33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

GUARDIOLA, CONTE VITANI ENGLAND LEO

LONDON, ENGLAND

KIVUMBI cha Ligi Kuu nchini England kinatarajia kuendelea leo timu mbalimbali zikishuka dimbani, lakini miongoni mwa timu hizo vita kubwa ni kati ya Chelsea na Manchester City.

Viwanja saba vitakuwa vikitimua vumbi mapema sana, lakini hisia za wadau na mashabiki mbalimbali zitakuwa pale kikosi cha Manchester City kitakaposhuka kwenye uwanja wa Stamford Bridge na kukutana na mabingwa watetezi, Chelsea saa 1:30 usiku.

Klabu ya Man City imetajwa kuwa imefanya usajili wa kutisha katika kipindi hiki cha majira ya joto kuliko klabu yoyote, hivyo inawapa wakati mgumu wapinzani hasa kutokana na matokeo waliyoyapata katika michezo ya hivi karibuni.

Mbali ya Manchester City kuwa na kikosi bora, lakini kocha wa timu hiyo, Pep Guardiola, ni miongoni mwa makocha bora duniani, mipango yake mara kwa mara inakuwa na matokeo mazuri.

Lakini kwenye mchezo wa leo, Manchester City itashuka dimbani huku ikikosa huduma za nyota wake, Sergio Aguero ambaye juzi alipata ajali ya gari na kusababisha mbavu mbili kuvunjika, hivyo atakuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili, hata hivyo beki wa kushoto, Benjamin Mendy, ataukosa mchezo huo kutokana na majeruhi yanayomsumbua.

Mbali na wachezaji hao wawili, Guardiola amedai kuwa hana wasiwasi na wachezaji waliobakia kikosini wana uwezo wa kubadilisha matokeo muda wowote kutokana na ushirikiano na umoja wao. Man City wanaongoza kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 16 baada ya kucheza michezo 6 wakiwa sawa na wapinzani wao, Man United na kufuatiwa na Chelsea wenye pointi 13.

Kwa upande wa Chelsea, bado wanaonekana kuwa imara hasa katika safu ya kiungo na ushambuliaji, kocha wa timu hiyo, Antonio Conte, ameweka wazi kuwa lengo lake ni kuhakikisha anaendeleza ubabe wake kwa Man City kama ilivyo katika msimu uliopita.

Msimu uliopita mchezo wa awali Chelsea walikuwa ugenini na walifanikiwa kushinda mabao 3-1 huku Manchester City wakimaliza pungufu baada ya wachezaji wao wawili kuoneshwa kadi nyekundu, huku mchezo wa marudiano Chelsea wakiwa nyumbani walishinda mabao 2-1, hivyo Conte anataka kuendelea na ubabe huo.

Haitakuwa kazi rahisi kwa pande zote mbili kutokana na uwezo wa makocha pamoja na wachezaji waliopo kwenye vikosi hivyo, lakini Man City wanaonekana kupewa nafasi kubwa kutokana na ubora.

Timu hizo jumla zimekutana mara 142 kwenye michuano mbalimbali, lakini Chelsea wanaongoza kwa kushinda mara 57, huku Man City wakishinda mara 47 na kutoka sare mara 38.

Michezo mingine ambayo itapigwa leo ni pamoja na Huddersfield dhidi ya Tottenham, Bournemouth dhidi ya Leicester City, Man United wakiwa nyumbani dhidi ya Crystal Palace, Stoke City wakipambana na Southamton, West Brom wakicheza dhidi ya Watford na West Ham dhidi ya Swansea City.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles