26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 6, 2024

Contact us: [email protected]

HAMAHAMA YA WABUNGE INATISHIA UKUAJI WA DEMOKRASIA

KITENDO cha mbunge kuhamia chama kingine huku akijua kuwa kufanya hivyo kutamfanya akome kuwa mwakilishi wa wananchi wa jimbo husika kinaweza kutafsiriwa ni usaliti kwa wapigakura wake, kwa kuwa sababu wanazokuwa wakizitoa wabunge hao wanaohama hazitoshelezi.

Kwanza alianza Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, aliyedai kuondoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kudai kutoridhishwa na baadhi ya mambo serikalini na akapigia chapuo hoja ya upatikanaji wa Katiba mpya.

Pia wakati Watanzania wakiendelea kumshangaa aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia, aliyeachana na ubunge wake hivi karibuni na kuhamia CCM, wiki hii tena kambi ya upinzani imekumbwa na dhoruba baada ya Mbunge wa Siha (Chadema), Dk. Godwin Mollel, kutangaza kujiuzulu ubunge na kuhamia CCM.

Wanasiasa wote waliohama upinzani na kuhamia chama tawala hivi karibuni wamedai wanafanya hivyo baada ya kuridhishwa na utendaji wa Rais Dk. John Magufuli, unaolinda rasilimali za umma na kupiga vita vitendo vya rushwa na ufisadi kwa vitendo. Dk. Mollel amedai anahama ili kwenda kuungana na Magufuli kupigania rasilimali za nchi pamoja na kupigania Wilaya ya Siha kupata maendeleo.

Lakini Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alimponda Dk. Mollel na kusema mtu hawezi kusema anaweza kulinda rasilimali kwa kuondoka bungeni.

Sisi wa MTANZANIA Jumamosi pia tunajiuliza, kama wanaunga mkono utendaji wake, kwanini wasifanye hivyo wakiwa katika kambi ya upinzani, kwa sababu hata Magufuli mwenyewe amekuwa akisisitiza kuwa, maendeleo hayana vyama.

Tunajiuliza je, kuna ulazima gani wa kuhama na kuyaacha majimbo wazi?

Kwa sababu wimbi la wanasiasa wa kuhamia CCM linaleta hisia miongoni mwa watu kwamba, pengine wapinzani hao ‘wamenunuliwa’, ingawa madai hayo hayajathibitishwa bado na kama ni kweli, basi wanasiasa wa namna hiyo hawafai kuaminiwa tena katika jamii.

Kwa sababu wabunge kuachia majimbo yao kutasababisha kuwapo kwa uchaguzi mdogo utakaotumia fedha nyingi na kupoteza muda wa wapiga kura.

Pia fedha zitakazotumika katika uchaguzi mdogo wa marudio zingeweza kutumika katika shughuli za huduma za jamii kama afya, barabara na elimu na hao waliohama watambue kwamba, wanaitia hasara nchi.

Pia tunaamini kwamba, moja ya sababu za kulazimika kuitisha uchaguzi mdogo wa ubunge ni iwapo mbunge atafariki dunia na sababu nyingine yatupasa kuhoji kwamba, kama hii hamahama ya wabunge isipodhibitiwa, itaendelea kututia hasara na kufifisha demokrasia.

Tunaona wakati umefika sasa kwa Bunge kukaa na kutafakari kutunga sheria itakayozuia wabunge kujiuzulu ubunge baada ya kujitoa katika vyama vyao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles