33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Hilal aelekeza nguvu zake Jumuiya ya Madola

Hilal Hilal
Hilal Hilal

NA WINFRIDA NGONYANI,

BAADA ya kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya Olimpiki nchini Brazil, mwogeleaji kutoka nchini Tanzania, Hilal Hilal, amedai kuwa anaelekeza nguvu zake kwenye michuano ya Jumuiya ya Madola.

Mwanamichezo huyo amedai kwamba, amefanya makubwa nchini Brazil kwa kuliwakilisha taifa, japokuwa hajafanya vizuri kama wengi ambavyo walikusudia.

“Najiamini na naona nimefanya kitu kwa nchi yangu, nitaendelea kujifua ili niendelee kufanya vema kwa ajili ya kuliwakilisha taifa hasa katika michuano ya Jumuiya ya Madola,” alisema Hilal.

Hiyo ni kauli ya mwogeleaji pekee aliyeweka rekodi mpya ya taifa kwa kuogelea mita 50, akitumia muda wa sekunde 23.70, rekodi ambayo haijawahi kushikwa na Mtanzania yeyote.

Hilal ameweka rekodi hiyo baada ya kushiriki kwenye michezo ya Olimpiki iliyomalizika nchini Rio de Janeiro, Brazil hivi karibuni, akiwa na mwenzake Magdalena Moshi.

“Nitaendelea kujifua ili niendelee kufanya vema na sasa najiandaa na michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 2018, na ile ya Olimpiki mwaka 2020,” alisema Hilal, alipozungumza na gazeti hili.

Hilal ni miongoni mwa wachezaji wa kuogelea wanaofanya vizuri katika mchezo huo hapa nchini, licha ya kukosa medali mwaka huu ameboresha kiwango chake na kuiwakilisha nchi yake kimataifa.

Akiogelea kwa mtindo wa ‘free style’, alitumia muda wa sekunde 23.70 akiwa amefanya vizuri zaidi kuliko mashindano yake yaliyopita ambapo hakuweza kufikia kiwango hicho.

Hilal anasema michezo ya Olimpiki mwaka huu ilikuwa na ushindani mkubwa, licha ya kuwa wamefanya juhudi binafsi, lakini pia kwa mashindano yajayo wanahitaji kujifua zaidi na ‘sapoti’ kubwa kutoka kwa Watanzania wote.

Katika mashindano hayo ya Olimpiki, waogeleaji Chad Le Clos wa Afrika Kusini na mwenzake kutoka Cameroon, Van der Burgh ni wawakilishi pekee kutoka Afrika ambao wameweza kufanya vizuri wakiwa wameambulia medali ya fedha.

Hilal ni miongoni mwa waogeleaji wa timu ya taifa inayoundwa na Aliasghar Karimjee, Joseph Sumari, Ammaar Ghadiyali, Adil Bharmal na Denis Mhini kwa upande wa wanaume.

Aidha, Hilal ameshawahi kushiriki mashindano ya dunia ya kuogelea ambayo kwa mwaka huu yanatarajiwa kufanyika Desemba, jijini Windsor, Canada na kushirikisha zaidi ya wanariadha 1,000.

Hilal ambaye ni nahodha wa timu ya taifa, ameshatwaa  medali ya shaba katika mashindano ya kuogelea ya CANA Kanda ya Nne  nchini Mauritius yalishirikisha nchi kutoka Uganda, Kenya, Rwanda Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudani Kusini na Sudan.

Katika mashindano hayo akitumia mtindo wa kuogelea wa butterfly alitumia muda wa sekunde 26.70.

Mwogeleaji huyo nyota hapa nchini, ameshawahi kunyakua medali nne za dhahabu kwenye mashindano ya kuogelea ya taifa yaliyofanyika kwenye bwawa la Braeburn, jijini Arusha.

Hilal alizaliwa mwaka 1994 na alianza kujishughulisha na mchezo huo tangu akiwa shuleni, anaeleza siri ya mafanikio yake ni kujituma, kufanya mazoezi mara kwa pamoja na kuhakikisha kuwa anakuwa na nidhamu ya mchezo huo.

Aidha anatoa wito kwa vijana wanaochipukia kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mchezo huo, kwani ni miongoni mwa michezo mizuri katika kujenga afya ya mchezaji kwa ujumla.

Hilal ameiomba serikali kufanya jitihada za kutatua changamoto mbalimbali zinazoukabili mchezo huu nchini ili kuendeleza mchezo huo kimataifa.

Anasema nchi yetu ina waogeleaji wengi wenye vipaji na wenye malengo endelevu, ila tatizo kubwa ni vifaa ambavyo wanatumia kufikia malengo yao.

Anasema moja ya changamoto kubwa ni bwawa la kuogelea lenye vifaa vya kisasa kwa ajili ya mashindano na mazoezi.  Mabwawa mengi hayana ubora kwa mujibu wa sheria na taratibu za mchezo huo za Chama cha Kuogelea Duniani (Fina) na chama cha Afrika (Cana).

Anaongeza kuwa mabwawa mengi ya Tanzania ni ya mita 25 ambayo hayatumiki katika mashindano ya kimataifa kama ya Cana, Michezo ya Jumuiya ya Madola, Olimpiki na mashindano ya dunia ya kuogelea.

“Mabwawa yapo, lakini si ya viwango vya Cana na Fina, mbali ya mabwawa pia tunahitaji  ‘touchpad’  kwa ajili ya kurekodi muda kwa mwogeleaji, siyo kwa kutumia ‘stop-watch’ kama ilivyo sasa, katika mashindano ya kimataifa, ‘stop watch’ zinatumika sambamba na ‘touchpad’ ambayo inaendeshwa kisasa si kwa mtu kuendesha kifaa hicho,” anasema  Hilal.

Anasema kuwa mbali ya mabwawa ya kisasa, mabwawa hayo pia hayana vifaa vinavyotakiwa kutumiwa wakati wa kuanza kuogelea ‘Diving blocks’ ambazo ni za kielektroniki.

Anasema kuwa mara zote wao huvitumia vifaa hivyo wanapokwenda nje ya nchi kwenye mashindano.

“Hapa hakuna jinsi, unalazimika kuwahi siku mbili kabla ili ufanye mazoezi, lakini wenzetu wanavyo katika nchi zao, pia hata vilabu vya mchezo huo wanatumia vifaa hivyo, ni changamoto kwetu kwani unaweza kufutiwa matokeo kwa kushindwa kuanza kwa mujibu wa taratibu,” anasema Hilal.

Anaongeza kuwa mchezo wa kuogelea kwa sasa unashika kasi kubwa, lakini viongozi wa vilabu wanaweza kukata tamaa kutokana na changamoto hizo. Hilal pia amewaomba wadau kusaidia serikali kutatua tatizo hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles