24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Halmashauri ya Muleba yatoa mkkpo wa milioni 558 kwa makundi maalum

Renatha Kipaka, Muleba

Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa sura ya 290 kifungu cha 37A(1-4) kinaeleza kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zitatenga asilimia kumi (10%) ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwezesha vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

Katika kutekeleza hilo, kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/22 ambayo ni Oktoba hadi Desemba, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba imetoa mkopo wa fedha Sh milioni 558.63 kwa vikundi 70 vya akina Mama, 15 vya Vijana na 10 vya watu wenye Ulemavu.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa wilaya ya Muleba, Toba Nguvila, amewasihi vikundi vilivyopokea mkopo huo, kutumia fedha hizo zilizotolewa kufanya kazi iliyopangwa kama ambavyo wameelimishwa na wataalamu kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii na maafisa kutoka benki ikiwa ni pamoja na kukuza mitaji na biashara zao.

“Serikali imeona uhitaji wa kuwezesha jamii ikaamua kutoa mikopo isiyokuwa na riba. Mikopo hii mliyokopeshwa mtaanza kurejesha baada ya siku 90 yani miezi mitatu hivyo nawasihi fedha hii mliyokopeshwa muende kufanyia biashara na shughuli za ujasiriamali iwe ni ufugaji, iwe ni uvuvi ama ufundi na shughuli zingine za kimaendeleo ili muinue vipato vyenu na kukuza uchumi wa Taifa letu,” amesema Nguvila.

Pia, amewaasa kuzitumia fedha hizo kuwatoa kwenye hali ya chini kwenda kwenye hali ya kati na hata ya juu ya kiuchumi lakini pia amewasisitiza kutozitumia fedha hizo kwa ajili ya kununua nguo bali itumike kuinua hali zao za kimaisha .

Aidha, ameviomba vikundi hivyo kuhakikisha wanakuwa waaminifu katika suala la kurejesha fedha hizo ambapo amewasihi kutokuanza kusubiri wataalamu wa maendeleo ya jamii kuwafuatilia bali wao wenyewe wakumbushane kurejesha hizo fedha ili ziweze kutumika kuwakopesha na watu wengine.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba, Elias Kayandabila ameviomba vikundi vilivyopokea mikopo hiyo kuhakikisha wanakwenda kuzitumia fedha zile kufanya yale ambayo wamekubaliana na ambayo wameelekezwa kwenye mafunzo yaliyotolewa na watu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba, Magongo Justus amevisihi vikundi vya akina Mama, Vijana na Watu wenye Ulemavu kuhakikisha wanazitumia vizuri fedha hizo ili waweze kupata faida ili ile faida ambayo wangerejesha kama riba basi ndio iwasaidie kununua mboga na hata kuwasaidia kufanya shughuli nyingine ambazo wanafikiri wangezifanya lakini kwanza wazalishe kwa mujibu wa malengo ya mikopo waliyopewa.

Mbunge wa jimbo la Muleba Kusini, Dk. Oscar Kikoyo amevisisitiza vikundi hivyo kuwa hiyo fedha iliyotolewa kwao ni fedha ya mzunguko, wamekopeshwa wakizalisha robo ya tatu vitakopeshwa vikundi vingine hivyo amewaomba wazitumie fedha hizo kuzungusha katika biashara zao na kuhakikisha wanarejesha ili robo ya tatu Januari-Machi, 2021/22 waweze kukopeshwa vikundi vingine.

Jovitha Juston ambae ni miongoni mwa wanakikundi waliopokea mkopo, pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji wanawake kiuchumi wilaya ya Muleba amemshukuru sana Mhe. Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwezesha jamii kwa mikopo hii isiyokuwa na riba inayowawezesha makundi haya kuinuka kiuchumi na hata kumudu maisha yao ya kila siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles