25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

HAMAR: KABILA AMBALO WANAWAKE HUPENDA KUCHAPWA KIKATILI

 

 

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA YA HABARI

WIKI mbili zilizopita katika safu hii tulikuja na makala inayohusu utamaduni wa wanaume kuwabeba wake zao nchini Finland tukieleza kuwa ni moja ya tamaduni za kushangaza zinazoendelea hadi leo hii.

Kwamba katika sayari hii iwe kwenye mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea bado kuna tamaduni za kushangaza, kuchekesha au kusikitisha na kuhuzunisha hata katika zama hizi za sayansi na teknolojia.

Leo hii kwa mara nyingine tunakuja na utamaduni mwingine wa ajabu ambao bado ungalipo hadi sasa.

Kutoka hapa tulipo tunasafiri kwa ndege umbali wa maili 1,139 hadi kusini mwa Ethiopia, katika Bonde la Mto Ommo, linalopakana na mataifa ya Kenya na Sudan Kusini.

Katika eneo hilo lililotanda kutoka mji mkuu wa Ethiopia kuelekea Ziwa Turkana linalopakana na Kenya zinaishi jamii mbalimbali, ambazo nyingi bado zipo katika vijiji vya kienyeji vya zama zile za kale hata kabla ya kuingia kwa ustaarabu.

Hata hivyo, katika eneo hilo wengine wamehamia maeneo ya mijini ikiwamo Addis Ababa katika kile kinachoonekana kufumbuka macho kuhusu uwapo wa dunia nyingine mbali ya hiyo yao ya gizani pamoja na kusaka malisho bora zaidi.

Miongoni mwa jamii hizo ni Kabila la Hamar lenye wakazi 20,000 katika ukanda huo wenye utajiri wa rutuba na wingi wa mifugo, ambayo inaabudiwa mno hasa ng’ombe.

Kikubwa cha ajabu katika kabila hili ni kitendo cha wanawake kuruhusu kuchapwa fimbo au mijeredi kikatili mno na wanaume.

Wakati kichapo kikiendelea, badala ya wanawake hawa kukimbia ndio bado huchochea moto zaidi kwa kuwabembeleza wachapaji wao kuendelea kuwatandika tena na tena.

Hilo hutokea katika maisha ya kila siku na kuonekana hadharani wakati wa sherehe za jando, ambazo wanawake wenye umri mdogo hushuhudiwa wakichapwa ili kuonesha walivyo tayari kujitoa muhanga kwa wanaume.

Ng’ombe ni kitu muhimu mno kwa jamii ya Hamar, ushahidi ni uwapo wa maneno tofauti 27 yanayoeleza rangi ya ng’ombe kwa lugha ya kabila hilo.

Kabila hilo linaamini kuwa alama za makovu yanayotokana na vichapo hivyo ni ishara ya uwezo wa mwanamke kutoa pendo lote kwa waume zao.

Na humhakikishia ‘bima’ wanawake watakaojikuta katika matatizo ikiwamo ujane au njaa katika siku za usoni.

Kwamba hilo likitokea katika siku hizo za mbeleni watawageukia wale wanaume waliowachapa zama zile za ujana huko nyuma wajaribu kukumbuka makovu hayo na hivyo wawasaidie utatuzi wa shida zao.

Hivyo, inakuwa ngumu mno kwa mwanamume kukataa kumsaidia mwanamke huyo aliye katika uhitaji, shida au dharura.

Wanawake wanachapwa kama sehemu ya kutoka ujana kwenda utu uzima kwa wavulana, wakati wanafamilia wanawake wanapotangaza penzi lao kwa kijana wa kiume aliye katikati ya sherehe hizo. 

Baada ya sherehe, mvulana anakuwa mwanamume kamili, na anaruhusiwa kuoa. 

Utamaduni huo wa kikatili hujulikana kama Ukuli Bula na ulikutwa na mpiga picha wa Daily Mail, Jeremy Hunter.

Badala ya kukimbia, wanawake huwaomba wanaume kuwachapa tena na tena wakati wa sherehe hizo zinazofanyika katika bonde hilo la Mto Omo. 

Wanawake wa Hamar huvaa mitindo ya namna nyingi ikiwamo mavazi kutokana na ngozi ya mbuzi zilizonakishiwa kwa shanga zinazotokana na majani, huku nywele zao zikifunikwa kwa mchanganyiko wa grisi na udongo mwekundu.

Kwa wanaume, mitindo ya uvaaji wao ni ya kawaida isipokuwa upakaji rangi katika nyuso zao ambazo alama huonesha hadhi zao au upandaji wa ngazi ya kijamii.

Kufikia uanaume, wavulana wa Hamar hupitia taratibu mbili za sherehe za jadi: jando na kuwaruka ng’ombe dume.

Wakati wa mchakato wa kutoka ujana kwenda utu uzima. Wanawake huimba kwa vigeregere na shangwe, wakitangaza penzi lao kwa kijana huyo na nia yao ya kutaka wapate makovu kwa kutandikwa naye.

Huipaka miili yao kwa jibini kupunguza makali ya kichapo, ambacho huendeshwa tu na Maza – yaani wale wavulana waliopitia tayari jando.

Baadhi ya utandikaji huwa wa wenye huba lakini mwingineo huwa wa kikatili.

Lakini mara wanapochapwa, wasichana hawa ambao hawaruhusiwi kupiga kelele au kulia, katika hali ya kujivunia huonesha makovu yao kwa ufahari mkubwa– kama ushahidi wa ushupavu na uadilifu wao.

Hii ni aina ya sera ya bima ya kuja kuwasaidia hapo baadaye.

Hilo linalenga kubaini iwapo mvulana wa Hamar yu tayari kwa mruko wa kijamii kutoka ujana kwenda utu uzima.

Baada ya kufanikiwa kumruka ng’ombe dume – daima wakiwa watupu – mvulana wa Hamar, sasa anakuwa mwana jamii aliyepevuka – anaweza kuoa. Wakati wa hilo, anatarajiwa kukabidhi zaidi ya ngombe 17.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles