21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Halmashauri ya Mbogwe ilivyofanikiwa huduma ya afya ya uzazi

Na Yohana Paul, Geita

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita ni miongoni mwa halmashauri changa kwani  bado haijafikisha miaka kumi tangu kuanzishwa kwake huku robo tatu ya wananchi wake wakiwa ni wakazi wa vijijini.

Pamoja na uchanga wake, serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeweza kufikisha huduma bora za afya na kufikiwa kwa hatua kubwa ya maendeleo kitengo cha afya ya uzazi, mama na mtoto.

Akizungumuza katika mahojiano maalumu na Mtanzania Digital, Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi, mama na mtoto katika halmashauri hiyo, Hidaya Ntandu anasema hadi sasa wilaya ina jumla ya zahanati 19 na vituo vya afya viwili.

“Mbogwe kuna Zahanati 19 lakini zahanati zinazotoa huduma ya afya ya uzazi na watoto ni zahanati 16 na tuna vituo vya afya viwili ambavyo vinatoa huduma pia ya upasuaji na huduma ya kina mama kujifungua na anaposhindwa kujifungua kawaida basi anafanyiwa upasuaji,” anasema.

Hidaya anasema uwepo wa zahanati nyingi kwenye halmashauri hiyo kwa kiwango kikubwa umeongeza mwamko wa kina mama wajawazito na wale wenye watoto wachanga kuweza kuhudhuria kliniki mara kwa mara kwa kuwa huduma muhimu zimeweza kusogezwa kwenye maeneo yao.

Anasema mahudhurio ya kliniki yamesaidia sana kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga kwa kuwa wameweza kupatiwa elimu ya afya ya uzazi na hadi sasa mwelekeo ni mzuri na unatoa matumaini mazuri.

“Kwa kipindi cha 2018/19 bado tulikuwa na asilima ndogo sana, lakini hadi 2020 tumeona mwelekeo umeanza kupanda, tunapopata kina mama wajawazito wanaokuja kliniki mapema ina maana afya ya uzazi lazima iboreke, na tunapoangalia afya ya uzazi, tunamuangalia mama pia.

“Mwamko huu umesaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto kwani tunapoona akina mama wanakuja kliniki mapema na idadi kubwa ya wanawake wanakuja kujifungulia hospitali maana yake wanakuwa kwenye mikono salama,” anasema Hidaya.

Anakiri kwamba vifo vingi vya wajawazito vinatokea kwenye jamii pale mama anapochelewa kufika hospitali kupata huduma kwa wakati, lakini mjamzito anapopatiwa elimu na wataalamu wa afya anakuwa katika hali ya usalama zaidi na anapata huduma anayostahili yeye na mtoto.

Akizungumuzia juu ya hali ya huduma ya uzazi wa mpango wilayani humo, Hidaya anasema elimu na huduma hiyo inatolewa kwenye zahanati zote na hadi sasa mwamko umeanza kuonekana kwa kina mama wengi kujitokeza kupatiwa huduma ya uzazi wa mpango. 

“Kipindi cha nyuma mwamko wa elimu ya uzazi wa mpango ulikuwa mdogo sana, tulikuwa tunapata mpaka asilimia tano hadi kumi za kina mama waliokuwa wanakuja kujiunga na huduma ya uzazi wa mpango.

“Kwa sasa huduma inaenda inapanda japo kuwa ni taratibu ila huduma inakwenda vizuri sana sana katika hizi njia za muda mrefu kwa sababu akina mama wengi wameonekana kupenda sana huduma ya njia ya njiti na sindano,” anaeleza.

Anasema kuwa mbali na mwamko uliopo lakini imeonekana bado kuna mfumo dume ambapo wanaume wamekuwa hawaruhusu wanawake zao kwenda kupata huduma ya uzazi wa mpango kwa sababu ya dhana potofu mbalimbali.

Kina Mama mbalimbali wakiwa na watoto wachanga wakisubiri huduma katika kliniki ya mama na mtoto iliyopo kata ya Masumbwe, halmashauri ya wilayani Mbogwe mkoani Geita. PICHA Na Yohana Paul, Geita.

Anasema amepokea taarifa watu wengi wanaamini kwamba mama akipata huduma ya uzazi wa mpango anakuwa Malaya na wengine wanasema njia za uzazi wa mpango zinaleta magonjwa kama kansa ama zinaleta ulemavu kwa watoto watakaozaliwa.

“Pamoja na hayo, ila baada ya kuwa wanaendelea kupatiwa elimu za masuala ya afya ya uzazi pamoja na uzazi wa mpango tunaona mwamko wa kutumia uzazi wa mpango unaongezeka na japo ni kidogo kidogo lakini mwamko unaonekana siku hadi siku.

“Zamani tulikuwa tunakwenda hadi vijijini, tulikuwa hatupati kina mama wanajitokeza kujiunga na uzazi wa mpango lakini sasa hivi wanakuja wenyewe mpaka vituoni wanahitaji huduma na hadi kufikia mwaka jana mwitikio wa uzazi wa mpango ulifikia asilimia 28,” anasema.

Hidaya anaeleza kuwa kipindi cha nyuma masuala ya uzazi wa mpango yalikuwa kati ya asilima 15 hadi 17 kati ya kina mama wote wanaopata huduma ya kliniki na wale walio kwenye umri wa kuweza kuzaa.

Mapokeo ya Kina Mama

Prisca Fanuel ni mama kutoka kitongoji cha shinyanga A, kata ya Masumbwe anakiri wazi kwamba huduma za afya kwenye kata hiyo zimeboreshwa sana kwa miaka ya hivi karibuni tofauti na hapo awali kwa kuwa sasa ana uhakika wa kupata huduma za kliniki na uzazi wa mpango. 

Anasema kwa kutumia zahanati zilizopo ameweza kupata elimu na huduma ya uzazi wa mpango ambayo imemuletea ubora katika familia yake kwa sababu amepanga uzazi pasipo shida yeyote ile na  ameweza kutenganisha umri sahihi wa watoto kwa usahihi.

Anasema matumizi ya uzazi wa mpango yamemuwezesha kumudu gharama za malezi na wameweza kusoma vizuri na hadi sasa uzazi wa mpango hauna shida kwake kwa kuwa anachokiona umemuongezea maboresho ndani ya familia hivo anawashauri kina mama wengine kutumia njia za uzazi wa mpango.

“Wengine wanasema kwamba ina madhara, hapana, mimi nimetumia miaka mitano sasa na haina madhara yeyote yale, na bado sasa hivi nimejifungua mtoto yupo salama kabisa,” anaongeza.

Naye Restuta Cosmas mkazi wa kata ya Masumbwe wilayani Mbogwe ni mzazi wa watoto wawili na hadi sasa hana mpango wa kutumia njia ya uzazi wa mpango kwa sababu anahitaji kupata watoto  lakini kwa baadaye akitafakari anaweza kutumia.

“Sasa hivi sitaki kutumia uzazi wa mpango kwa sababu wanasema yana madhara, unaweza ukaharibu uzazi au ukazaa mtoto kilema, ila nikifikisha hata watoto wanne ninaweza nikaanza kutumia mpango wa uzazi,” anasema Restuta.

Mapokeo ya Kina baba 

Steven Magembe mkazi wa masumbwe anasema maboresho ya huduma za afya yaliyofanyika yamemufanya aone siyo tatizo kuhudhuria kliniki yeye na mke wake kwa ajili ya kupata maelekezo ya afya.

Anasema anaridhishwa na huduma ya afya inayotolewa na watoa huduma kwa kuwa wanatoa maelekezo na kuwasaidia watu pale wanapohitaji msaada hasa kwa kina mama wajawazito.

Mbali na maboresho hayo lakini anasema yeye na mke wake hawatumii njia yeyote ya uzazi wa mpango kwa kuwa haoni sababu ya kufanya hivo na imani yake ya kidini inamufanya aamini kutumia uzazi wa mpango ni kosa na siyo sawa.

Anasema hadi sasa ana watoto watatu na lengo lake ni kuendelea kuzaa kwa kiwango ambacho anaona anao uwezo wa kuwalea huku akisisitiza iwapo atafanikiwa kupata watoto angalau 10 ndio anaweza kuacha kuzaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles