24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Hall akiri Azam kuzidiwa uwezo

Stewart HallNA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Klabu ya Azam FC, Stewart Hall, amekiri timu yake kuzidiwa uwezo na wapinzani wao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Esperance ya Tunisia iliyowatoa kwenye michuano hiyo.

Mchezo huo wa marudiano wa raundi ya pili ya michuano hiyo ulifanyika juzi  Uwanja wa Olimpique de Rades na wenyeji Esperance kushinda kwa mabao 3-0, hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 4-2, kutokana na Azam FC kushinda 2-1 jijini Dar es Salaam siku 10 zilizopita.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Hall alisema Esperance walicheza vizuri hususani kipindi cha pili na kuweza kuyatumia makosa waliyoyafanya wachezaji wake kupata ushindi huo, uliowavusha hatua inayofuata ya michuano hiyo.

“Esperance ilicheza vizuri sana hasa kipindi cha pili, walicheza kwa haraka na soka la kushambulia hivyo kusababisha madhara kwa upande wetu na tukajikuta tukifanya makosa ambayo yalikuwa ni faida kwao, timu yangu ilipambana lakini tulizidiwa,” alisema.

Alisema kukosekana kwa wachezaji wake Kipre Tchetche, Pascal Wawa na Shomari Kapombe ambao ni majeruhi pamoja na Jean Mugiraneza ambaye anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano, pia kumechangia kikosi chake kupwaya hivyo kushindwa kuwadhibiti Waarabu hao.

“Kushindwa kudhibiti mpira ni udhaifu mwingine ambao ulionekana kwenye kikosi changu, hivyo kuzidi kuwapa nafasi wapinzani wetu kutushambulia lakini pia baadhi ya wachezaji walionekana kuchoka mapema,” alisema.

Alisema atahakikisha anayafanyia kazi mapungufu hayo ili yasiweze kujirudia kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na kuhatarisha harakati zao za kuchukua ubingwa.

Kikosi cha Azam kitarejea nchini kesho na kupitiliza moja kwa moja mkoani Mwanza kwa usafiri wa ndege, kujiandaa na mchezo wao wa FA dhidi ya Mwadui FC utakaocheza keshokutwa Uwanja wa CCM Kirumba mkoani humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles