24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Gwajima afunguka sakata la Mbasha

NA GABRIEL MUSHI

gwajima na mbasha
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam, Josephat Gwajima (kushoto) na Emmanuel Mbasha (kulia), mume wa mwimbaji wa nyimbo za Injili nchini, Flora Mbasha.

MCHUNGAJI Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam, Josephat Gwajima, amefunguka na kuuweka hadharani uhusiano wake na familia ya waimbaji wa nyimbo za Injili nchini, Flora Mbasha na mume wake, Emmanuel Mbasha.

Gwajima amekuwa akitajwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Flora na kwamba hatua hiyo inadaiwa kuchangia mvurugano kwenye ndoa ya wanamuziki hao.

Mbali ya kutajwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Flora, pia anatajwa kuwa nyuma ya kesi ya ubakaji inayomkabili Mbasha ambapo kumekuwa na taarifa mbalimbali zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikimuhusisha mchungaji huyo na kesi hiyo iliyoanza kutajwa Juni 17 mwaka huu.

Akizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu sakata hilo kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili, Gwajima akiwa katikati ya madhabahu ya kanisa lake lililopo Kawe jijini Dar es Salaam huku akiwa na wasaidizi wake pamoja na watoto wake wawili, alisema taarifa zinazoenezwa ni za kijinga na hazina ukweli wowote.

Alisema mgogoro wa Mbasha na Flora unaonekana kuwa ni wa muda mrefu na kwamba umekuja kujitokeza kanisani kwake baada ya kuanza kufanya nao kazi ya kutoa huduma ambapo wawili hao walikuwa waburudishaji kwenye mikutano yake.

“Nilimfahamu Flora na Mbasha mwezi wa tisa mwaka jana… kipindi hicho nilikuwa na mkutano Arusha. Wote wawili niliwaalika tukaenda nao kwenye mkutano na pindi mkutano ulipomalizika walirudi nyumbani tukaenda tena katika mikoa mingine ya Moshi, Tanga, Morogoro na Kilombero wote wawili walikuja kushiriki mikutano hii kama waimbaji na wote walirudi nyumbani kwao.

“Nimekuwa nikiona kwenye mitandao wakisema kuwa nilikwenda na Flora peke yake katika baadhi ya maeneo kama Morogoro… si kweli, muda wote walikwenda wote wawili na walirudi wote wawili, pia sina uhusiano wa kimapenzi na Flora kama inavyodaiwa.

“Kwanza watu wote waliokwenda kwenye mkutano walikuwa 300, kila mkoa walikuwa watu 300. Naamini kuna mtu ana hoja zake binafsi anataka kuudanganya umma kwamba Gwajima ana uhusiano na Flora.

“Nataka niwakumbushe Watanzania kuwa baada ya kumaliza hii mikutano hawakuwa washirika wetu kanisani, kwa maana kuwa hawakuwa wakisali kanisani kwangu kwa sababu tuliwaalika kuja kuimba na walikuwa wanalipwa kwa sababu ya kuimba pekee,” alisema.

Aidha alisema baada ya kumaliza mikutano hiyo na kukaa kwa muda, Flora aliamua kwa mapenzi yake kwenda kusali kanisani kwake na baadaye mumewe naye akajiunga na mke wake kushiriki ibada kwenye kanisa lake.

Akizungumzia suala la kuwa nyuma ya kesi inayomkabili Mbasha na kuwa amekuwa akimpatia fedha Flora ili kufanikisha dhamira ovu dhidi ya mumewe, Gwajima alisema si la kweli.

“Hili suala la kumpatia fedha Flora ili amuangamize mume wake halina ukweli, ukweli ni kwamba baada ya Mbasha kutuhumiwa kubaka alitoweka nyumbani, mke wake hakuwa na sehemu ya kupata msaada, kutokana na hali hiyo ndipo Flora alikuja kanisani kwetu kuomba msaada wa fedha na kwa vile ni mshirika wetu tulimsaidia.

“Nilizungumza na wachungaji wenzangu tukaona ni vyema tuitishe harambee ili waumini wamchangie kama wanavyochangia watu wengine wenye matatizo mbalimbali kwa sababu Flora alisema jamani hana fedha na mume wake amemkimbia na hana chochote, watu wakamchangai!

“Sasa nadhani zipo fikra kwamba, Gwajima anachangisha fedha za Flora ili apate fedha za kuendelea kumshtaki mumewe, pia zipo fikra kwamba kanisa langu ndilo limemzuia Flora kurudi kwake.

“Zikianza kusambazwa picha mbaya za Gwajima kwenye mitandao ya kijamii ili nichukue uamuzi wa kumfukuza Flora kanisani kwangu ili akapate matatizo, siwezi kumfukuza Flora kanisani kwangu wala hilo halitatokea… nimechukua hatua mbalimbali ikiwamo kumshauri Flora arudi kwa mume wake lakini alikataa mwenyewe,” alisema.

Aidha, Mchungaji huyo pamoja na kukanusha kuwa yeye sio chanzo cha mgogoro huo pia alisema hajamsomesha wala hakuwahi kutoa fedha za kufadhili masomo ya Flora nchini Uingereza.

“Unaweza kumpeleka ng’ombe kisimani lakini jukumu la kunywa maji ni lake, akikataa ni mwenyewe, akinywa ni mwenyewe, mimi siku zote nawashauri Flora na Mbasha wawe na uhusiano mzuri, warudishe uhusiano wapatane, hata kesho (leo) nitampigia simu baba yake mzazi Mbasha na wadogo zake ili nijaribu kuwaita tena kujaribu kuona kama tunaweza kuwasaida kuwarejesha kwenye ndoa yao.

“Hata hivyo uamuzi wa kurudiana bado utakuwa ni wa kwao wao mimi siwezi kuwalazimisha,” alisema.

Mbasha (32) alipandishwa kizimbani Juni 17 mwaka huu katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala akikabiliwa na mashtaka mawili ya ubakaji na kusomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Wilberforce Luago.

Akisoma mashtaka Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, alidai mshtakiwa ambaye pia ni mfanyabiashara alitenda makosa hayo mawili maeneo ya Tabata Kimanga jijini Dar es Salaam.

Kesi ya Mbasha inatarajia kusomwa tena Juni 17, mwaka huu kwenye Mahakama hiyo ambapo mshtakiwa huyo yuko nje kwa dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

4 COMMENTS

  1. jamani ukweli wa haya yote anaujua flora na mumewe.ila wamejiharibia sana hivi ni nani atae amini huduma yao tena!! kibaya zaid flora anaonesha yuko kimaslahi zaidi kilichomfanya kwena kusafisha thamani zote nyumbani ninni?ina maana harudi tena mchawi wa mtu ni mtu mwenyewe,wasituchanganye kama wamechoka kuishi pamoja waende mahakamani ili kila mtu awe huru kufanya lake. mmetukera. harafu kuna watu wengi sana wanamatatizo katika ndoa zao.publications hazisaidii sana sana zinaongeza chuki na hasira kwa wahusika.

    • Jamani,pamoja na gwajima kuhusika na Kesi Hii ya mbasha, pia ukweli ni kwamba mbasha alibaka maana kuna kipindi alirikodiwa akiwa anaomba msamaha. Wote wanamakosa.ukitaka ukweli tafuta hiyo sauti kwenye mtandao.

  2. Jamani kuna msemo unaosema hata kama hujui kusoma hata picha huoni……ina maana huyo mchungaji anayajua mengi…ivi muda gani umepita mpaka aseme frola alienda kuomba msaada kanisani..si alikimbia nyumba kabla?.ivi mwenye shida ya namna iyo anaendesh PRADO…kuna wamama wangapi mpka kuna mama mmoja alikuwa anashinds kanisani hapo kwa jili yya kusaidiwa maradhi akashindwa akaenda mpaka clloud fm…yule mama ADRIANO WA brock 41 BIAFRA…..TAFADHALINI TUSIDANGANYWE MANA HATUDANGANYIKI!

  3. Mti wenye matunda ndio hupigwa mawe. Nashauri Watanzania wezangu tusiwe wepesi wa kudaka mambo, kuyaamini na kutoa hukumu. Kuna kitu kinanishangaza hapa. Hicho chanzo cha habari kilichotoa habari mwanzo kwamba pastor kauza robo tatu ya mali zake kimetoa wap hizo habari? Maana inaonekana hazina ukweli ndani yake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles