Na Safina Sarwatt, Mwanga
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, imeweka mikakati ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka Sh bilioni 3.1 kwa mwaka hadi kufikia Sh bilioni 9.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Salehe Mkwizu amesema hayo jana Desemba 20, huu wakati akizungumza na wandishi wa habari Moshi.
“Halmashauri ya Mwanga imechukua juhudi mbalimbali za kuhakikisha kwamba inaibua vyanzo vipya pamoja na kuviimarisha vyanzo vingine vilivyopo ili tuweze kuongeza nguvu zaidi za ukusanyaji na ufuatiliaji wa mapato haya,”amesema Mkwizu.
Mkwizu ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Shighatini(CCM), ambaye aligombea nafasi ya udiwani katika kata hiyo, kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu na kushinda kwa kishindo amesema halmashauri ya Mwanga kwa sasa inakusanya mapato ya Sh bilioni 3.1, kwa mwaka na kwamba mkakati wake wa miaka mitano ni kufikisha bilioni 9.
“Nimeingia kwenye halmashauri hii nimeikuta inakusanya mapato ya Sh. bilioni 3.1, mkakati wangu kwa kushirikiana na Madiwani pamoja na Wataalamu wa halmashauri ni kupandisha mapato hayo kutoka Bilioni 3.1 kwa mwaka hadi kufikia bilioni 9.
“Sisi Wilaya ya Mwanga tumejipanga vema kuhakikisha tunaongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutumia vyanzo vyetu vilivyopo ili kuweza kufikisha huduma za msingi kwenye jamii,”amesema Mkwizu.
Amefafanua kuwa kwa kushirikiana na Wataalamu wa halmashauri hiyo, watajikita katika kuhakikisha kwamba mapato yanayotokana na Uvuvi, Kilimo na Madini yanakwenda kuongeza makusanyo ya ndani ili yaweze kuipatia fedha nyingi halmashauri hiyo.
“Baraza la Madiwani wa Mwanga, tunayo mikakati mbalimbali ambayo tumejiwekea moja wapo ni mpango wa kuanzisha Utalii wa ndani kwa kulitumia Bwawa la Nyumba ya Mungu pamoja na Ziwa Jipe,”amesema.
Amesema uwepo wa vyanzo vingi vya mapato kimsingi vitasaidia kuongeza makusanyo na hivyo kukuza mapato yake ya ndani ambapo halmashauri itaweza kujitegemea na kutekeleza miradi mbalimbali , ikiwemo kuimarika kwa huduma za kijamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mwanga, Zefrin Lubuva amesema wilaya ya Mwanga inazo fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo Madini ya ujenzi, Mifugo, Uvuvi pamoja na Kilimo cha umwagiliaji.
Lubuva amewataka wataalamu wa halmashauri hiyo kutumia elimu yao kutafuta na kubuni vyanzo vipya vya mapato vitakavyosaidia halmashauri hiyo kutekeleza mipango yake ya maendeleo badala ya kusubiri ruzuku kutoka serikalini.