26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Griezmann ampa Ronaldo Ballon d’Or

Antoine Griezmann
Antoine Griezmann

PARIS, UFARANSA

BAADA ya michuano ya Euro 2016 kumalizika huku Ureno ikitwaa ubingwa huo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Ufaransa, mshambuliaji wao, Antoine Griezmann, ameweka wazi kuwa tuzo ya Ballon d’Or itachukuliwa na Cristiano Ronaldo.

Ronaldo alipambana katika michuano hiyo hadi timu yake kufika fainali japokuwa ilianza kwa kusuasua na kuingia hatua ya 16 kwa ‘best loser’ lakini umoja wao umewafanya wabebe taji hilo.

Katika mchezo huo, mshambuliaji wa Ufaransa na klabu ya Atletico Madrid, Griezmann, alikuwa anapambanishwa na mshambuliaji wa Ureno na klabu ya Real Madrid, Ronaldo, kuwa ni nani ataweza kuibeba timu yake.

Hata hivyo, Ronaldo hakuweza kumaliza mchezo huo baada ya kuumia katika dakika za mwanzo kipindi cha kwanza, ila Griezmann alishindwa kuonesha uwezo wa kutosha kuweza kuibeba timu yake.

Kutokana na hali hiyo, Griezmann anaamini wazi Ronaldo anastahili kutwaa taji la Ballon d’Or msimu huu kutokana na mchango wake kwa timu ya taifa na klabu yake ya Madrid.

“Nilikuwa na ndoto za kutwaa tuzo ya Ballon d’Or msimu huu kwa kuisaidia timu yangu hasa timu ya taifa kwenye michuano ya Euro, lakini ndoto hizo hazijakamilika kwa kuwa nimeshindwa kuisaidia timu kutwaa ubingwa huo.

“Ninaamini wazi hii ni nafasi pekee kwa Ronaldo kutwaa taji hilo bila kipingamizi chochote, ameweza kuchukua mataji mawili makubwa msimu huu akiwa na klabu na timu yake ya taifa,” alisema Griezmann.

Ronaldo msimu huu ameisaidia klabu yake ya Real Madrid kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na kutwaa taji la Euro 2016 akiwa na timu yake ya taifa, hivyo ana kila sababu ya kutwaa Ballon d’Or msimu huu.

Mpinzani wa Ronaldo, Lionel Messi, naye alipewa nafasi kubwa ya kutwaa Ballon d’Or msimu huu lakini ameshindwa kuisaidia timu yake ya taifa kutwaa ubingwa kwenye michuano ya Copa America nchini Marekani, huku timu yake ilipokutana na Chile kwa mara ya pili mfululizo.

Messi aliisaidia klabu yake katika michuano ya Ligi Kuu nchini Hispania na kufanikiwa kutwaa ubingwa huo, pamoja na ubingwa wa Copa de Rey.

Hata hivyo, Messi anaongoza kwa kuchukua Ballon d’Or, ambapo amechukuwa mara tano, mwaka  2010, 2011, 2012 na 2015, wakati Ronaldo akichukua mara tatu mwaka 2009, 2013 na 2014.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles