24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

GHARAMA ZA MAISHA ZATESA FAMILIA

Na THOBIAS NSUNGWE,

WAKATI wananchi wengi wakilalamikia ugumu wa maisha, uchunguzi umebaini kwamba Sh 10,000 haitoshi kukidhi bajeti ya chakula kwa familia ya kawaida kabisa ya baba, mama na watoto wanne.

Uchunguzi unaonyesha kuwa, hata familia ya aina hiyo ijibane vipi, inahitaji angalau Sh 12,700 kukamilisha milo ya siku moja.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, gharama hiyo inakidhi chakula cha kawaida ambacho hakipaswi kuitwa mlo kamili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya ‘balanced diet’.

Ugumu huo wa ‘kuikimbiza’ 10,000/- unatokana na bidhaa kupanda bei na shilingi ya Tanzania kutokuwa imara.

Ukokotozi uliofanywa na gazeti hili baada ya kufanya mahojiano na familia mbalimbali zenye kipato cha chini kabisa hadi cha kati, ili familia ya baba, mama na watoto wanne waweze kumudu milo hiyo, wanahitaji yafuatayo;

Asubuhi: Kifungua kinywa, mkate mmoja wa Sh 1,200, sukari robo kilo kwa Sh 650, majani ya chai ( pakiti moja) Sh 100, mkaa Sh 2,000. Bajeti ya asubuhi inaishia hapo kwa kuzingatia kuwa huo mkate utagawanywa kwa wanafamilia wote sita, huku watoto wakitegemewa kupata vipande vidogo na hivyo kufanya jumla ya matumizi kwa mlo huo kuwa Sh 3,950.

Mchana: Huku tukifikiria kwamba familia hiyo itatumia mkaa uliobaki asubuhi kupikia chakula cha mchana, basi familia hiyo itanunua nusu kilo ya maharage kwa Sh 1,400, mafungu ya mboga za majani kwa Sh 1,000, nyanya fungu Sh 500, vitunguu Sh 200, unga wa sembe kilo moja kwa Sh 2,400 na mafuta ya kupikia kwa Sh 800, ambayo jumla yake ni Sh 6,300.

Usiku: Familia hiyo itanunua kilo moja ya mchele kwa Sh 2,500 na kupika kwa kutumia mkaa na mboga zilizobaki mchana.

Kwa milo hiyo mitatu, familia itakuwa imetumia jumla ya Sh 12,700, ambayo ukizidisha kwa siku 30 unapata wastani wa Sh 381,500 kwa mwezi.

Ukokotozi huu haujahusisha nyama ya ng’ombe, kuku, mayai wala maziwa ambapo kwa mujibu wa familia zilizozungumza na gazeti hili, vitoweo hivyo hubaki kama anasa kwao.

Ripoti ya mwenendo wa uchumi ya Machi, mwaka huu iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilionesha kupanda kwa mfumuko wa bei za vyakula kutoka asilimia 5.2 Januari hadi asilimia 5.5 Februari, mwaka huu.

Jambo hilo limesababisha kupanda kwa bei za nafaka, hasa mahindi na hivyo unga wa mahindi, ndizi na maharage, huku vinywaji baridi navyo bei yake ikipanda.

Taarifa ya BoT pia ilisema kiwango cha kukua kwa mfumuko wa bei kwa vyakula na vinywaji visivyo na kileo ni asilimia 8.7 Februari, toka asilimia 7.6 ya Januari, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, mfumko wa bei wa Taifa kwa Machi, 2017, umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.4 kutoka asilimia 5.5 Februari, 2017.

Kuongezeka kwa mfumuko huo kunamaanisha kuwa, kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Machi, 2017 umeongezeka ikilinganishwa na kasi ya upandaji ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia Februari, 2017.

Taarifa hiyo inaonesha kwamba, mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi Machi, 2017 umeongezeka hadi asilimia 11.0 kutoka asilimia 8.7 ilivyokuwa Februari, 2017.

 Uchunguzi unaonesha bei za vyakula zimepanda sana ukilinganisha na miezi sita iliyopita. Kwa mfano, kilo moja ya maharage ambayo ilikuwa inauzwa Sh 2,000 Novemba mwaka jana, sasa inauzwa Sh 2,800. Kilo moja unga wa sembe sasa ni Sh 2,400 kutoka 1,800 za hapo awali.

Pamoja na kwamba familia zenye kipato cha chini ndizo zinazoteseka zaidi, lakini hata wale wenye kipato cha kati wameathirika sana na mfumuko wa bei, kwa mfano mtungi wa gesi wa kilo 16 uliokuwa unauzwa Sh 45,000 sasa umepanda hadi Sh 56,000. Hali hii inafanya nia ya Serikali kutaka huduma ya gesi kuwafikia watu masikini kuendelea kuwa ndoto.

Familia zenye kipato duni, hususan jijini Dar es Salaam, zinapata wakati mgumu sana kupangilia matumizi yao kwa siku na hata mwezi, hasa ukizingatia kuwa ukokotozi uliofanywa umezingatia chakula tu na kuacha matumizi mengine ambayo ni muhimu pia, kama bili mbalimbali za maji, umeme, kodi za nyumba, ada za watoto shuleni na nauli za daladala.

“Mimi sasa nimepunguza sana matumizi. Najibana sana. Zamani mlo wangu ulikuwa na matunda muda wote, lakini siku hizi mara nyingi mboga yangu kuu ni mboga za majani. Kuhusu vitafunio vya chai asubuhi, mimi na familia yangu tunatumia kiporo cha ubwabwa uliobaki usiku” anasema Daudi Kyando, mkazi wa Kimara Baruti.

Kyando aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa, siku wakipika ugali usiku basi yeye, mkewe na watoto wake watatu hunywa chai bila kitafunio.

“Pesa imebana sana siku hizi, inabidi niache vitafunio ili nijibane zipatikane nauli za watoto wa shule. Mambo magumu sana kaka,” alisema mkazi huyo wa jiji la Dar es Salaam, aliyedai kuwa yeye ni dalali wa viwanja.

Yete Gonde (45), mkazi wa Gongolamboto, anasema yeye siku hizi amebadili mlo na vikao vya jioni (baa) haendi.

Anasema yeye siku nyingine hanywi chai na hali ikiwa mbaya zaidi hata mchana unapita pasipo kuonja chochote, ili kuokoa pesa za kukidhi mlo wa watoto.

“Kaka ukichenji 10,000 inakwisha kabla hata hujakamilisha kununua bidhaa muhimu,” alisema.

“Kazi yangu ni mwalimu wa shule ya msingi, naishi nyumba ya kupanga. Mshahara hautoshi. Kwa hali ya hivi sasa lazima nijibane sana,” alisema Zuwena Mkamba (54), mkazi wa Kipawa jijini Dar es Salaam, aliyedai kuwa na watoto watano.

Kwa mujibu wa mama huyo, inamuwia vigumu kupanga bajeti, hasa ya chakula kwa familia yake, kwani gharama zimepanda sana.

Shirika la Chakula Duniani (FAO), katika uchunguzi wake wa hali ya chakula kwa nchi za Afrika Mashariki, linaeleza upungufu wa mvua kwa mwaka 2016 umesababisha kushuka kwa mavuno, hali ambayo imesababisha bei za vyakula kama mahindi kupanda.

Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili wamesema kutokana na hali kuwa ngumu, imewabidi waache baadhi ya matumizi yanayodaiwa kuwa ya starehe, kama unywaji bia ili kuhifadhi fedha ya ada za shule kwa ajili ya watoto wao.

Ugali ndicho chakula kikuu kwa familia nyingi hapa Tanzania. Hivyo kuongezeka kwa bei kunaziumiza familia nyingi.

Hivi sasa kunywa maziwa au kununua vitu kama vyama na mayai imekuwa ‘starehe’.

“Kama siku hizi mimi nimepunguza vikao vya jioni (kwenda baa) na hata nikienda nakunywa bia ya …. (anaitaja),” anasema Anania Julius, mkazi wa Ilala.

“Vitu vinazidi kuwa ghali sana. Hii hali lazima ikome, kwa vile tunakufa na tai shingoni. Hebu Rais wetu Magufuli (John) aingilie kati,” anasema Ashura Nurdin wa Tandika, jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba zake mbalimbali, Rais Magufuli amekuwa akiahidi kulishughulikia suala la mfumuko wa bei na kusisitiza nchi kutokuwa na janga la njaa.

Mara zote amekuwa akiwataka Watanzania kuchapa kazi kwa bidii, ili kuongeza kiwango cha mavuno, hali ambayo itapunguza bei za vyakula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles