NA CHRISTOPHER MSEKENA
MWANAMUZIKI wa muziki wa Injili nchini, Frank Kikungwe anatarajia kuachia albamu yake ya kwanza inayoitwa ‘Nimeuona Mkono wa Bwana’ kesho katika Kanisa la KKKT, Usharika wa Kimara, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Swaggaz, Kikungwe alisema, albamu hiyo ina jumla ya nyimbo nane za kumsifu na kumuabudu Mungu ambazo zimejaa mafundisho katika maisha ya wanadamu.
“Baada ya misa ya kwanza kumalizika ndipo onyesho la uzinduzi litakapoanza, watu wote wanakaribishwa kuhudhuria uzinduzi huu kwani watapata nafasi ya kununua nakala halisi ya albamu yangu,” alisema Kikungwe na kuongeza:
“Ina nyimbo nzuri sana kama Peke Yangu Siwezi ambazo zinarudisha watu kwenye mstari na kuwaweka karibu na Mungu wetu wa upendo.”
Alisema albamu hiyo ipo katika mfumo wa sauti yaani Audio na mapato yatakayopatikana kupitia mauzo ya albamu hiyo yatamsaidia kutengeneza video.
“Mashabiki wangu wamenisikia, bado tu kuniona kwenye video, nilikuwa na upungufu wa fedha kidogo kwa ajili ya kufanya video lakini nadhani mauzo ya albamu hii yatanisaidia kukamilisha mpango wa video,” alisema Kikungwe.