ANDREW MSECHU – dar es salaam
HATMA ya wabunge 23 wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoka Unguja na Pemba itajulikana ndani ya miezi mitatu ya Bunge la bajeti linaloanza leo.
Hiyo inatokana na taarifa kwamba baadhi ya wabunge hao watajiuzulu ndani ya Bunge hili na kumuunga mkono aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye amejiunga na ACT-Wazalendo.
Wabunge hao ambao awali walikuwa wakimuunga mkono Maalim Seif katika mgogoro na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, sasa wanatakiwa kufanya uamuzi kama watabaki CUF ama nao wataondoka.
Hata hivyo, mara kadhaa Maalim Seif amezungumza na umma akisema amewaachia wabunge hao kuamua kama watajiunga naye sasa hivi ama watasubiri hadi muda wao wa ubunge uishe.
Kwa upande wake, Lipumba amekuwa akisema ni wakati sasa wa wabunge hao kujitokeza kwa umma na kuomba radhi kwa waliyofanya nyuma ili waendelee kukijenga chama chao.
Tayari baadhi ya wabunge wa CUF kutoka bara, akiwamo Mussa Mbaruku (Tanga Mjini), Hamidu Bobali (Mchinga) na Selemani Bungara Bwege (Kilwa Kusini) wametangaza kumuunga mkono Lipumba.
Baadhi ya wabunge wengine waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina, walisema ndani ya Bunge la bajeti hatima yao ndiyo inajulikana.
“Mimi nasubiri kamati ziishe, tukirudi bungeni muda wowote nitatangaza kuondoka,” alisema mmoja wa wabunge hao.
Wabunge wa Zanzibar, wanakabiliwa zaidi na shinikizo la kuondoka kutoka kwa wapigakura wao ambao wengi wamejiunga na ACT.
Walio wengi hasa kutoka Pemba, safu za uongozi wao wa majimbo kuanzia ngazi za matawi wamejiunga na ACT, jambo litakalokuwa vigumu kwao kufanya kazi.
Lipumba akizungumzia hatima ya wabunge wanaomuunga mkono Maalim Seif, alisema bado wana fursa ya kueleza msimamo wao hadharani na kuwaomba radhi wanachama ili kuendelea na uanachama wao.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Lipumba alisema wabunge hao wanatakiwa kueleza msimamo wao wakati uongozi wa chama hicho ukiendelea kujipanga kuijenga upya CUF, baada ya kuondoka kwa Maalim Seif.
“Kwa sasa tunawasikiliza msimamo wao mmoja baada ya mwingine. Bado wanapewa fursa hiyo ya kueleza msimamo wao iwapo wanaendelea kuwa kwenye chama au wanaondoka. Kwa walio tayari kubaki, watatakiwa kufuata taratibu za chama.
“Wanatakiwa kuwa wazi. Waeleze utayari wao wa kushiriki kukijenga chama na wataomba radhi kwa wanachama ili kurejesha imani yao kwa chama. Kila mmoja atatakiwa kutekeleza hili, kwa taratibu zetu hili lazima lifanyike kwa uwazi,” alisema.
Lipumba alisema hatua hizo ni muhimu katika kusimamia kujenga chama chao kilichokumbwa na misukosuko ikiwamo hatua ya Maalim Seif na wafuasi wake waliohitimisha kesi zaidi ya 35 dhidi yake kwa kutangaza kuhamia ACT-Wazalendo Machi 18, mwaka huu.
Alisema kwa sasa wanaona hakuna tena ukomo wa muda ila wanahitaji hatua hiyo ichukuliwe mapema na uongozi wa chama unaendelea kuwasiliana na wabunge hao ili kujua misimamo yao iwapo wataendelea kuunga mkono chama hicho au watahama kama walivyofanya wanachama na viongozi wengine waliokuwa wakimuunga mkono Maalim Seif.
Lipumba alisema msimamo huo unawahusu wabunge hao 27 wa CUF ambao walikuwa wakimuunga mkono Maalim Seif katika kipindi cha miaka mitatu ya mgogoro wa kiuongozi.
Awali, wabunge 28 wa majimbo kati yao 22 kutoka Zanzibar, wanne wa Bara na mmoja wa viti maalumu walionekana kuwa na Maalim Seif, huku watatu wa majimbo ya Bara na tisa viti maalumu wakionekana kuwa upande wa Lipumba.
Tayari Profesa Lipumba na wenzake wameshabadili katiba inayompa mamlaka ya kuteua katibu mkuu, na alimteua Khalifa Suleiman Khalifa kuchukua nafasi ya Maalim Seif.
Hadi sasa, kati ya wabunge hao 28 waliokuwa wakimuunga mkono Maalim Seif, ni mmoja tu, Bobali (Mchinga) ambaye ametekeleza masharti hayo, kwa kuomba radhi wanachama katika mkutano wa wazi ulioitishwa na Lipumba Machi 17, huku akieleza msimamo wake kuwa yuko tayari kushiriki kuijenga CUF.
Mvutano huo ulianza baada ya Maalim Seif kutangaza uamuzi wa kuhama CUF na kuhamia ACT-Wazalendo, baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi namba 23 ya mwaka 2016 kuhalalisha uenyekiti wa Profesa Lipumba.
Katika kesi hiyo, Maalim Seif, wabunge na wanachama wanaomuunga mkono walikuwa wakilalamikia hatua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho, ilihali alitangaza kujiuzulu uenyekiti kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Hata hivyo, mwaka 2016 Lipumba alirejea na kudai uenyekiti wake, hatua iliyoibua mgogoro wa kiuongozi uliowagawanya wanachama katika pande mbili, moja ikimuunga mkono Maalim Seif na nyingine Lipumba.
Katika mgogoro huo, wabunge wengi zaidi walijitokeza hadharani kuunga mkono upande wa Maalim Seif, hata kuamua kugharamia zaidi ya kesi 33 zilizofunguliwa Mahakama Kuu na kukodi ofisi mpya za CUF Magomeni, hivyo kumwachia Lipumba ofisi za CUF Makao Makuu Buguruni.