23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Hati fungani: Njia rahisi kutajirika zaidi ya ujasiriamali

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SERIKALI  kupitia Mamlaka ya Masoko ya Dhamana na Mitaji nchini (CMSA), iliyo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, imekuwa na kazi ya kuhamasisha jamii kutambua manufaa ya ununuaji wa hati fungani kutoka katika taasisi mbalimbali.

Hiyo ni moja ya mbinu nzuri za kujiwekea akiba, kupata faida na kutajirika.

Kutokana na umuhimu huo, ikiwa wajasiriamali na wananchi nchini wataendelea kujenga tabia ya kuweka akiba zao kwa kununua hisa katika kampuni mbalimbali za kibiashara, wataweza kutajirika kwa njia ya kupata gawio kila mwaka, baada ya kampuni husika kupata faida na kugawa faida kwa wanahisa wake.

Fursa hiyo ni muhimu kwa wafanyabiashara na wanachi wanaonunua hisa katika kampuni za kibiashara, kufuatilia mwenendo wa bei za soko la hisa ili kutambua ni wakati upi bei imepanda ili wauze na kupata faida, ikiwa ni moja ya mbinu ya kujiongezea faida.

Faida za kuuza hisa ni kwamba, kampuni husika hupata mtaji wa kuendesha na kupanua shughuli za uwekezaji wakati huo huo mnunuzi wa hisa anapata faida ya kuwa sehemu ya wamilki wa kampuni hiyo na kupata faida kutoka katika fedha aliyowekeza bila yeye kuhangaika kufanya kazi.

Mbali na gawio la faida ya kila mwisho wa mwaka baada ya kampuni kupata faida, mmiliki wa hisa anaweza kuuza hisa zake muda wowote na kupata faida baada ya kugundua kuwa kipindi hicho hisa za kampuni husika zimepanda bei katika soko la hisa.

Moja ya taasisi ambazo zimekuwa zikipata mafanikio ni Benki ya NMB, ambayo hivi majuzi ilitangaza matokeo ya mauzo yake ya toleo la tatu la programu ya hati fungani, ikisema imekusanya Sh bilioni 83.3 sawa na asilimia 333 ya mauzo yaliyotarajiwa awali ya Sh bilioni 25.

Mauzo ya toleo la tatu la hati fungani ya NMB yalifunguliwa Juni 10 na kufungwa Julai 8, mwaka huu.

Kipindi hicho cha miezi miwili, kilikuja baada ya Mamlaka ya Masoko na Mitaji na Dhamana (CMSA) kutoa idhini ya mauzo hayo.

Akizungumzia  hilo katika hafla ya kutangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa NMB, Ruth Zaipuna, anasema wanajivunia kiwango hicho cha mauzo, kinachothibitisha imani ya wananchi na jamii kwa benki yao.

Zaipuna anabainisha kuwa tayari NMB imeyapokea na kuyakubali maombi yote, na tayari waombaji wa manunuzi wametaarifiwa kuorodhesha hati fungani zote, kabla ya wanunuzi kukabidhiwa vyeti mwezi ujao.

Anafafanua kuwa mauzo hayo ya kiwango cha juu kuliko walivyotarajia, yanaiongezea benki nguvu ya kiuchumi katika kufanikisha utoaji wa mikopo kwa wateja wao na kwamba mchakato mzima umeshirikisha zaidi ya matawi 200 kote nchini.

“NMB inatoa shukrani za dhati kwa taasisi zote zilizofanikisha uuzwaji wa toleo la tatu la hati fungani ya NMB, ikiwamo CMSA, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mshauri Kiongozi wa NMB, Stanbic Bank Tanzania Ltd na Dalali Mfadhili wa NMB, Orbit Securities Company Ltd,” anasema Zaipuna.

Hati fungani ni aina ya uwekezaji unaomwezesha mteja kuwekeza fedha katika taasisi (hasa shirika la kibiashara au Serikali), kwa kuikopesha fedha kwa muda maalumu na kwa riba isiyobadilika. Riba ya hati fungani za NMB kwa mwaka ni asilimia 10.

“Mteja anaponunua hati fungani ya NMB, anakuwa ameikopesha benki, ambayo inaahidi kurejesha fedha zake (msingi) katika kipindi maalumu cha ukomavu – kuanzia muda uliowekeza hadi muda wa ukomavu ambao unakuwa miaka mitatu,” anasema.

Hati fungani za NMB zimekuja kwa ajili ya watu wenye kipato cha chini wanaoweka akiba kiasi na hawaitumii hadi muda waliojipangia au dharula inapotokea.

Kuna watu wanasema kuliko kupata hiyo faida kwa mwaka akiweka Sh milioni moja  ni bora akafanyie biashara apate faida zaidi, kumbe kwa kutokujua anaweza kupata faida mara dufu kupitia uwekezaji wa hati fungani.

Kwa kiasi kidogo tu cha uwekezaji cha Sh 500,000 unapata faida ya asilimia 13 kwa mwaka kwa muda wa miaka mitatu ambapo faida hii hulipwa mara mbili kwa mwaka, bila kusahau kuwa bondi itakapo komaa, NMB hulipa fedha iliyowekezwa awali.

Hati fungani ya NMB walengwa wakuu ni wawekezaji wadogo na wakati, japo hata wakubwa na ni tofauti na uwekezaji wa kampuni nyingine hivyo, Watanzania wanaaswa kuchangamkia fursa hii muhimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles