26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hoja 23 za kibiashara kupatiwa majibu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Hoja 23 zinazohusu changamoto mbalimbali za kibiashara zimewekewa mkakati wa kufikishwa kwenye taasisi husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Hoja hizo ambazo ziliwasilishwa kupitia mkutano uliowakutanisha wafanyabiashara na wenye viwanda 127 zinahusu masoko, kodi, miundombinu ya uwekezaji katika viwanda, taratibu za kupata vibali vya ubora, usajili wa kampuni, vifungashio, vibali vya kusafiri nje ya nchi, unafuu wa riba kutoka taasisi za fedha na hati hataza.

Akizungumza wakati wa kufunga Maonesho ya Saba ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Profesa Ulingeta Mbamba, amesema kutokana na hoja hizo mkakati wa pamoja wenye maazimio 17 ulifikiwa na unatarajiwa kufikishwa kwenye taasisi husika kufanyiwa kazi.

“Zipo baadhi ya changamoto ambazo zimepata wasaa wa kushauri wazalishaji wetu kuzifanyia kazi ili kuendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazokubalika katika masoko, nina Imani kuwa wakizifanyia kazi Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zinazozalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika kimataifa,” amesema Profesa Mbamba.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Christopher Mramba, amewataka wafanyabiashara na wenye viwanda kuuza bidhaa zao kwa bei za kizalendo ili kuwe na utulivu katika soko.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Latifa Khamis, amesema kuna mafanikio katika maonesho hayo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya washiriki kutoka 106 mwaka 2021 hadi kufikia 502 mwaka 2022 huku sekta ya uzalishaji ikiongoza kwa kuwa na washiriki wengi.

Amesema pia watahakikisha wanatanua wigo na kuongeza bidhaa za Tanzania katika maonesho hayo.

Maonesho hayo ambayo yalianza Desemba 3, 2022 yalifanyika katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere maarufu Sabasaba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles