yanatokana na matumizi ya plastiki, lakini kwa mujibu wa sayansi na tafiti zilizofanywa, plastiki ina madhara mengi yanayosababisha magonjwa hayo na kuna uhusiano mkubwa wa plastiki na maradhi hayo.

Agosti, mwaka huu, Shirika la Afya Duania (WHO), ililieza kupitia tafiti yake ya athari za uchafu wa chembechembe za  plastiki kwa binadamu kwa kusema plastiki zimepatikana katika mazingira ya viumbe vya baharini, majitaka na majisafi, chakula na hewa na maji ya kunywa iwe ya chupa au bombani.

Utafiti huom ulieleza kwa kawaida chembechembe hizo za plastiki ni zile ambazo ni chini ya milimita tano kwa urefu na idadi kubwa hupatikana katika maji ya kunywa vikitokana na vipande vidogo vya chupa za plastiki za maji.

Kutokana na hali hiyo, shirika hilo lilisema uwepo wa chembechembe hizo hauhatarishi afya kwa viwango vya sasa lakini utafiti zaidi unahitaji

Akizungumza hilo, Bruce Gordon kutoka Kitengo cha Afya ya Umma, WHO alisema sasa hatari kubwa kuliko chembechembe hizo, ni maji yasiyo safi na salama huku yakiathiri watu bilioni mbili duniani kote na kusababisha vifo vya watu milioni moja kila mwaka.

Alisema mwarobaini wa suala hilo ni kuweka mifumo bora ya kuchuja maji na hivyo kupunguza uchafuzi wa plastiki ndogondogo kwa asilimia 90.

Dk. JOHN POSITIVE HEALTH AND WELLNESS

Naye taarifa iliyochapishwa katika Mtandao wa Dk. Joh Positive Health and Wellness,  ilieleza maradhara ya plastiki na usalama wa afya kwa binadamu.

Ilielezwa  kundi kubwa la watu hutumia vifaa mbalimbali vya plastiki ikiwamo kutumia maji yaliyohifadhiwa kwenye chupa za plastiki, kuhifadhi vyakula vya moto kwenye mifuko ya plastiki lakini bado hawajawahi kufikiria ni aina gani ya plastiki kama ni salama kwa afya au ina madhara kwenye afya.

Aina ya plastiki PET au PETE ambacho kirefu chake ni  Polyethylene Terephthalate, hutumika inatumika kwenye kufungashia vitu kama vinywaji mfano soda, maji, juisi na jam.

“Usalama wa aina ya plastiki ni salama kutumia japo zinapokaa muda mrefu zinaachia kwenye kitu kilichotunzwa ndani yake kemikali inayojulikana kama Antimony Trioxide. Mtu anapokula kemikalihii kwa kiasi kikubwa inapelekea aina mbalimbali za saratani ikiwemo saratani ya mapafu, utumbo.

“Pia plastiki hii inaachia kemikali ya phthalate ambayo inaharibu mpangilio wa hormone,” ilielezwa.

Hata hivyo inashauriwa kuwa ni vyema kimiminika au chakula kilicho kwenye aina hiyo ya plastiki kitumiwe mapema na kisakae muda mrefu na pindi unatumia mara moja usitumie tena.

Aija nyingine ya plastiki hatari ni HDPE ambayo kirefu chake ni  High Density Polyethylene ambayo huwa kwenye mifuko ya plastiki, chupa za maji, soda, maziwa na juisi na hata chupa za shampoo.

“Hii pia ipo kwenye kundi la plastiki ambazo ni salama ila inapopata joto huachia kemikali aina ya nonylphenol ambayo inavuruga mpangilio wa hormone, inaongeza uzalishwaji wa hormone ya estrogen hata kwa wanaume kitu kinachopelekea kupunguza uzalishwaji wa mbegu za kiume na kupunguza hormone ya testosterone. Yaani kitaalamu ina estrogenic effect.

“Aina hii ya plastic inaathiriwa sana na jua, inapopigwa na mwanga wa jua au kupata joto inaongeza kasi ya kuachia kemikali hizi hatari kwa afya hivyo epuka kuwekea vitu vya moto, kutunza sehemu zenye joto au kuiweka kwenye jua,” ilieleza taarifa hiyo

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here