32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

HIVI NDIVYO WAJAWAZITO WANAVYOTEMBEA NA VIFO

Na Bakari Kimwanga


KWA muda mrefu Serikali imekuwa ikieleza mikakati kadhaa ya kukabiliana au kuondoa vifo vya kinamama wajawazito na watoto waliokuwa chini ya miaka mitano nchini.

Pamoja na hali hiyo, lakini bado vifo vya mama na watoto vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku, hali inayochangiwa na kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.

Hali hiyo kwa kiasi kikubwa huchangiwa na huduma za afya kuwa mbali na makazi ya watu na uhaba wa usafiri wa kuaminika wa kuvifikia vituo vya afya na hata kuhatarisha maisha ya wajawazito na watoto wao.

Ni wazi zaidi ya theluthi mbili ya Watanzania wanaishi vijijini na wanategemea vituo vya afya vya Serikali.

Asilimia 80 ya Watanzania hupata huduma za afya chini ya umbali wa kilomita 5 na kuchangia kuwapo kwa vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

Hata hivyo, huduma za afya ya msingi nchini zipo katika mfumo wa piramidi ambao huundwa na huduma kutoka ngazi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya. Hadi sasa kuna zahanati 4,679, vituo vya afya 481 na hospitali 219.

Takwimu zinaonyesha kuwa akinamama 578 kati ya 100,000, hufariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi. Asilimia 46 ndio wanaojifungua chini ya uangalizi wa wataalamu waliobobea, kundi kubwa wakipata tiba kienyeji na hatimaye hufariki dunia.

Serikali ilitangaza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi 2007-2017 ambao ungepunguza vifo vya wajawazito kutoka 578 hadi kufikia 175 kwa kila vizazi hai 100,000, lakini bado hali ni mbaya.

Katika siku za hivi karibuni, Mkoa wa Kigoma Shirika la World Lung Foundation (WLF), walizindua Kampeni ijulikanayo kama ‘Thamini Uhai, Okoa Mjamzito na Mtoto,’ lengo kubwa likiwa ni kupunguza vifo vya wajawazito na watoto vijijini kwa kuwa wao ndio waathirika wakubwa wa janga hili.

 

Hata hivyo, sababu kubwa imekuwa ikitajwa kuwa ni takwimu zinaonesha kuwa kati ya wajawazito 100,000 wanaotarajiwa kujifungua, vifo 410 hutokea.

Hata hivyo, mila na desturi za Watanzania wengi hasa maeneo ya vijijini zimekuwa ni moja ya chanzo cha matumizi madogo ya vituo vya afya wakati wa ujauzito, hali inayochangiwa na uwepo wa fikra potofu kuhusiana na usalama wa kujifungua nyumbani na ukosefu wa mpango binafsi wa kujifungua.

Zipo tafiti kadhaa ikiwemo zilizofanywa na World Lung Foundation kwa Mkoa wa Kigoma ambapo ilibainika kuwa asilimia kubwa ya wajawazito huhudhuria kliniki mara moja tu katika kipindi chote cha ujauzito na ni theluthi moja tu ndio ambao hujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Mwaka 2010, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 260 duniani zilizotoa ahadi mbalimbali mbele ya Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na tatizo la vifo vya wajawazito na watoto, ikiwa ni njia mojawapo ya kuboresha huduma za afya kupitia mpango wa kuboresha afya ya mama na mtoto ujulikanao kama ‘Kila mwanamke kila mtoto’.

Pia nchi iliahidi kuongeza bajeti katika sekta ya afya kutoka asilimia 12 mpaka 15, kuongeza udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vya afya kutoka 5,000 hadi 10,000 pamoja na kuboresha mifumo ya mawasiliano kwa njia ya simu kwenye vituo vya afya na kuanzisha matumizi ya magari ya wagonjwa yenye gharama nafuu.

Si jambo jipya hili kwani hata mwaka 2000, Serikali ilijiwekea malengo au mipango mbalimbali ya kimaendeleo ya milenia maarufu kama ‘Millenium Goals’ ambapo mojawapo ya mipango hiyo ilikuwa ni kupunguza vifo vya wajawazito mpaka asilimia 75 kufikia mwaka 2015.

Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), iliweka malengo mbalimbali ili kuendelea kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ambayo ni pamoja na kupunguza vifo vya kinamama wajawazito kutoka vifo 578 hadi kufikia 175, kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka 5.

Kutoka vifo 112 mpaka 45 na kuongeza idadi ya akina mama wajawazito  wanaohudumiwa na wahudumu wa afya wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha kutoka asilimia 46 mpaka kufikia asilimia 88.

Kutokana na hali hiyo, bado tunahitaji kuwa na mipango madhubuti ya kukabiliana na vifo kwa mama wajawazito na watoto kwa vitendo badala ya maneno.

Kwa hakika naweka kalamu chini na hata kutafakari kwa kina, ama kweli hivi ndivyo akina mama wajawazito wanavyotembea na vifo mkononi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles