25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Adi: Watanzania kucheza soka England inawezekana

adii

NA BADI MCHOMOLO,

MTANZANIA ambaye anacheza soka la kulipwa katika klabu ya Crawley Town ya nchini England, ambayo inashiriki Ligi Daraja la Pili, akitokea klabu ya Mansfield Town kwa mkopo, Abdillahie Yussuf ‘Adi’, ameweka wazi kuwa wachezaji wa Tanzania wanaweza kucheza soka la kulipwa nchini Uingereza.

Nyota huyo, ambaye alizaliwa nchini Zanzibar, aliwahi kuitumikia klabu ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Leicester City mwaka 2011, lakini hakupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo hadi anaondoka na kujiunga na klabu ya Tomworth kwa mkopo, ambapo alicheza michezo 10 na kufanikiwa kufunga mabao 2.

Huyu ni mchezaji ambaye ameamua kutaka kulitumikia taifa lake la Tanzania katika michuano mikubwa kama vile ya Mataifa ya Afrika, japokuwa Tanzania imeshindwa kufanya vizuri katika michuano na kuweza kufuzu.

Lakini mchezaji huyo anaamini kuwa, kutokana na vipaji vilivyopo Tanzania, kuna uwezekano mkubwa wa msimu ujao kuweza kufanya vizuri na kufuzu kama ilivyo kwa mataifa mengine barani Afrika.

Hadi sasa mchezaji huyo hajapata nafasi ya kuonesha uwazo wake katika timu ya taifa, alipata nafasi ya kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Mataifa ya Afrika, lakini mchezo huo haukupigwa baada ya wenyeji, Chad kujitoa.

Huo ulikuwa ni mchezo ambao Watanzania wengi walikuwa na kiu ya kutaka kumuona mchezaji huyo ambaye anakipigi nchini Uingereza, akishirikiana na Watanzania wenzake ambao wanachezaji soka hapa ndani na nje ya Tanzania.

Adi baada ya kuitwa na kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Boniface Mkwasa, alipata nafasi ya kufanya mazoezi na wachezaji wenzake na kugundua kuwa kuna wachezaji wengi wana vipaji vya hali ya juu ambao kama wataamua kujitoa, wanaweza kucheza soka nchini England.

Mshambuliaji huyo amedai kuwa, kama wachezaji wengi wataamua kufanya yafuatayo, basi Tanzania itakuwa na wachezaji wengi ambao wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi na kuliwakilisha vizuri taifa lao.

Kujiamini

Kwa kipindi kifupi ambacho alipata nafasi ya kukaa na wachezaji wa Tanzania na kufanya nao mazoezi, aligundua kwamba, wachezaji wengi wana vipaji lakini wamekosa kujiamini, kama wataligundua hilo wanaweza kucheza soka sehemu yoyote duniani.

Amedai kuwa hilo ni jambo la msingi kwa mchezaji yeyote, kujiamini akiwa uwanjani, kwa kuwa hapo ni sehemu yake ya kazi, kila mmoja anakuwa anamuangalia yeye nini anakifanya, hivyo akikosa kujiamini hawezi kufika kokote.

Kujituma

Adi amedai kuwa, kuna baadhi ya wachezaji wana uwezo mkubwa, lakini wanashindwa kujituma, hasa pale timu yao inapokuwa ipo nyuma na inatafuta bao la kusawazisha, uwezo wa kuchezea soka pekee uwanjani hautoshi, kuna mambo ya ziada ambayo mchezaji anatakiwa kuyaonesha.

Amesema wachezaji wanaweza wakawa na uwezo wa kucheza mpira, lakini timu ikiwa imezidiwa na wao wanakuwa hawana mpango mwingine wa kuweza kuisaidia, hivyo kila mmoja anatakiwa kujituma kwa nguvu kama yupo peke yake uwanjani ili kuweza kuisaidia timu kupata ushindi.

Kulala vizuri

Mchezaji huyo amedai kuwa, mchezaji ili aweze kuwa bora uwanjani anatakiwa kulala vizuri, amesema kama mchezaji atakuwa analala sehemu ya shida au ni sehemu ambayo inaweza kuhatarisha maisha yake, basi anaweza kuwa na wakati mgumu hata uwanjani.

Mchezaji anatakiwa kulala sehemu salama na yenye amani kwa ajili ya kupumzisha vizuri mwili wake na kuweza kujengeka vizuri.

Mazoezi

Suala la mazoezi amedai kuwa wachezaji wengi wakiambiwa na mashabiki wao kuwa wana kiwango kizuri na uwezo mkubwa uwanjani basiw anavimba kichwa na kujisahau.

Wengi wakisifiwa wanapunguza kasi ya kufanya mazoezi kwa kuwa tayari wanajiona wamemaliza, lakini mchezaji huyo amewataka wachezaji wa Tanzania kufanya mazoezi kwa hali ya juu kwa ajili ya kuweza kukuza na kuongeza kiwango chao.

Amesema wachezaji wanatakiwa kwenda Gym kwa mpango maalumu, hiyo itawasaidia kuongeza stamina ili kuweza kupambana wakiwa uwanjani.

Kula vizuri

Hata hivyo, mchezaji huyo amewataka wachezaji wa Tanzania kula vizuri kwa ajili ya afya yao, amedai kuwa kuna vyakula ambavyo wachezaji wanatakiwa kula kwa ajili ya kuongeza nguvu mwilini, hivyo ni bora kufuata ushauri juu ya vyakula gani wanatakiwa kula.

Mchezaji huyo anaamini kuwa, endapo wachezaji hao watayafuata hayo, basi watakuwa na nafasi kubwa ya kucheza soka nje ya Tanzania.

Adi amedai kuna baadhi ya wachezaji kwa sasa wana uwezo wa kucheza nchini England, kama vile Mbwana Samatta, ambaye anakipiga katika soka la kulipwa nchini Ubelgiji katika klabu ya Genk pamoja na Thomas Ulimwengu, ambaye alikuwa anacheza soka la kulipwa nchini Congo katika klabu ya TP Mazembe.

Adi anaamini kuwa ipo siku Tanzania itafanikiwa kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika kama wachezaji wataamua kujitolea kwa ajili ya taifa lao, na yeye yupo tayari kuungana na wachezaji wengine kufanya hivyo kwa ajili ya Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles