UCHUMI wa Tanzania kwa kiasi kikubwa unategemea sana kilimo ambacho kimeajiri karibu asilimia 80 ya Watanzania.
Hata hivyo pamoja na kuajiri Watanzania wengi kilimo bado kinachangia kidogo katika Pato la Taifa.
Kulingana na Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2014, kilimo kimechangia kwa asilimia 23 katika pato la nchi na takriban asilimia 30 katika mauzo ya nje.
Wingi na ubora wa mazao yanayozalishwa unaashiria fursa ya kufanya biashara ya tija.
Aidha kukua kwa soko la mazao kunakotokana na kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya watu duniani kunaashiria kuongezeka kwa mahitaji ya chakula na kuuza katika masoko ya nje.
Kwa kutambua umuhimu wa fursa hizo, Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) iliendesha mafunzo kwa wananchi kuhusu fursa mpya katika kilimo biashara.
Katika mafunzo hayo washiriki walielimishwa kuhusu shamba kitalu, kilimo bila kutumia udongo, ujasiriamali, ufugaji samaki katika mabwawa, matanki na vizimba, chakula cha mifugo na mbolea na ufugaji bora wa kuku.
Mkurugenzi wa ESRF, Dk. Tausi Kida, anasema kukua kwa teknolojia duniani kumeongeza fursa nyingi katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwano kilimo.
Anasema walifanya utafiti katika wilaya za Bukoba Mjini, Sengerema, Bunda, Ilege na Nyasa na kujifunza mengi kuhusu fursa zilizoko katika kilimo biashara.
“Teknolojia imewezesha wakulima katika sehemu mbalimbali duniani kutokutegemea tena mvua, wakulima kutumia eneo dogo la ardhi kuzalisha mazao mengi yaliyo bora, wakulima sasa wanaweza kupata taarifa mbalimbali kuhusu kilimo cha kisasa toka kwa wataalamu kwa haraka hivyo kusaidia kupata mavuno mengi na bora,” anasema Dk. Kida.
Ufugaji wa samaki
Ofisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, John Mapunda, anasema kutokana na ongezeko la watu na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, mahitaji ya samaki yameendelea kuongezeka siku hadi siku, hivyo kusababisha uzalishaji samaki kutoka kwenye vyanzo vya asili kupungua kwa kasi.
“Ili kukabiliana na upungufu huu hivi sasa tunahamasisha sekta binafsi kuingia katika ufungaji wa samaki ili kutosheleza mahitaji ya soko. Tunahamasisha wananchi watumie teknolojia mpya ya vizimba ambayo huwezesha kuzalisha samaki wengi katika eneo dogo,” anasema Mapunda.
Ofisa huyo anasema samaki wanaozalishwa kupitia ufungaji wa kisasa ni tani 10 tu lakini kuna fursa zaidi ya tani 200,000. Alisema malengo ni kuzalisha tani 100,000 kufikia mwaka 2021.
Kilimo bila udongo
Abdullatif Mbulo ni mtaalamu wa teknolojia ya kulima bila kutumia udongo, anasema kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia inawezekana kuendesha kilimo bila kutegemea ardhi.
“Udongo si lazima unaweza kulima kwenye maji au kwenye mawe na tunafanya hivi hasa kwa kulima mboga mboga kule Ruvu (Pwani) na Bunda (Mara),” anasema Mbulo.
Anasema kilimo hicho kinaweza kufanywa katika mfumo wa vyumba visivyotumika, mabanda ya uani na majengo yaliyotelekezwa nyumbani kwako.
Anasema kilimo hicho ni rahisi na chenye tija na kinaweza kumkomboa mjasiriamali au mkazi wa miji mikubwa ambayo kuna shida ya kupata ardhi za kuendesha shughuli za kilimo.
Teknolojia ya shamba kitalu (green house)
Teknolojia ya shamba kitalu ni aina ya mabanda yanayojengwa na kuzungushiwa vyandarua maalumu ambavyo husaidia kuchuja mionzi ya jua isiyofaa na kuzuia wadudu wasiingie ndani ya mimea
Mkuu wa kitengo cha ujasiriamali katika Taasisi ya Usimamizi na Maendeleo Iringa (iMADS), Dominick Haule, alihamasisha watu kutumia teknolojia hiyo ina sifa pia ya kuyafanya mazao kukua kwa haraka na kuwa na ubora unaotakiwa.
“Ubora wa mazao ni changamoto kwa wakulima wengi wa Tanzania, lakini kwa kutumia teknolojia hii mkulima ana uhakika wa kutumia gharama kidogo na kuvuna mazao bora,” anasema Haule.