27 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

HALMASHAURI ZATAKIWA KUSIMAMIA SHERIA ZAKE

WENYEVITI na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoani Kagera, wametakiwa kusimamia sheria za mamlaka zao za ukusanyaji wa mapato na kuwatoza ushuru wafanyabiashara wa mazao ili waweze kupata fedha za kuendesha miradi yao.

Ilielezwa kuwa ukusanyaji wa mapato katika halmashauri za Mkoa wa Kagera umedorora na kusababisha baadhi yake kupata hati yenye shaka kwani halmashauri kama ya Ngara ilitegemea tozo ya kulipia ushuru tani moja kwa wanaosafirisha mazao nchini ambayo ilifutwa kwa agizo la Rais Dk. John Magufuli la kufuta tozo zinazokera wananchi.

Akizungumza katika kikao cha Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) kilichofanyika juzi wilayani Muleba, Mwenyekiti wa CCM mkoani Kagera, Costansia Buhiye, alisema halmashauri nyingi zimekosa fedha baada ya kufutwa kwa baadhi ya vyanzo vya mapato.

Buhiye alisema kitendo cha kufuta tozo na ushuru ambao ulitajwa kuwa ni kero kwa wananchi, kimesababisha baadhi ya huduma kukabiliwa na  upungufu wa fedha za uendeshaji, licha ya wananchi kufurahia kuondoa ushuru huo, bado wataathirika kwa kutopatiwa huduma bora kwa wakati kwenye maeneo yao.

Aidha alisema halmashauri za mkoa huo zinaunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kuwaondoa kazini watumishi wasiokuwa na sifa wakiwamo wenye vyeti vya kughushi, lakini hana budi kuchukua hatua za haraka kuajiri wengine wapya kupunguza changamoto na athari zilizoanza kujitokeza.

“Idara ya Afya kila halmashauri inakabiliwa na uhaba wa watumishi, ikifuatiwa na Idara ya Elimu… Idara hizo zinatoa huduma kila kukicha zikiwa na idadi kubwa ya wateja ambao ni wagonjwa na wanafunzi,” alisema Buhiye.

Akizungumzia athari ya tetemeko la ardhi, alisema Serikali inapaswa kuwasaidia wawekezaji ambao watauza vifaa vya ujenzi kwa gharama nafuu kwa waathirika ambao wanazidi kuhangaika katika kurudisha makazi na miundombinu yao katika hali yake ya kawaida.

Wajumbe wa kikao hicho walipendekeza Serikali kutenga fedha za kuwalipa posho za utendaji kazi wenyeviti wa vitongoji, vijiji na mitaa kote nchini kwani wanafanya kazi katika mazingira magumu ya kusimamia usalama na amani sambamba na kuhimiza upatikanaji wa maendeleo ya wananchi.

Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (Chadema), alisema wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoani humo, wanatakiwa kusimamia sheria za ukusanyaji wa mapato na kuunganisha nguvu za pamoja kukuza uchumi.

  • Alisema Serikali imeunda chombo cha kusimamia ujenzi wa barabara za halmashauri (Tarula), lakini kupitia Jumuia ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, wajumbe wake wanatakiwa kuisimamia na kuishauri Serikali, kwamba miongoni mwa wasimamizi wa chombo hicho watoke kwenye Baraza la Madiwani
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles