31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Halmashauri Ngara yatumia milioni 460 kuboresha mafunzo FDC

Na Allan Vicent, Ngara

Maboresho makubwa yaliyofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) yameongeza udahili wa wanafunzi (Vijana) kutoka 40 hadi 200 kwa Mwaka.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Aidan Bahama, alipokuwa akiongea na www.mtanzania.co.tz aliyemtembelea ofisini kwake.

Amesema kuwa matengenezo hayo ambayo yamegharimu kiasi cha Sh milioni 460 yamewezesha kuboreshwa kwa miundombinu ya chuo ikiwemo kufungwa kwa vifaa vya kisasa vya kujifunzia kozi mbalimbali.

Alibainisha kuwa chuo hicho kilipoteza mvuto kwa kiasi kikubwa kutokana na uchakavu wa miundombinu na mazingira yake hali iliyopelekea kukosa wanafunzi.

“Tumeboresha Chuo chetu kwa kiasi kikubwa, sasa kinavutia, naomba wazazi na walezi kutoka wilaya na mikoa mbalimbali kuleta watoto wao kwa wingi ili kunufaika na mafunzo yatolewayo,” amesema.

Alifafanua kuwa chuo hicho kimeongeza idadi ya mafunzo na kufunga vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia jambo ambalo limechochea ongezeko la wanafunzi kutoka 40 hadi 200 kwa mwaka.

Bahama amesisitiza kuwa fani zilizoanzishwa zimelenga kuingiza vijana katika soko la uchumi wa viwanda kwa kujiajiri au kuajiriwa katika fani za komputa, uselemala, uashi, magari, udereva na ushonaji.

Aidha, aliongeza kuwa wamefunga kompyuta mpya 60 kwa ajili ya kutolea mafunzo, vyerehani 70 vya kutumia umeme na mikasi ya kisasa ya kukatia vitambaa na kununua vifaa vya umeme vya ufundi selemala.

“Vyuo vingi vya maendeleo ya jamii vilisahaulika sana hali iliyopelekea kukosa ushindani na vyuo vingine hivyo kutotimiza azma ya serikali ya kuandaa vijana kuingia katika soko la uchumi wa viwanda,” alisema.

Bahama amebainisha kuwa jambo lolote lenye ushindani ni lazima lifanyiwe maboresho ili mazingira yake yaendane na hali ya soko vinginevyo halmashauri zitaendelea kulaumu kuwa vyuo vya FDC havina soko.

Ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kuchangamkia fursa za mafunzo yanayotolewa katika chuo hicho ili kuendana na kasi ya maendeleo ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles