27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Heche atangaza kukubali matokeo, aonya wizi wa kura

Na BENJAMIN MASESE-TARIME VIJIJINI

MGOMBEA ubunge Jimbo la Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) amesema yupo tayari kukubali matokeo ya kuzidiwa kura na mpinzani wake, Mwita Waitara (CCM) endapo haki na uwazi utatendeka.

Kauli hiyo aliitoa juzi kwenye mkutano wa uzinduzi kampeni kwenye Jimbo la Tarime Vijijini, uliofanyika Kata ya Sirari ambapo wagombea wengine, Julius Mwita (Musoma Mjini), Ester Bulaya (Bunda Mjini), Ester Matiko (Tarime Mjini), Ezekiah Wenje (Rorya), Catherine Ruge (Serengeti) walihudhuria na kuwataka wananchi kutofanya kosa la kumchagua Waitara kwa kuwa ni msaliti na hana msimamo.

Heche alisema yeye ni muumini mkubwa  wa kutaka haki katika jambo lolote, hivyo anatamani kuona uchaguzi wa mwaka huu ukifanyika kwa amani na upendo hadi  matokeo yatakapotangazwa.

Hata hivyo alisema  anasikitishwa kuona baadhi ya viashiria kutoka kwa watumishi wa umma na jeshi la polisi wakifumbia macho baadhi ya kauli zinazotolewa na wapinzani wake.

“Ndani ya miaka mitano nimefanikiwa kujenga vituo vya afya tisa na hospitali moja inayomilikiwa na halmashauri, ipo pale Nyamwaga, kila shule ya sekondari na msingi nimepeleka saruji, mabati, mbao na misaada kadhaa ambayo yote ililenga kuondoa changamoto kwa wanafunzi wetu.

“Wananchi wa Tarime Vijijini wote ni mashahidi kwa namna ninavyowapambania wananchi, sasa nashangaa mtu mmoja anakuja kusema yeye anafaa.

“Mimi nikishindwa na Waitara kwa haki nitakubali  kusaini na kwenda nyumbani kufanya shughuli zangu, hili nalisema kwa uwazi kabisa maana nimeanza kusikia watendaji wanajigamba kwamba hawawezi kuwatangaza madiwani wa upinzani hata kama wameshinda.

“Kuna vitendo vinatendeka na vinasemwa hadharani lakini polisi wanakaa kimya, nimesikia mtu mmoja anasema nisikanyage Kata ya Kibaso, sasa natangaza kwamba kule nitakwenda nikiwa mwenyewe tena wale wanaonilinda siku nitawaacha nyumbani kwangu, sasa polisi naomba mlijue hilo na mjipange kweli,”alisema.

Heche alisema endapo wananchi watamwamini na kumpa kura za kutosha, atahakikisha barabara za lami zinajengwa katika baadhi ya kata na kuwataka wananchi kumchangua mtu ambaye atakuwa mwakilishi wa wananchi siyo mwakilishi wa Serikali.

Wagombea ubunge waliomsindikiza Heche katika uzinduzi huo, waliwataka wananchi kumpa kura  mgombea urais  wa chama hicho, Tundu Lissu kama  pole ya kupigwa risasi 16 mwilini na kunusurika kifo.

Walisema zawadi pekee kwa Lissu amabye ni mgombea urais  ni kumpa kura za kutosha  zitakazomwezesha kuingia Ikulu na kuleta amani na uhuru kwa Watanzania wote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles