24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Gambia na mgombea urais aliyeahidi kuhalalisha bangi

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

HEKAHEKA za Uchaguzi Mkuu zinaendelea nchini Gambia, huku ukitarajiwa kufanyika Desemba 4, mwaka huu. Rais aliyeko madarakani, Adama Barrow, anamaliza awamu yake ya kwanza aliyoianza mwaka 2017 alipochukua nafasi ya Yahya Jammeh aliyeondoka madarakani akiwa amekaa Ikulu kwa miaka zaidi ya 22 (1994-2017).

Mwezi uliopita, Rasi Barrow alifanya kile alichokina kinaimarisha uwezekano wake wa kushinda awamu ya pili katika uchaguzi huo. Alichokifanya ni kuutangazia umma kuwa Chama chake, National People’s Party (NPP), kimeungana na APRC kinachoongozwa na mtangulizi wake, Jammeh.

Hata hivyo, wakati Rais Barrow akihisi kuungwa mkono na Jammeh ni fursa kwake katika uchaguzi ujao, wengi wanaitafsiri hatua yake hiyo kuwa ni ‘kujichimbia kaburi’. Wananchi wengi walioteseka chini ya utawala wa kidikteta wa Jammeh wanahisi ushindi wa Rais Barrow utamrejeshea nguvu kiongozi huyo aliyekimbilia Guinea ya Ikweta tangu alipoondoshwa madarakani mwaka 2017.

Kwa upande mwingine, kile kinachoweza kuwa hatari kwa Rais Barrow katika Uchaguzi Mkuu ni kwamba wananchi walio wengi wameanza kuhisi amewadharau kwa kitendo chake cha kuungana na APRC kwa sababu anafahamu kila kitu juu ya mateso waliyopitia chini ya utawala wa kimabavu aliokuwa nao Jammeh. Itoshe kuishia hapo juu ya Rais Barrow na mtangulizi wake, Jammeh.

Katika vyama vya siasa 18 vilivyosajiliwa, huku wapiga kura wakitajwa kuwa ni zaidi ya milioni moja, yupo mgombea aliyevuta hisia za wengi katika siasa za Gambia kuelekea Desemba 4. Si mwingine, bali ni Bankole Yao Jojo Ahadzie, wengi wakimfahamu kwa jina la ‘Banky’.

Akiwa na umri wa miaka 43, Banky kutangaza nia ya kuwania kiti cha urais isingetosha kuwa sababu ya kuwa gumzo katika medani ya siasa za taifa hilo la Magharibi mwa Afrika. Pai, hata elimu yake ya uhandisi wa mitandao nayo isingekuwa kigezo cha kumfanya awe kivutio kwa walio wengi.

Kilichomfanya awe kwenye macho na masikio ya wengi ni mwonekano wake wa rasta. Kwamba kama atashinda kiti cha urais, basi Banky mzaliwa wa Banjul, Mji Mkuu wa Gambia, atakuwa ameingia kwenye kitabu cha historia kwa kuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo kuingia Ikulu akiwa na staili hiyo ya nywele.

Iko wazi kuwa wafuasi wengi wa mtindo wa nywele wa rasta wamekuwa wakihusishwa na tabia za ajabu, kubwa ikiwa ni uvutaji wa bangi, lakini kundi hilo hujivunia ushawishi mkubwa kwa vijana wa Gambia, Afrika na maeneo mengi duniani, vikiwamo visiwa vya Jamaica, Haiti na Barbados.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Banky aliyesindikizwa na marasta wenzake, aliwaomba raia wa Gambia kuachana kuhukumu mwonekano wake na kumuona asiyefaa, na badala yake wampe tiketi ya kwenda kuunda Serikali itakayowaletea maendeleo. “Msinihukumu kwa mwonekano wangu wala mtindo wa nywele, sikilizeni sera zangu na ninavyoweza kubadili maisha yangu pindi nitakapochaguliwa,” alisema.

Banky aliweka wazi kuwa atashindania kiti cha urais bila kupitia chama cha siasa, kwa maana ya mgombea binafsi, na katika sera zake amejikita katika mambo matano; elimu bila malipo, ajira zenye mishahara minono, maendeleo, michezo, na marekebisho ya Katiba kulazimisha urais wa muhula mmoja.

Juu ya sera ya rais kuongoza muhula mmoja, alisema kukaa Ikulu kwa zaidi ya muda huo ni kujinufaisha na si kuwatumikia wananchi. Katika michezo, Banky aliahidi Serikali atakayoiunda itawekeza kwenye soka kiasi cha Dola za Marekani bilioni moja, akiamini itaifanya Ligi Kuu nchini humo iwe bora na kuvuta wachezaji wa kigeni.

Aidha, mbele ya waandishi, Banky aliweka wazi msimamo wake wa kuhalalisha kilevi aina ya bangi mara tu atakapopewa ridhaa ya kuingia Ikulu. Katika kuilinda hoja yake hiyo, amesema Gambia haiwezi kubaki nyuma wakati mataifa mengine barani Afrika yamekuwa yakiingiza mabilioni ya dola kutokana na biashahara ya kusafirisha bangi.

Kile kinachoweza kutafsiriwa kuwa ni dalili njema kwake kuelekea kinyang’anyiro cha Desemba 4, tayari Umoja wa Marastafari nchini Gambia umeshampa udhamini, huku yeye akiamini atapata ‘sapoti’ kubwa ya vijana kwa kuwa kundi hilo limeshachoshwa na ahadi zisizotimia kutoka kwa wanasiasa waliopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles