Aveline Kitomary, Mwanza
Kaimu Mkuu wa Maabara wa Mamlaka ya Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi (TMDA) Kanda ya Ziwa, Bugusu Nyamweru amesema maabara ya ukanda huo inamashine ya kisasa yenye uwezo wa kuchunguza kemikali katika mwili wa binadamu.
Mashine hiyo inayoitwa Liquid Chromatogragh Mass Spectroscopy (LCMS) pia inauwezo wa kupima vipande vidogo vya kemikali vilivyopo katika mazingira, chakula na maji.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara iliyofanyika katika Maabara hiyo Jijini Mwanza, Nyamweru amesema uwepo wa mashine hiyo umekuwa msaada mkubwa katika Ukanda huo.
“Tunafanya chunguzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kitafiti, za kawaida, chunguzi za kung’amua au kutambua kiwango cha kemikali na dawa ndani ya mwili wa binadamu.
“Faida ya mashine hii ni kuwa unapofanya uchunguzi inauwezo wa kugundua vitu vidogo sana vilivyo katika mwili wa binadamu au katika sampuli inaweza kutambua hata kiasi cha kemikali.
“Uchunguzi unafanyika mara mbili hadi ile kemikali imeweza kuchanganuliwa katika vipande ambapo mwisho tutaweza kung’amua kwamba kipande hiki kinatokana na maumbile au kipande hiki kinatoka bacteria wa aina fulani,”ameeleza Nyamweru.
Amesema kuwa mashine hiyo pia inaweza kutumika katika kupima uchafuzi katika dawa na uwepo wa viambata hai sahihi.
“Kama kuna kiambata kingine ambacho sio hai au kiambata hai kilichoharibika katika mwili wa binadamu au tiba na katika masuala ya tafiti inaweza kutambua umbo la kemikali ya dawa au mchanganyiko unaotakiwa kufanyiwa kazi kwa tiba au shughuli yoyote.
“Katika kuangali dawa inavyofanya kazi mwilini tunafanya baada ya dawa kufika na mabaki yakatokea yana umbo gani na yametengenezwa kwa kemikali ipi tukitaka kujua kwamba dawa iliyotumika katika mwili wa binadamu katika eneo Fulani iko kwa kiasi gani.
“Tunataka kujua dawa iliyoko katika mkojo au mate au katika tishu ya mwili labda kwenye moyo,ini iko kwa kiasi gani,”amefafanua.