25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

Geita ilivyojipanga kudhibiti mimba za utotoni

Na Yohana Paul, Geita.

SERIKALI kupitia mpango wa kuinua uchumi kwa mkopo wa shilingi trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF), imedhamiria kukabiliana na athari za ugonjwa wa Uviko 19 kwa kuboresha miundombinu ya sekta ya afya na elimu.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule, akizungumuzia manufaa ya mradi huo, anasema, mkoa ulipokea jumla ya sh. bilioni 17.4 kufanikisha mradi.

Senyamule anasema pesa hiyo imetumika kujenga jumla ya vyumba 844 vya madarasa kupitia Mpango wa Kukabiliana na Virusi vya Corona Nchini (TCRP) ili kuboresha miundombinu ya kujifunzia shuleni.

Anasema kati yake, kiasi cha Sh Bilioni 14.84 ilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 742 kwenye shule za sekondari na sh. 2.4 kwa ajili ya ujenzi wa vituo shikizi na vyumba vya madarasa 102 katika shule za msingi.

Anaeleza, mradi huo umefungua milango ya wanafunzi wakiwemo watoto wa kike kujifunza pasipo kikwazo ambapo kwa mwaka huu wa masomo mkoa unatarajia kusaili wanafunzi 41,454 wa kidato cha kwanza.

Senyamule anakiri, mbali na maboresho ya miundombinu ya kujifunzia yaliyofanyika huenda tatizo la watoto wa kike kukatishwa masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba na kuolewa likaendelea kuwepo.

Anasema, kwa kulitambua hilo mkoa umejipanga kusimamia kikamirifu suala la elimu ya afya ya uzazi na elimu ya kijinsia kwa watoto wa kike sambamba na kusimamia kikamirifu sheria kwa watuhumiwa wa kosa hilo ili kuhakikisha mtoto wa kike anafikia ndoto zake.

“Yote hayo yanatokana na tabia za watu, na kubadilisha tabia za watu ni jambo gumu, na mara nyingi kuna njia mbili za kubadili tabia za watu.

“Aidha kwa kutumia sheria kwa umakini wake ndio maana sheria zipo, lakini zaidi sana kwa kutumia elimu, ili kubadilisha mitazamo ya watu na tabia zao.

“Sisi tunachokifanya pamoja na kwamba tutaendelea kusimamia sheria kwa umakini, na vyombo vinavyohusika vitachukua hatua linapotokea tatizo, lakini kwetu tunaona kungoja litokee tatizo pia haina faida kwa sababu madhara yanakuwa yameshatokea,” anaeleza.

Anaongeza “tumesema tuweke nguvu kubwa kwenye suala la uelimishaji, kupitia wataalamu wetu waliopo kwenye mambo ya ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii, lakini zaidi sana kwa kushirikisha wadau,”.

Mikakati ngazi ya Wilaya

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyangh’wale, Jamuhuri William, anaeleza kuwa kwenye wilaya yake kwa sasa hakuna tena kizuizi kwa mtoto ikiwemo watoto wa kike kusoma.

“Serikali imeshatekeleza jukumu lake, lakini mdau muhimu ni mzazi ambaye mtoto anatoka nyumbani kwake na kwenda shule,” anasema.

Anasema kama wilaya wamefanya vikao na watendaji wa vijiji, Kata, madiwani na mikutano ya hadhara kuwahamasisha wazazi kupeleka watoto shule hususani watoto wa kike.

“Kwa mtoto wa kike kiukweli anapaswa atazamwe kipekee sana, kwa sababu mazingira ambayo yanamuzunguka mtoto wa kike ni tofauti na mtoto wa kiume.

“Kwenye shule zetu tunao walezi wa watoto, kwa maana ya walimu wanaosimamia, maadili ya watoto, na kila wakati wanafuatiliwa, ili kujua mienendo yao pale shuleni vilevile mazingira wanakoishi,” ameeleza

Jamuhuri anakiri moja ya changamoto kubwa iliyopo ni watoto wengi kutembea umbali mrefu kufuata masomo mazingira ambayo ni hatarishi kwa mtoto wa kike.

Anaeleza kwa kuliona hilo wilaya yake baada ya kukamilisha mradi wa ujenzi wa madarasa sasa wamejipanga kujenga hosteli kwa ajili ya watoto wa kike ili kumuweka kwenye usalama zaidi.

Mhandisi Charles Kabeho ni Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, akifanya mahojiano na mwandishi wa makala hii anaeleza kwa mwaka huu wa masomo jumla ya wanafunzi 4487, wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wilayani humo.

Anasema, kikubwa kubwa zaidi wamejipanga kutekeleza sera ya elimu na miongozo ya serikali ili kumulinda mtoto wa kike asipate ujauzito na hatainapotokea basi asijione mkiwa na ndoto zake zisiishie pale.

“Sisi kama wilaya tunaendelea na utaratibu wa serikali, kila inapofika wakati tunawapima watoto ujauzito, na endapo itakapobainika kwamba kuna watoto wanapata ujauzito, basi kwa sababu sheria zipo tutawachukulia hatua wale waliowapatia ujauzito.

“Lakini tutahakikisha kwamba wanafunzi hawa waliolubuniwa, wao wanaendelea na masomo, hata kama akiwa ni mjamuzito,” aneleza Mhandisi Kabeho.

Kwa upande wa Wilaya ya Geita, Mkuu wa Wilaya hiyo, jamuhuri William anasema walipata Sh. Bilioni 9.3 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ambayo yameondoa kero ya misongamano madarasani.

Anaamini mradi huo utachagiza mahudhurio na wanafunzi kuacha utoro na kuweza kusaidia kuinua maendeleo ya kitaaluma kwa wanafunzi ikiwemo wanafunzi wa kike.

Shimo anaeleza, kwa wilaya yake imejipanga kikamirifu kusimamia sheria kwa wale watakaobainika kuwarubuni watoto wa kike wasiendelee na masomo.

“Lakini pia kwa watoto wetu wa kike cha kwanza tutoe onyo kwa watu ambao wanawapa vishawishi na kuchangia watoto kupata mimba.

“Tutakawenda kuchukua hatua kubwa sana kwa yeyote atakayehusika na kumukatiza mtoto wa kike masomo yake na hasa kwa sababu ya mimba akiwa shuleni,’ anasisitiza.

Ushauri wa Wadau Wa Elimu

Mkurugenzi wa Shule ya Msingi ya Kadama iliyopo kata ya Buselsele wilayani Chato mkoani Geita, Leticia Pastory anasema changamoto ya malezi, maadili, kupungua kwa hofu ya Mungu na tamaa za wazazi ndio mizizi ya tatizo la mimba za utotoni.

Anashauri ili kukabiliana na tatizo hilo ni lazima serikali isimamie suala la ujenzi wa hosteli kwa watoto wa kike, somo la dini liwekewe mkazo shuleni na kuzingatia usimamiaji wa sheria kwa kutoa hukumu thabiti wanaobainika kumulaghai mtoto wa kike.

“Adhabu kali zitolewe, zitolewe kisawasawa, watu hawapewi adhabu wanafanya vitendo hivo, lakini hawaadhibiwi, watu wanahonga,

“Mtu anabainika kabisa na vithibitisho, lakini wanahonga hela nyingi wanatoka, mtu akimuona mtu amefanya hivo na yupo mtaani na yeye kesho atafanya hayo,”

Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Maweni iliyopo kata ya Buseresere wilayani Chato, Winfrida Biteamanga, anashauri walimu, wazazi na jamii kwa ujumla kuwajibika kumulinda mtoto wa kike.

“Kwa hiyo wakipata nafasi ya kushauriwa, kuelimishwa kwamba haya utayafanya sasa hivi lakini yatasababisha kesho yako iwe mbaya inawezekana wakapunguza.

“Kinachotakiwa tu ni wazazi kuzungumuza na watoto, kutengeneza urafiki na watoto, watoto wapate ushauri na elimu,’ anasema Winfrida.

Anawakumbusha walimu pia wanao wajibu na nafasi kubwa kukaa na mwanafunzi, kumuelimisha, madhara ambayo atayapata endapo atajihusisha na masuala ya ngono katika umri mdogo.

Mkuu wa Shule ya Wasichana ya Nyankumbu iliyopo Mjini Geita, Georgia Mugashe anasema mambo muhimu kwa mtoto a kike ni elimu ya vijana kujikinga na mimba za utotoni na wao kukaa hosteli.

“Sisi ni mfano, watoto wote wapo ndani wapo hosteli na wote wapo salama, kwa hiyo ukiwalinganisha watoto wetu na wale wa shule nyingine za kutwa ni tofauti kubwa sana kitaaluma, kinidhamu,”

Anasema kwa shule hiyo ambayo imekuwa ikifanya vizuri mkoani Geita, suala la elimu ya uzazi endelevu kwa kutambua kuwa elimu hiyo inagusa masuala mtambuka mtambuka.

“Shuleni kuna kampeni mbalimbali, elimu ya uzazi, kwa vijana inatolewa, hivo hivo na hata jumatatu huwa tunawapitisha tena kuwapa wote elimu hiyo wanapokuwa paredi,’ anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles