25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Hatima ya Kubenea, Komu kujulikana leo

 

Mwandishi wetu-Dar es Salaam


HATIMA ya Mbunge wa Ubungo Saed Kubenia na yule wa Moshi vijini, Anthony Komu, itajulikana leo baada ya kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kutangaza kikao hicho.

Alisema kitafanyika Dar es Salaam leo na ajenda kuu ni masuala yanayoendelea ndani na nje ya Chama hicho.

“Tutatoa taarifa rasmi juu ya maazimio ya kikao hiki kitakapomalizika,”  ilisema taarifa ya Mrema.

Taarifa hiyo imetolewa  siku chache baada ya sauti zinazoaminika kuwa ni za Kubenea na Komu, kusambaa kwenye mitandao ya jamii wakijadili kuwashughulikia baadhi ya viongozi wa chama hicho.

Kwa mujibu wa sauti hizo, Kubenea na Komu walikuwa wakipanga kumshughulikia Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.

Awali inasikika sauti ikisema; “Boni hana msaada wowote kwenye haya mambo”.

Kisha inasikika sauti nyingine ikisema; “Anao msaada mkubwa sana kwa sababu Boni…ujue ndiyo wamemsambaratisha Waitara.

“Boni ni mjumbe wa kamati kuu, ni msema ovyo, ni mtu ambaye ana misimamo ya vuguvugu lakini anaheshimika.

“Kuna watu wanamchukulia kama ni mpiganaji, ni mtu mwenye msimamo ambao ndiyo hao wanampa uhalali Mbowe. Ukimuondoa Boni umempiga sana Mbowe, sana yaani.

“Unajua viko vitu vya msingi vya kufanya, ku – deal na Mbowe ni kwenye mambo ambayo ni halali”.

Hata hivyo baadhi ya watu wa karibu na Komu walidai   mbunge huyo alituma kwa makosa sauti hiyo katika kundi la WhatsApp la Kaskazini bila kujua.

Moja ya ‘screen shots’ kutoka katika kundi hilo la WhatsApp ambayo MTANZANIA imeiona,  inaonyesha sauti hiyo ilitumwa juzi saa 12:03 jioni.

Hata hivyo wabunge hao walipoulizwa walikana kuhusika na sauti hizo na kudai kuwa zimetengenezwa kwa lengo la kuwachafua.

KUBENEA

Kubenea alisema sauti hiyo si yake na kudai kuwa kuna watu wanaendeleza mchezo wa kuwachafua wenzao.

“Yaani watu wanatengeneza vitu vyao kwa ajili ya kuchafua watu, mimi hiki kitu sikijui na kimetengenezwa na inaonekana watu wako kazini kuendeleza mchezo wao ule ule wa kuchafua watu,” alisema Kubenea.

Kubenea alizihusisha sauti hizo na harakati za uchaguzi ndani ya chama hicho na uchaguzi mkuu wa 2020.

“Kuna uchaguzi ndani ya chama na watu wanajipanga kwa ajili ya 2020 na kuna makundi.

 

“Watu wanahitaji ubunge, urais, uongozi kwenye chama, hivyo sisi tunaamini ni makundi tu ndani ya chama,” alisema.

Alisema watu hao ni wale walioshiriki hata kutengeneza sauti za kumchafua Mwenyekiti wao wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza  na aliyekuwa mwanachama wa chama hicho, Wema Sepetu, mwaka mmoja uliopita.

“Hawa wanaochafua wenzao kupitia sauti za kutengeneza nahisi wana ajenda yao ya siri iliyojificha. Na kama ni hivyo, je na sauti ya wakati ule iliyotengenezwa  kumchafua mwenyekiti je watu pia waamini?

“Kama kuna watu wanataka kufanya siasa ni vema wafanye kwa ustaarabu na si kuchafua wenzao kwa malengo ovu wanayoyajua wao

 

KOMU

Naye  Komu alisema si mmojawapo wanaosikika katika sauti hizo.

Alisema sauti hizo zinachanganya na hakumbuki mahali ambako alizungumzia  vitu hivyo kwa mtiririko huo.

“Inawezekana kuna analysis (uchambuzi) tulikuwa tunafanya mahali mtu akachukua… mimi sielewi… akaenda aka – edit (kuhariri).

“Na nimeona wameitengenezea kwamba tulikuwa kwenye press conference (mkutano na waandishi wa habari) hali ambayo ni siasa tu za kutengenezwa.

“Siwezi kujua malengo yao ‘unless’ hao waliotengeneza wanaweza kujua wana malengo gani kwa sababu imekuwa kama maigizo yaani inaleta fedheha kabisa,” alisema Komu.

Alipoulizwa kama anatofautiana  na Mwenyekiti Freeman Mbowe katika jambo lolote, Komu alisema hana tatizo wala tofauti naye na hajawahi kugombana naye hivyo haoni shida iko wapi.

“Kama ni hivyo wanaweza wakasema ni wapi mimi nimekaa nikasema nataka sasa mabadiliko kwenye chama, hatumtaki Mbowe.

“Unajua sisi katiba yetu iko wazi, ukifika wakati wa uchaguzi wa mwenyekiti wa chama tunacho kipindi maalumu cha kutangaza nia hadi uchaguzi wenyewe.

“Kwa hiyo niseme tu hizo ni propaganda za watu wanaotaka kutimiza malengo yao ambayo mimi siyajui.

“Boni mimi natoka naye wapi?  Yaani Boni ni kijana mdogo sana, yeye ni Meya wa Ubungo na mimi Mbunge wa Moshi Vijijini, nakutana naye wapi?

“Yaani tuna masilahi gani tunayopigania mimi na Boni, sina nia na jimbo lake… sijui udiwani wake au umeya wake, mimi natoka naye wapi?” alihoji Komu.

Hata hivyo Komu alisema ana muda mrefu, zaidi ya mwaka mmoja, hajawahi kuzungumza na meya huyo au kuonyesha katika maongezi yao kuwa wamehitilafiana  kwa sababu hawana ukaribu wa namna hiyo.

“Kwa hiyo mimi nimepuuza tu lakini kuanza kuingia kwenye mitandao kujibu wala sina hiyo tabia,” alisema.

MEYA JACOB

Alipoulizwa kuhusu sauti hizo, Jacob alisema amezisikia na tayari amechukua hatua za kukiarifu chama chake na mamlaka nyingine.

“Nimezisikia hizo sauti na nimeshaarifu mamlaka mbalimbali.

“Kwanza nimekiarifu chama na mamlaka nyingine kwa ajili ya kufanya uchunguzi,” alisema Jacob.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles