28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Hatukubaliani na uamuzi wa Spika Ndugai

MOJA  ya habari kubwa iliyopewa uzito leo na vyombo mbalimbali vya habari nchini, ni uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai kupiga marufuku waandishi wa habari walioko bungeni kuandika habari za wabunge wa upinzani wanaotoka nje ya ukumbi.

Lakini pia, Spika amekwenda mbali zaidi na kutishia kuwanyang’anya vitambulisho waaandishi wa habari ambao watabainika kuwahoji wabunge kwenye viwanja vya Bunge, jambo ambalo tunaona haliko sahihi.

Kauli hizo za Spika zimekuja wakati ambao Bunge la Bajeti linaendelea na vikao vyake mjini Dodoma, huku  likitawaliwa na mijadala mingi. Mkubwa zaidi ni suala  la Bunge kugoma kufanya kazi na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Assad.

Jambo hilo limekuwa gumzo kubwa kila kona,  Watanzania wanajiuliza maswali mengi ambayo yanahitaji majibu, lakini mpaka sasa hakuna kiongozi aliyetayari kutoa ufafanuzi wa kina juu ya suala hilo.

Kwa kuwa Spika Ndugai ndiye kiongozi mkuu wa mhimili huu, anapaswa kujitafakari vizuri katika uamuzi wake ambao tunaona wazi hauna tija kwa manufaa ya Watanzania.

Tunasema tumesikitishwa na uamuzi huu kwa sababu ni wazi unaingilia uhuru wa wana habari katika kutimiza majukumu yao ya kila siku. Miaka nenda rudi waandishi wa habari wamekuwa wakitimiza majukumu yao kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za eneo la Bunge, lakini imekuwaje  leo hii wawekewe mipaka ya aina hii?

Tunasema hivyo kwa sababu hivi sasa Watanzania wengi hawaangalii bunge  mubashara ‘live’ hivyo waandishi walioko eneo la tukio ndiyo wanapaswa kuueleza umma nini kinachoendelea eneo hilo.

Wabunge wengi waliopo  pale bungeni wanawakilisha  mamilioni ya Watanzania, hivyo wana haki ya kupata habari iwe kupitia radio, magazeti au runinga. Vilevile, dunia ya leo imebadilika wananchi wanaweza kupata habari kupitia mitandao ya   jamii.

Kwa kuwa eneo hili ni la Spika Ndugai na yeye ndiye muamuzi wa kila jambo, tunasema vyombo vya habari vimekuwa mdau mkubwa mno katika kuripoti habari za  Bunge miaka yote, kwa nini kipindi hiki vionekane adui hadi waandishi kutishiwa kuondolewa au  kunyang’anywa vitambulisho vya kazi?

Hatukubaliani hata kidogo na sababu za Spika Ndugai eti waandishi wamekuwa wakiwakimbilia wabunge wa upinzani  wanapotolewa nje ama kutoka nje ya Bunge na kufanya nao mahojiano na kuacha mambo nyeti yakiendelea bungeni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Spika Ndugai alisema kuna baadhi ya wabunge wamekuwa wakitoka nje makusudi na waandishi wa habari wamekuwa wakiwakimbilia.

Wabunge kutoka nje hakuhusiani hata kidogo na waandishi wa habari kwa sababu wao wanatimiza wajibu wao wa kuwapasha wananchi nini kinachoendelea. Mwanahabari ana uhuru wa kuhoji nani na wapi katika mazingira yapi.

Hilo la kusema  wabunge wanaotoka nje wanapewa nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari, hii inatokana na taaluma ya waandishi wenyewe maana wamafundishwa  nini ni habari na nini si habari.

Kwa maana hiyo, Spika Ndugai anapaswa kuwaacha   watimize wajibu wao na yeye aendelee na majukumu yake ya  bunge kwa sababu tunaamini waandishi walioko pale ni watu makini waliotumwa kutimiza kazi zao.

  MTANZANIA  tunamsihi Spika Ndugai katika hili atambue mchango wa vyombo vya habari ambao vimekuwa vikiutoa miaka yote. Hatutapenda hata kidogo kuona mhimili wa Bunge unatofautiana na vyombo vya habari ikizingatiwa ushirikiano ambao umekuwapo miaka yote. Tunamaliza kwa kusema kazi ya waandishi wa habari waachiwe wenyewe watimize majukumu yao. Ndiyo manna tunasema uamuzi huo si sahihi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles