25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

Gekul aonya wanaojihusisha na uvuvi haramu

Na Mbaraka Kambona, Manyara

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amewataka wale wote wanaojihusisha na uvuvi usiozingatia sheria na taratibu kuacha mara moja kwani Serikali haitakuwa na huruma kwa watakaokamatwa.

Gekul alitoa onyo hilo alipokuwa akiongea na Wavuvi wa Mkoa wa Manyara alipofanya ziara mkoani humo jana Desemba 21.

Kwa mujibu wa Waziri Gekul katika operesheni ya kupambana na uvuvi haramu iliyopita ilitumika karibu bilioni 1. 2 jambo ambalo alisema halivumiliki na hivyo aliwataka wavuvi kutoa ushirikiano kwa serikali ili kukomesha vitendo hivyo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti alipomtembelea ofisini kwake Desemba 21, 2020. Waziri Gekul yupo mkoani Manyara kwa ziara ya Kikazi.

“Hatutavumilia jambo hili liendelee, Sisi kama Wizara tumesema ni lazima tupate muarobaini wa uvuvi haramu lakini na nyinyi wavuvi muwe tayari kutoa ushirikiano kwa serikali ili uvuvi haramu ukomeshwe mara moja,” alisema Gekul

Aliongeza kwa kusema kuwa uvuvi haramu ukikomeshwa itasaidia kuokoa mazalia ya samaki na kuongeza idadi ya samaki katika maziwa na maeneo mengine.

“Kwa kuwa mmeonesha nia ya kutoa ushirikiano katika hili, shirikianeni na viongozi wenu kuanzia leo hizo nyavu haramu zikatupwe, tusisikie tena kuhusu nyavu haramu iwe mwanzo na mwisho ,” aliongeza Gekul

Aidha, Waziri Gekul alisema kuwa kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa viumbe maji kwa kutumia Vizimba na Mabwawa jambo ambalo anasema likisimamiwa vizuri litaongeza ajira kwa wananchi na kupunguza umasikini na kuchochea uchumi wa taifa letu.

“Niwaombe Wakurugenzi na Viongozi wengine wa Halmashauri waangalie uwezekano kwenye zile asilimia kumi zinazotolewa na Serikali kwa Vijana, Wanawake na Walemavu badala ya kuwapa mkononi wafanye utafiti ili kujua ujenzi wa mabwawa unagharimu kiasi gani ili wawajengee mabwawa ya kufugia samaki na tukiweza kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza tatizo la ajira,” alisisitiza Gekul

Katika hatua nyingine, Gekul aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa uvuvi kuwafikia wavuvi wote na kuhakikisha wanalipia leseni za uvuvi ili kuzuia upotevu wa mapato na kukuza pato la Serikali.

“Hili litekelezwe haraka, kila mtu ajisikie vizuri kulipa kodi ya serikali, lipeni kodi na mpatiwe risiti za mashine za elekroniki kwa kufanya hivyo kutazuia upotevu wa mapato ya serikali,” alifafanua

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange alisema kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri wameyapokea na watayafanyia kazi kama ilivyoelekezwa ili sekta ya uvuvi mkoani humo iweze kupiga hatua inayotarajiwa.

“Tutahakikisha wavuvi wote tunawafikia kwa lengo la kutatua kero zinazowakabili lakini vile vile wale ambao hawana leseni waweze kukata leseni ili serikali iweze kuwatambua na kupata mapato kupitia shughuli za uvuvi,” alisema Twange

Mwenyekiti wa Wavuvi, Halmashauri ya Babati, Iddi Hassani alisema kuwa watafanyia kazi maelekezo na watahakikisha wanashirikiana na serikali ili wavuvi wote wawe na leseni za uvuvi na wataendelea kupambana na uvuvi haramu ili kunusuru viumbe maji na kuendelea kufanya uvuvi endelevu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles