25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hakimu sasa atoa siku 14 upelelezi ukamilike kesi ya akina Dk. Ringo

NA PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa siku 14 kwa upande wa mashtaka kuhakikisha wanakamilisha upelelezi katika kesi inayowakabili vigogo wa Six Telecoms akiwemo wakili Dk. Ringo Tenga na wenzake.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Mhandisi Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alitoa siku hizo mahakamani hapo jana, baada ya Wakili wa Serikali, Batilda Mushi, kuieleza mahakama hiyo kuwa jalada la kesi ya vigogo hao bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Wakili Mushi alieleza kuwa jalada hilo linafanyiwa kazi na kwamba wapo kwenye hatua za mwisho ya kukamilisha upelelezi.

Alieleza kwa kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado unaendelea, aliiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya kusema hayo, Hakimu Simba, alitoa siku 14 kwa upande wa mashtaka kuhakikisha wanakamilisha ili kesi hiyo iweze kwenda mbele siku itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Kutokana na maelezo hayo kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 5, 2019 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Dk. Tenga ambaye ni Mkurugenzi na Mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake wanadai kuwa kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14, 2016 maeneo ya Dar es Salaam, walitoza maalipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao pia wanadaiwa katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shtaka la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni, Tenga na Chacha, wanadaiwa kuwa walitumia ama walisimamia Dola za Marekani 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashtaka yaliyotangulia.

Wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22 (sawa na Sh bilioni 8).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles