Na PATRICIA KIMELEMETA- DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, Zacharia Hanspope, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mawili.
Hanspope alifikishwa mahakamani hapo jana saa 3:30 asubuhi baada ya kukamatwa juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA), wakati anarudi kutoka Marekani kutibiwa.
Kesi hiyo ilisikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, huku upande wa Serikali uliwakilishwa na Wakili Shadrack Kimaro na upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Augustine Shio.
Wakati kesi hiyo ikiendelea mahakamani hapo, mvutano wa kisheria uliibuka baada ya upande wa Serikali kutaka mshtakiwa huyo aunganishwe kwenye kesi inayowakabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange ‘Kaburu’.
Hata hivyo, upande wa utetezi ulipinga hoja hiyo kwa madai kuwa mahakama ilishatoa uamuzi kesi hiyo iendelee kwa washtakiwa waliopo mahakamani, hivyo ombi hilo ni sawa na kesi hiyo kuirudisha nyuma.
Baada ya mvutano huo wa kisheria, Hakimu Simba alimuunganisha Hanspope kwenye kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili Aveva na Nyange huku akisomewa mashtaka mawili na wenzake 10.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Kimaro alieleza kuwa Hanspope anakabiliwa na mashtaka mawili, kuwasilisha nyaraka za uongo na kughushi.
Mashtaka mengine yanayowakabili washtakiwa wenzake ni pamoja na kula njama, kutoa nyaraka za uongo, matumizi mabaya ya madaraka, kughushi, utakatishaji, kuwasilisha nyaraka za kughushi na kuendesha biashara bila kufuata sheria.
Katika shtaka la utakatishaji fedha linalomkabili Aveva, anadaiwa Machi 15, 2016 katika Benki ya Baclays Mikocheni, Dar es Salaam, alijipatia Dola za Marekani 187,817, takribani Sh milioni 400 wakati akijua zimetokana na kosa la kughushi.
Katika shtaka la kughushi linawakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa katika tarehe hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya dola 40,577, zaidi ya Sh milioni 90 huku wakijua kwamba si kweli.
Pia katika shtaka jingine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Marekani 40,577.
Hata hivyo, shtaka la mwisho halikusomwa kwa sababu linamhusu mshtakiwa 4 Franklin Lauwo ambaye bado hajafikishwa mahakamani.
Hanspope anatetewa na Wakili Augustine Shio ambaye aliieleleza mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo alikuwa Marekani kwa ajili ya matibabu, lakini aliamua kukatisha matibabu hayo ili arudi nchini kusikiliza tuhuma zinazomkabili.
Wakili huyo alieleza kuwa aliandikiwa barua na Hanspope ili aitaarifu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwamba anarudi Oktoba 15, 2018.
Wakili Shio alieleza kuwa aliwafikishia ujumbe Takukuru, ambapo usiku wa Oktoba 15, 2018 saa 7:25 usiku Hanspope alirudi na alipofika uwanja wa ndege walimkamata, lakini baadaye walimruhusu alale nyumbani kwake na kisha asubuhi wakamfikisha mahakamani.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba alitoa masharti ya dhamana kwa Hanspope ya kuwa na wadhamini  wawili watakaosaini bondi ya Sh mil 15 kwa kila mmoja, ambapo alitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana huku wenzake Aveva na Nyange wakiendelea kusota mahabusu.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 19, 2018 itakapotajwa tena