22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

GGML yagawa vitanda vya kujifungulia katika vituo Nyankumbu, Kasamwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML), imetoa msaada wa vitanda vinne vya akina mama kujifungulia katika vituo vya afya vya Nyankumbu na Kasamwa vilivyopo kwenye Halmashauri ya Mji wa Geita mkoani Geita.

Mkuu wa wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe (wa nne katikati) akikata utepe kuashiria makabidhiano ya vitanda vya akina mama wajawazito kujifungulia kwa vituo vya afya vya Nyankumbu na Kasamwa. Wengine wanaoshuhudia ni baadhi ya watendaji wa vituo hivyo, pamoja na Meneja Mwandamizi mahusiano GGML, Gilbert Mworia (wa pili kushoto).

Msaada huo umekabidhiwa wiki iliyopita na Meneja Mwandamizi Mahusiano wa GGML, Gilbert Mworia kwa niaba ya wafanyakazi wanawake wa kampuni hiyo (GGGML) baada ya kupokea ombi la vituo hivyo vya afya kuhusu upungufu wa vitanda hivyo.

Alisema katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake iliyofanyika Machi mwaka huu, kampuni hiyo ilipokea ombi kuhusu uhaba wa vitanda vya kujifungulia kutoka kwa wanawake wa eneo hilo.

Aliongeza kuwa suala la afya na ustawi wa jamii ni jambo muhimu katika kila hatua ya maisha ya mtu yeyote anayekua, ndio maana kampuni ya GGML imeendelea kuboresha huduma za afya katika jamii inayozunguka mgodi huo na Tanzania kwa ujumla.

“Leo tunakabidhi rasmi vitanda hivi ambavyo wazo lake lilitokana na adha wanazopata akina mama wakati wa kujifungua, ugumu wa maisha ambao ulibainishwa na akina mama wa Geita. Waliwasilisha hili kwa Menejimenti na sasa tumechukua hatua ipasavyo kwa kusikia kilio chao,” alisema.

Aidha, akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vitandani hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe aliagiza timu ya madaktari wa vituo vya afya vya Kasamwa na Nyankumbu kutunza vitanda hivyo vya kujifungulia vilivyotolewa.

“Hatupati msaada wa aina hii mara kwa mara kwa hivyo ninawahimiza kila mmoja wenu hapa kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika suala la utunzaji mzuri wa vitanda hivi vilivyotolewa na GGML,” alisema.

Meneja Mwandamizi mahusiano GGML, Gilbert Mworia (wa pili kushoto) akizungumza katika hafla ya kukabidhi vitanda vilitotolewa na kampuni hiyo kwa ajili ya akina mama wajawazito kujifungulia katika vituo vya afya vya Nyankumbu na Kasamwa.

Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Nyankumbu, Irene Temba alipongeza GGML kwa msaada huo na kubainisha kuwa kituo hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto nyingi hususani katika upande wa huduma ya kujifungua.

“Tunarekodi watoto wasiopungua 300 kila mwezi jambo ambalo huwalazimu baadhi ya mama zetu kutumia vitanda vya kawaida wakati wa kujifungua. Tungependa katika siku za usoni, GGML ifikirie pia kutusaidia na vitanda vya kufanyia uchunguzi, samani na vifaa vingine kwa sababu kila mwezi hapa tunapokea zaidi ya kesi 1,000 za huduma ya afya ya uzazi na ujauzito. Pia tunatoa huduma kwa watu 1,000 kila mwezi katika Kituo cha Matunzo na Tiba,” alisema.

Aidha, mmoja wa wanufaika wa awamu ya pili ya vitanda vya kujifungulia katika Kituo cha Afya cha Kasamwa, Mganga Mfawidhi Thomas Mafuru pia aliipongeza GGML kwa kuisaidia Kasamwa.

“GGML ni rafiki mkubwa wa Kituo cha Afya cha Kasamwa. Tangu kituo kilipoanzishwa mwaka 2007, GGML imetoa msaada wenye thamani kubwa ikiwa ni pamoja na usambazaji wa vifaa vya afya na hata ujenzi wa uzio kuzunguka kituo chetu,” alisema.

GGML imekuwa kinara wa uwekezaji katika jamii tangu ilipoanzishwa mwaka 2000, huku vipaumbele vikubwa vya kampuni hiyo vikiwa ni afya, elimu, maji, barabara, miradi ya maendeleo na miradi mingine mingine ya kijamii inayolenga kuboresha ustawi wa jamii inayozunguka mgodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles