Elizabeth Joachim Dar es salaam
Bendi ya First Class Modern Taarabu inatarajia kuzindua albamu mpya ya ‘Mama wa Hiyali’ Jumamosi Novemba 10 Hoteli ya Travetine Magomeni jijini Dar Es Salaam.
Mkurugenzi wa Bendi hiyo, Aboubakar Soud (Amigo) amesema albamu hiyo imebeba nyimbo sita huku wimbo mmoja wakimshirikisha msanii nguli wa nyimbo za taarabu, Khadija Kopa.
Amigo amesema katika uzinduzi huo utahudhuliwa na Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Omary Kumbilamoto na wasanii ws taarabu, Khajida Kopa, Hawa Sabaha Salum na Patricia Hillary ambao pia watatumbuiza katika uzinduzi huo.
“Nimekuja kurejesha heshima ya muziki wa taarabu baada ya Mzee Yusuph kustaafu kwenye uzinduzi huu kutakuwa na vionjo vingi,” amesema Amigo
Naye Mkurugenzi wa Mipango wa bendi hiyo, Said Safi amesema kundi hilo lenye wasanii 10 lilianzishwa Februari 14 Mwaka huu na limeanzishwa baada ya kuona muziki wa taarabu ukipoteza washabiki baada ya Mzee Yusuph kuacha kujihusisha na muziki.