VERONICA ROMWALD Na PATRICIA KIMELEMETA – DAR ES SALAAM
ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ameonesha nakala ya cheti cha matokeo ya mtihani wa kumaliza kidato cha nne (CSEE) alichodai kuwa ni cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Katika siku za karibuni, Askofu Gwajima kwa nyakati tofauti akiwa kanisani kwake alidai kuwa mkuu huyo wa mkoa anatumia vyeti vya mtu mwingine aitwaye Paul Christian Malanja wakati jina lake halisi ni Daudi Albert Bashite.
Akizungumza kanisani kwake Ubungo Dar es Salaam jana, kwenye ibada aliyoipa somo lisemalo ‘Nitavunja vunja magari ya chuma’ Gwajima alidai cheti hicho ni nakala halali ambayo ilitolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kwa Shule ya Sekondari ya Pamba Mwanza ambako Makonda alisoma.
“Wiki iliyopita nilisema nimefunga mjadala wa Makonda kwa sababu lengo langu lilikuwa Rais John Magufuli asikie na afanye maamuzi, lakini nilisema akinichokoza nitampiga na moshi utatoka hataweza kufumbua hata macho. Leo nimeamua kuweka wazi cheti chake cha kwanza na wiki hii nitaendelea kumpiga.
“Sasa nakala hii inasomeka cheti hiki kimetolewa baada ya kufanyika mtihani wa mwaka 2000, namba ya shule ya pamba ni S0546, namba ya mtihani ya Daudi A Bashite ni S0546/0016, jinsia mwanamume na kinaonesha amepata F katika masomo yote. Yaani mtu huyu amepata zero hadi somo la bible knowledge (somo la biblia),” alisema Askofu Gwajima huku akishangiliwa na waumini wake waliokuwa wamefurika kanisani hapo.
Aliongeza “Hiki ndicho cheti chake halali, watu wanasema Gwajima huogopi kufa, mimi siogopi kufa…. ‘let me say something’, unaweza kuua mwili wangu lakini huwezi kuiua roho yangu, nitaendelea kuwepo.
“Fikra ya kifo ipo hivi, kwanza kila mtu atakufa, mbili ni tofauti ya umri kati ya mtu mmoja na mwingine pindi wanapokufa, tatu ni ile ‘impact’ anayoiacha mtu pindi anapokufa, na nne ni ule ujasiri aliouacha huyo aliyekufa,” alisema.
Alisema anashangazwa na ukimya wa Rais Magufuli dhidi ya Makonda, kwani ni zaidi ya wiki tatu sasa Makonda amekuwa akilalamikiwa kuhusu kutumia vyeti vya mtu mwingine hata hivyo hajamchukulia hatua yoyote kama alivyofanya kwa wengine.
“Juzi tu, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe aliteleza kuhusiana na tangazo lake la kupiga marufuku watu kuoana bila kuwa na cheti cha kuzaliwa lakini ndani ya saa 24 Rais Magufuli alijitokeza hadharani na kumsahihisha,” alisema.
KUZAA NA MUUMINI WAKE
Akizungumzia sakata la mtoto anayedaiwa kuzaa na muumini wake na kisha kumtelekeza, Askofu Gwajima alisema huo ni mkakati wa kuzima moto wa vyeti alioibua hivi karibuni.
“Yule kweli ni muumini wangu ana ugonjwa wa akili, mumewe aliyezaa naye ambaye anaitwa Said Amir Kapinga, na baba mkwe wake wote wanasali hapa na kesho (leo) wataeleza ukweli wote,” alisema.
“Walimchukua jumatano usiku, wakiwa hawajui kama ana tatizo la akili,wakampeleka hadi Sinza Mori ambako walirekodi kipindi hicho ambacho kilitakiwa kurushwa katika kituo ambacho watangazaji hao wanafanya kazi.
“Kipindi hicho kinahusu mambo ya umbea, si mnakijua (alikitaja), walipatana kukirusha Ijumaa saa 3:00 hadi 3: 30 usiku lakini vijana wale hawakukirusha kama walivyokubaliana kwa sababu walikuwa hawaja-balance kama ambavyo Sheria ya Huduma za Habari inavyotaka,” alisema.