Asifiwe George na Evans Magege
HATIMAYE Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ameshitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa mawili ya kutoa lugha ya matusi na uzembe wa kuhifadhi silaha yake.
Askofu Gwajima ameshitakiwa pamoja na wenzake watatu, waliotajwa mahakamani hapo kuwa ni Yekonia Behanaze, Jofrey Andrew na George Mzava.
Mbele ya Hakimu Mkazi Wilfred Dyansobera, wakili upande wa Serikali, Joseph Maugo, alidai kuwa Askofu Gwajima anakabiliwa na shtaka la kumtukana Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo.
Wakili Maugo alidai kuwa Askofu Gwajima alitenda kosa hilo kati ya Machi 16 hadi 25, katika Viwanja ya Tanganyika Peckers, vilivyoko Kawe, Jijini Dar es Salaam, mahali ambako kanisa lake lipo.
Katika shitaka la pili, Wakili Maugo alidai kuwa Askofu Gwajima anashtakiwa kwa uzembe wa kuhifadhi silaha ya moto anayomiliki kisheria.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili Maugo alidai Askofu Gwajima alitumia lugha ya matusi na kumfedhehesha Askofu Pengo kwa kumuita mpuuzi na asiyekuwa na akili.
Hata hivyo, Askofu Gwajima alikana mashtaka yote mawili.
Wakili Maugo alidai mbele ya Hakimu Dyansobera kuwa washitakiwa wengine watatu katika kesi hiyo walitenda kosa la kukutwa na silaha kinyume cha sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Machi 29, katika Hospitali ya TMJ Mikocheni, iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam.
Aliendelea kudai kuwa washitakiwa Behanaze, Andrew na Mzava walikutwa na risasi tatu za bastola, 17 za shotgun na bastola moja.
Baada ya kusoma mashitaka hayo, Wakili Peter Kibatala ambaye anamtetea Askofu Gwajima, aliiambia mahakama kuwa shitaka linalomkabili mteja wake linadhamika kisheria, hivyo aliiomba mahakama iridhie kumpatia dhamana.
Wakili huyo alieleza kuwa mshtakiwa ni Askofu wa Kanisa la Glory’s of Christ Tanzania (Kanisa la Ufufuo na Uzima) na anafahamika nchi nzima, lakini mbali na tuhuma hizo, nyumba yake jana ilizingirwa na polisi.
Aliendelea kueleza kuwa mteja wake amekuwa nje kwa dhamana tangu Machi 27 na awali hata alipokuwa akihojiwa na polisi na kuzimia ghafla amekuwa mwaminifu kwa kuripoti mwenyewe polisi kila alipohitajika, hivyo pamoja na kuzingatia wasifu wake, aliiomba mahakama ikubali ajidhamini mwenyewe.
Akijibu hoja hizo, Mwanasheria wa Serikali, Shedrack Kimario, alisema hoja zilizotolewa na wakili wa mshtakiwa hazina mashiko, kwa sababu mshitakiwa alionekana kutaka kukwepa mkono wa sheria.
Hata hivyo, alisema iwapo mahakama itaona anastahili kupata dhamana na iwapo atatimiza masharti, basi upande wa mashitaka hauna pingamizi.
Hakimu Dyansobera baada ya kuzingatia hoja za pande zote mbili alisema Askofu Gwajima ajidhamini mwenyewe kwa bondi ya Sh milioni moja na washitakiwa wenzake aliwataka kuwa na mdhamini mmoja akila mmoja ambaye atasaini bondi ya Sh milioni moja.
Washtakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana na kuachiwa hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Mei 4, mwaka huu.
Awali Askofu Gwajima aliwasili katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam saa 9:10 akiwa ndani ya gari lake lenye namba za usajili T. 159 DDH, akiwa ameongozana na mawakili wake.
Alikwenda kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kabla ya kupelekwa Mahakama ya Kisutu kwa kutumia gari lenye namba za usajili Z 322 FN, lililoingia kwenye viunga vya mahakama ya Kisutu majira ya 9:27 alasiri.
Polisi wazingira nyumba ya Gwajima
Askari Polisi jana waliizingira nyumba ya Askofu Gwajima kwa muda wa saa 8, kuanzia saa 12 asubuhi.
MTANZANIA Jumamosi liliwasili nyumbani kwa Askofu Gwajima, iliyo Barabara ya Nyaruke, Mtaa wa Kilimahewa, huko Salasala na kukuta magari sita yakiwa na askari waliokuwa wamebeba silaha za moto.
Hadi majira ya saa 3.30 asubuhi, Mtaa wa Kilimahewa ulikuwa kimya, huku askari wenye silaha wakirandaranda na baadaye waumini wa kanisa hilo walianza kukusanyika nje ya nyumba hiyo.
Waumini hao walianza kuwashutumu askari polisi kuwa wameshindwa kukamata magaidi na badala yake wanamng’ang’ania baba yao wa kiroho.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilimahewa, Richard Njera, aliliambia gazeti hili kuwa Polisi walifika mtaani kwake saa 12 asubuhi na wakamueleza wako pale kwa ajili ya kumkamata Askofu Gwajima.
“Wameniambia wamekuja kumkamata Gwajima na wana mazungumzo naye, lakini imekuwa ngumu kumchukua kwa sababu lango halijafunguliwa mpaka sasa,” alisema Njera.
Ilipofika sasa nne asubuhi umati wa waumini ulizidi kuongezeka na waligawanyika katika makundi mbalimbali, huku wakizidi kusogea zaidi eneo la nyumba hiyo.
Ilipotimu saa 6:03 walifika baadhi ya viongozi wa Kanisa la Ufufuo na kufanya kikao na askari ambacho kilidumu kwa takribani dakika tano, baadaye alifika Mwanasheria wa Askofu Gwajima, Peter Kibatala, ambaye aliungana na viongozi hao.
Muda mfupi baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo, askari polisi walianza kuondoka na kuwaacha waumini wakishangilia.
Hadi inatimu saa 6:35, askari wote walikuwa wameshatoweka.