25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Halmashauri ya Same kikaangoni

Na Jonas Mushi, Dar es Salaam

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imewaweka kikaangoni watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kwa uzembe na kufanya kazi kwa mazoea.

Jana, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Monica Kwiluhya na Mwekazina wake, Antonia Ndawi, walijikuta wakiomba radhi kila mara kutokana na upungufu kwenye ripoti ya hesabu zao.

Akitoa maagizo kwa Halmashauri hiyo, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Abdallah Chikota alisema umegundulika udhaifu katika utendaji na kutoa maagizo sita kwa Halmashauri hiyo.

Kamati ilimtaka mkurugenzi kuandika barua ya kuthibitisha utekelezaji wa maagizo hayo.

“Kamati imebaini changamoto ya watendaji wa halmashauri kufanya kazi kwa mazoea na wamesababisha kushindwa kutekeleza miradi mbalimbali,” alisema Chikota na kuongeza:

“Kamati imebaini kuwa halmashauri imekuwa haipeleki vijijini asilimia 20 ya fedha inazopata  kutoka serikali kuu na hivyo kuwa na deni la Sh milioni 77.2 kwa miaka minne tangu 2010 hadi sasa.

“Pia Sh milioni 280 za mfuko wa vijana na wanawake ambayo ni asilimia 10 ya mapato ya ndani hazikupelekwa kwenye mfuko huo kwa miaka miwili (2012/13 na 2013/14)”.

Kamati pia ilibaini kuwapo  kiasi kikubwa cha fedha zinazobaki wakati wa kufunga hesabu za mwaka huku miradi ikiwa haijatekelezwa.

Kamati ilibaini kuwapo kwa makisio madogo ya mapato na kwa mwaka ujao wa fedha halmashauri imepanga kukusanya Sh bilioni 2.2 lakini kamati iliagiza ikusanye Sh bilioni 2.5.

Kutokana na hali hiyo, kamati iliagiza halmashauri iandae mpango mkakati wa kupeleka deni la Sh milioni 77.2 kwenye vijiji husika pamoja na madeni mengine yote ya watumishi wake.

“Kamati imeshindwa kujiridhisha na fedha za bakaa na tunataka iandae upya mchanganuo wa fedha hizo kwa sababu ni fedha za serikali hivyo fedha hizo zitumike kwa miradi ambayo haikukamilika,” alisema Chikota.

Kamati pia ilibaini uzembe wa kutofunga akaunti 38 za TASAF ambazo zilitakiwa kufungwa tangu mwaka 2013 kwa maelekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) baada ya kukamilika   miradi yake.

Kutokana na hali hiyo kamati iliagiza halamashauri hiyo kuhakikisha akaunti hizo zinafungwa hadi kufikia Juni mwaka huu  kuepusha makato ya benki kutokana na akaunti hizo kuwapo.

Ilimtaka Kiluhya kuandika barua ya kujizatiti kuwa atatekeleza maagizo hayo kwa kamati na kupeleka nakala kwa CAG.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles