33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Heshima ya Rooney imebakia Everton si Man United

rooney

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO,

SIKU zote mchezaji akikosa nafasi katika kikosi cha kwanza kutokana na ushindani uliopo, basi kuna uwezekano uwezo wake ukawa unashuka siku hadi siku.

Hali hiyo inawafanya wachezaji wenye umri mkubwa katika soka au wale ambao wamelitumikia soka kwa muda mrefu kutafuta sehemu sahihi ambayo haina ushindani mkubwa, hasa katika kutumia nguvu na kwenda kumaliza soka lake huko.

Nyota wa timu ya taifa ya England na klabu ya Manchester United, Wayne Rooney, amekuwa na jina kubwa sana Ulaya kutokana na tabia ya watu wa England kupenda cha kwao.

Uwezo wa Rooney haukuwa mkubwa kwa kiasi hicho ambacho England ikaweza kulitangaza jina lake duniani, lakini kutokana na jinsi walivyoheshimu uwezo wake wameweza kumpa utajiri mchezaji huyo.

Katika kikosi cha timu ya taifa ya England yeye ndio nahodha wa timu hiyo, wakati huko katika kikosi cha Man United ambacho kinaongozwa na Kocha Jose Mourinho pia yeye ni nahodha, hapo ndipo tunapoona kuwa England wanaweza kumpaisha mtu wao.

Leo hii Rooney anaonekana kuwa hana jambo lolote ndani ya kikosi cha Mourinho, hata timu ya taifa ya England, huku watu wakidai kuwa mchezaji huyo umri wake wa kucheza soka la ushindani umefikia kikomo.

Rooney kwa sasa ana umri wa miaka 31, sawa na Cristiano Ronaldo, Andres Iniesta mwenye umri wa miaka 32, Zlatan Ibrahimovic mwenye umri wa miaka 35 na wengine wengi, lakini wachezaji hao wanaonekana bado kuwa na uwezo mkubwa tofauti na Rooney.

Kuna msemo unasemwa, ‘Mimi cha nini na wengine wanasema nitakipata lini’, msemo huu kwa sasa unaweza kutokea kwa kiungo huyo mshambuliaji wa Man United na timu ya taifa ya England, ambaye baada ya kukosa nafasi chini ya Mourinho sasa anawindwa na kikosi chake cha zamani cha Everton.

Mchezaji huyo kabla ya kujiunga na kikosi cha Manchester United mwaka 2004, alitokea klabu ya Everton, ambapo alicheza kwa miaka miwili kabla ya kujiunga na United.

Mashabiki wengi wa klabu ya Everton wanaukumbuka mchango wa mchezaji huyo, wanaamini kuwa bado ana kiwango kizuri, hivyo wanatamani kumuona akishuka katika dimba la Goodison Park na kuvaa jezi ya bluu.

Everton wanamhitaji kwa hali na mali mchezaji huyo, tofauti na vile ambavyo wanamhitaji Man United, ambao amewatumikia kwa jumla ya michezo 376 ya Ligi Kuu, huku akiwafungia jumla ya mabao 179.

Wakati huo anakipiga katika klabu ya Everton alicheza jumla ya michezo 67 ya Ligi Kuu na kufunga mabao 15, lakini wanaheshimu kila ambacho alikifanya mchezaji huyo, huku wakiwa na uhakika kwamba anaweza kufanya makubwa zaidi ya yale ambayo aliyafanya kwa misimu miwili ambayo aliitumikia.

Kocha wa Klabu ya Everton, Ronald Koeman, amedai kuwa atakuwa na furaha kubwa kumuona mchezaji huyo akirudi katika kikosi hicho cha zamani.

Koeman amesema mashabiki wengi wa Everton wanatamani kumuona nahodha huyo wa timu ya taifa ya England akirudi katika klabu yake ya zamani ambayo alitokea katika soka.

“Jambo la kwanza ni kwamba, mchezaji huyo ni nahodha wa timu ya taifa ya England, pili ni nahodha wa Man United, hivyo ana heshima kubwa ndani ya timu hizo mbili.

“Ukweli ni kwamba hana nafasi ya kudumu katika timu zote mbili, na sisi tuko tayari kumsajili mchezaji huyo kama atapenda kujiunga na timu yake ya zamani.

“Tunatambua uwezo wake, japokuwa anakosa nafasi, lakini tunaamini hapa ni sehemu sahihi ya yeye kuzidi kufanya yale ambayo watu walikuwa wanayaona akiyafanya akiwa United, ni kiongozi mzuri ndani ya timu,” alisema Koeman

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles