26.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 4, 2024

Contact us: [email protected]

Hakimu atishia kufuta kesi ya vigogo NIDA

mahigacourt

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

HAKIMU Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage ameiambia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),  kwamba hataki ubabaishaji na kama hawataki kuendelea na kesi ya vigogo wa Mamlaka ya Vitambulisho vyaTaifa (NIDA) awaachie huru washtakiwa.

Hakimu Mwijage alisema hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa mbele yake bila kuwepo wakili kutoka taasisi hiyo.

“Dickson Maimu na wenzako wote mpo, mwendesha mashtaka yuko wapi….,”alihoji Hakimu Mwijage.

Hakukuwa na jibu mahali alipo mwendesha mashtaka wa kesi hiyo, Hakimu alimuuliza wakili mwingine wa Takukuru Devotha Mihayo kama yuko kwa ajili ya kesi hiyo.

Devotha alijibu kwamba alikuwepo mahakamani hapo kwa ajili ya kesi nyingine iliyopo katika hatua ya utetezi, lakini akakubali kumwakilisha aliyetakiwa kuingia mahakamani kwa kesi ya vigogo hao.

“Msiwe na kiherehere cha kuwaleta watu mahakamani kama hamjajipanga, kama hakuna kesi niifute.

“Mawakili wa Takukuru hawapo mahakamani, ifike mahali kila mmoja atimize wajibu, ubabaishaji fanyeni mahakama zingine kwangu sitaki.

“Kama hamna haja ya kuendelea na kesi waachiwe huru, mlikuwa mnawakimbiza kimbiza hapa kwa hati za nyumba leo aibu, mahakamani hampo.

“Mlikuwa mnaonyesha kesi ina maslahi ya umma, mnaleta mativii , hayo masilahi ya umma kwa kipi, mnaleta picha gani kwa jamii,” alisema Hakimu Mwijage na kuongeza.

“Hivi mnapata safari za nje kweli au mnajifungia ndani, ndio maana hamuwezi kujifunza, kuna usemi wa hapa kazi tu, hapa kazi tu bila malengo haiwezekani, mimi nasema hapa kazi tu na malengo, malengo yangu kumaliza kesi haraka,”alisema.

Devotha alidai upelelezi wa kesi unaendelea akaomba tarehe nyingine ya kesi kutajwa.

Alidai jalada la kesi hiyo linahusiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hivyo watawasiliana kwa ajili ya kukamilisha upelelezi haraka.

Hakimu Mwijage alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 29,  mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na aliruhusu mshtakiwa wa saba, Sabina Raymond kusafiri kwa shughuli za kifamilia Morogoro na Mwanza lakini ahakikishe siku ya kesi anakuwepo mahakamani.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake saba, wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 1.16.

Mbali na Maimu, washtakiwa wengine ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA, Benjamin Mwakatumbula, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege,  Xavery Kayombo, Meneja Biashara wa mamlaka hiyo, Avelin Momburi na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Joseph Makani.

Washtakiwa pamoja na mashtaka mengine yakiwemo kuisababishia Serikali hasara wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 15 hadi 19,  mwaka 2010 katika Makao Makuu ya NIDA wilayani Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi walizokuwa nazo walitumia madaraka  vibaya kwa kuidhinisha malipo bila kufuata viwango vya kubadilishia fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles