KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
RUFAA iliyokatwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Esther Matiko imepingwa mahakamani na Jamhuri wameomba itupwe kwa sababu kifungu kilichotumika kuifikisha Mahakama Kuu hakiko sahihi.
Hayo yaliibuka jana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Sam Rumanyika wakati rufaa hiyo ilipotakiwa kuanza kusikilizwa na Jamhuri wakawasilisha pingamizi.
Akiwasilisha hoja za kupinga rufaa huyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Dk. Zainabu Mango alidai vifungu vya sheria walivyotumia kuwasilisha rufaa si sahihi hivyo aliomba rufaa hiyo itupwe.
Alidai walitakiwa kuwasilisha rufaa chini ya kifungu cha sheria namba 359 na 361 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai.
“Kukosekana kwa vifungu hivyo kunaifanya rufaa kukosa uhalali wa kuwepo mahakamani, “alidai.
Wakili wa Serikali Simon Wankyo akiwasilisha hoja za pingamizi pia alidai mwenendo wa kesi uliofikishwa mahakamani haujakamilika na haujachapwa hivyo hausomeki vizuri kwani kuna maneno yamekatika na mwandiko wa hakimu hausomeki vizuri katika baadhi ya maeneo.
Alidai mwenendo huo huwezi kusoma ukaelewa kwa ukamilifu kwani kuna maneno yamekatika.
Wankyo alidai walitakiwa kupata nyaraka hizo zikiwa kamilifu ili kufanya maandalizi ya kutosha.
“Tulitaarifiwa kwamba mwenendo wa kesi uko katika hatua ya mwisho hivyo tulitegemea tuzipate zikiwa zimechapwa ili ziweze kusomeka vizuri, “alidai.
Naye Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai bila kuwa na mwenendo wa kesi uliochapwa wanaona haki ya kikatiba haitatendeka.
Akijibu Wakili wa Warufani, Peter Kibatala alidai hoja za wajibu rufani hazina msingi wala mashiko kwa sababu notisi ya kukata rufaa inaweza kutolewa kwa mdomo ama kwa maandishi.
Kibatala alidai hakuna mahali ambapo walieleza kifungu cha sheria wakati wakitoa notisi ya kukata rufaa.
Wakili Kibatala aliendelea kudai kwamba suala la mwenendo wa kesi kuwa haujachapwa lilishatolewa uamuzi juzi na Jaji Rumanyika na wakakubali ziletwe kama zilivyo.
Alidai mahakama ilitoa haki ya kusikiliza pande zote mbili katika suala la mwenendo wa kesi.
Kibatala alisema rufaa yao ina msingi inalindwa na Katiba na sheria ya nchi, upungufu uliotajwa hauwezi kuiondoa rufaa.
Warufani waliomba rufaa isikilizwe ili washtakiwa wapate haki yao ya kikatiba ya kuwa nje kwa dhamana.
Jaji Rumanyika baada ya kusikiliza hoja zote jana aliahirisha kesi hadi léo kwa ajili ya kutoa uamuzi wa pingamizi la Jamhuri la kutaka rufaa itupwe.
Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana Ijumaa iliyopita katika kesi ya jinai Namba 112 imayosikilizwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Walifutiwa dhamana kwa madai kwamba hawakufika mahakamani kuhudhuria katika kesi yao Novemba 8 mwaka huu na taarifa za kutokuwepo zilikinzana.