NA CHRISTINA GALUHANGA-DAR ES SALAAM
MKOA wa Geita unaogoza miongoni mwa mikoa saba kwa kuwa na upungufu mkubwa wa madawati.
Jambo hilo limetajwa kuirudisha nyuma juhudi za serikali katika kuboresha elimu nchini.
Mbali na Geita, mikoa mingine ambayo haijakamilisha madawati ni Mwanza, Mara, Kigoma, Rukwa, Simiyu na Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, ametoa mwezi mmoja kwa viongozi wa mikoa hiyo kuondoa kero hiyo vinginevyo wajitumbue wenyewe kwa kushindwa kuendana na kasi ya Rais Dk.John Magufuli.
Simbachawene aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akipokea msaada wa madawati 3,500 yaliyotolewa na Benki ya NMB.
Alisema ni jambo la kusikitisha mikoa hiyo kushika nafasi za mwisho katika suala la kupatikana kwa madawati.
“Wapo wadau wengi ambao wameona umuhimu wa kuchangia elimu nchini lakini kwa mikoa hii inaonyesha jinsi ilivyofanya vibaya, nawaagiza hadi Januari wawe wamekamilisha upungufu huo vinginevyo viongozi wake wajing’oe wenyewe kwa sababu watakuwa hawawezi kuendana na kasi ya uongozi wa sasa,”alisema Simbachawene.
Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker, alisema hadi sasa benki hiyo imekabidhi kwa serikali madawati 10,000 ambayo yamesambazwa katika shule 71 nchini za sekondari na msingi.
“Mkakati wa NMB ni kuisaidia serikali kuondoa changamoto ya wanafunzi kukaa chini, hivyo tuna imani wanafunzi watapata elimu kwa kiwango kinachostahili,”alisema Ineke.