26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Filikunjombe awavaa mawaziri wa JK

Deo filikunjombeNa Mwandishi Wetu, Njombe
MBUNGE wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), amewavaa mawaziri walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, hasa wanaotoka Mkoa wa Njombe, kwamba wameshindwa kuusaidia mkoa huo kuweza kupiga hatua ya maendeleo.
Amesema hatua ya kushindwa kwao inawafanya mawaziri hao kubaki kuwa viongozi walalamikaji.
Hayo aliyasema jana katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), kilichofanyika mjini Njombe, baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Rehema Nchimbi, kuwataka wajumbe hao kujadili namna ya kutumia Sh bilioni 158.6 kwa ajili ya bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016.
Baada ya kutolewa hoja hiyo, alisimama Filikunjombe kuchangia, ambapo alipingana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge pamoja na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Pindi Chana waliotangulia kuchangia, ambao wote waliwataka watendaji wa Serikali wawajibike.
Filikunjombe, alisema kwa upande wake asingependa kuchangia suala hilo kwani wapo mawaziri katika Mkoa wa Njombe ambao ndio wapo jikoni, hivyo ni matumaini yake angesikia majibu yao badala ya kuishia kulalamika.
“Kweli mimi kunitaka niseme hapa ni kunionea kwani humu ndani katika kikao chetu tunao vijana wetu ambao ni mawaziri, sasa ni vema wao kusema zaidi na sio kuishia kulalamika.
“Kwa maoni yangu binafsi ningependa sana kila mmoja kutimiza wajibu wake, Serikali itimize wajibu wake, wabunge na watendaji pia hivyo hivyo… kuna shida, hapa tunapanga mambo, tunawapangia hadi wahisani halafu baadaye tunaanza kulalamika,” alisema.
Filikunjombe aliwataka watendaji serikalini kuacha kuwa walalamikaji na badala yake kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa pale walipo.
Alisema kuwa ilipendeza mawaziri hao ambao ndiyo Serikali Kuu kuzipongeza halmashauri za Mkoa wa Njombe kwa kufanikisha kukusanya mapato kwa asilimia 40 badala ya kutoa majibu ya kulalamika, huku halmashauri hizo zikiendelea kuidai Serikali Kuu fedha zao za ushuru wa mazao.
Pamoja na hilo, alieleza kusikitishwa na baadhi ya watu wanaotaka nafasi za uongozi kwa kutumia mauaji ya albino ambapo alimwomba mkuu wa mkoa huo, Dk. Nchimbi, kuwaandikia barua viongozi wa taasisi za dini na vyama vya siasa ili kusaidia kukemea suala hilo kabla ya kuingia mkoani hapo.
Katika kikao hicho, Dk. Chana aliungana na Dk. Nchimbi kupinga vitendo vya ukatili wa adhabu za viboko zaidi ya vitatu kwa wanafunzi nchini.
Alisema pamoja na hali hiyo, anapinga na kukemea tabia ya baadhi ya wazazi wanaowafundisha watoto wao wa kike masuala ya uzazi wa mpango na kusema suala hilo halina budi kukomeshwa mara moja.
Wakati huo huo, Dk. Nchimbi ameagiza wanafunzi wa shule za msingi kuvaa sare za suruali badala ya kaptula kama ilivyoagizwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kama njia ya kukabiliana na baridi.
Alisema kutokana na hali ya hewa ya baridi kali katika Mkoa wa Njombe, ni vema viongozi mkoani hapa kuangalia uwezekano wa kufanya mabadiliko ya sare hizo za wanafunzi ili wavae suruali.
Dk. Nchimbi alisema hali ya hewa ya Mkoa wa Njombe ni ya baridi kali, hivyo kuna haja ya wanafunzi hao kulindwa kiafya zaidi kwa kubadilishiwa sare hizo ili kuvaa suruali kwa ajili ya kujisitiri na baridi kali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles