*Ndalichako, Dk. Tulia wazua balaa Kinondoni
*Mtoto wa Sitta meya mpya, Ubungo uchaguzi wakwama, Ukawa kutua kortini
JONAS MUSHI Na VERONICA ROMWALD
DAR ES SALAAM
NI Figusufigisu uchaguzi wa umeya Dar! Ndivyo unavyoweza kusema hasa baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kufanikiwa kushinda umeya wa Manispaa ya Kinondoni, huku vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vikitangaza kwenda mahakamani kupinga uchaguzi huo.
Uchaguzi huo uliofanyika jana huku katika Manispaa ya Ubungo, ukiahirishwa kwa kile kilichodaiwa kutofuatwa kwa taratibu za uchaguzi ikiwemo kuhamishwa kwa wapiga kura kinyume cha sheria.
Baada ya mvutano na vita ya maneno iliyodumu kwa takribani mwezi mmoja baada ya kuvunjwa kwa Manispaa ya Kinondoni ili kuruhusu kufanyika uchaguzi kwa manispaa hizo, hali ilikuwa tofauti baada ya madiwani wa Ukawa kususia uchaguzi wa meya wa Kinondoni na kudai kwamba Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Aron Kagurumjuli, ameshirikiana na CCM kuhujumu zoezi hilo.
Moja ya njama zinazodaiwa kufanywa na mkurugenzi huyo ni kugawanya madiwani kinyume na kanuni kwa kuhamisha madiwani wa upinzani kwenda Halmashauri ya Ubungo na kuwahamishia Kinondoni madiwani wa CCM kutoka halmashauri nyingine.
Mapema jana katika Ofisi za Halmashauri ya Kinondoni madiwani wa vyama vyote waliwasili tayari kwa kufanya uchaguzi lakini baada ya muda madiwani wote wa upinzani walitoka nje ya ukumbi.
Akizungumza na waandishi wa habari mbele ya wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema wametoka kwenye uchaguzi baada ya baadhi ya madiwani wao kuzuiwa kuingia kwenye kikao hicho.
Mbali na hilo alisema CCM wameingiza madiwani ambao si wajumbe halali wa kikao hicho kwasabau wanatoka katika halmashauri zingine.
“Madiwani wa Ukawa tumetoka kwa sababu hatuwezi kukubali figisu na ukiukwaji mkubwa wa kanuni na taratibu kwa lengo la kuwanyima haki wananchi wa Kinondoni,” alisema Mdee.
“Mkurugenzi wa halmashauri kwa makusudi hakuwaandikia barua madiwani wetu wawili kuwajulisha kuhusu uchaguzi na leo (jana) wamekuja kupata haki yao ya kushiriki uchaguzi lakini wamezuiwa kwa madai kwamba wao si madiwani wa Kinondoni.
“Lakini wakati mkurugenzi akifanya njama za kupunguza madiwani wetu amewaingiza katika kikao madiwani wa CCM wateule wa Rais ambao si wajumbe halali wa kikao kwasababu wanatoka halmashauri zingine,” alisema Mdee.
“Humo ndani yumo Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na alisajiliwa kama mkazi wa Ilala na alipiga kura za umeya Ilala hivyo mnaweza kuona uhuni unaofanywa.
“Lakini yumo pia Tulia Akson (Dk. Tulia Akson, Mbunge wa Kuteuliwa na Naibu Spika) ambaye si mkazi wa Kinondoni yeye amesajiliwa kama mkazi wa Ubungo,” alisema Mdee.
Pia alisema kwa mujibu wa kanuni halmashauri moja haiwezi kuwa na wabunge wa kuteuliwa zaidi ya watatu na kueleza kuwa katika kikao hicho wamo wabunge wanne wa kuteuliwa.
Alisema kutokana na hali hiyo watakwenda mahakama ili kupata tafsiri za kisheria za suala hilo kupata haki.
Hata hivyo Mdee alisema uchaguzi huo usingeweza kufanyika kwa sababu idadi ya wajumbe wa CCM waliopo isingeweza kutimiza akidi.
“Uchaguzi hauwezi kufanyika kwa sababu wajumbe waliopo wa CCM ni 18 na akidi ambayo ni theluthi mbili ya madiwani wote ni wajumbe 24,” alisema Mdee.
MBOWE AKUMBUKA UKUTA
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye naye alifika eneo la tukio alisema “Hiki si kipindi cha kawaida na awamu ya tano si awamu ya nne”
Alisema demokrasia, Katiba na sheria haziheshimiwi na kwamba Jeshi la Polisi limekuwa wakala wa CCM na kinachofanywa kwenye uchaguzi huo kinawapa sababu ya kurejea operesheni yao wanayoiita Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA).
“Kwa hila kama hizi ndio maana tulianzisha Ukuta ili kupambana na mambo kama haya kwamba hakuna mtu atakayekuwa salama katika utawala kama huu na sasa wanatupa ajenda ya kurejea kwenye Ukuta na tutarejea”
Alisema kiongozi ambaye hajawekwa na watu bali amepachikwa na dola hawezi kuwa kiongozi halali.
“Huyo Meya wao wa ‘magumashi’ wanayefikiria watampata mimi nina imani hana baraka za wananchi hana baraka za Mungu na sisi hatuwezi kumpa baraka,” alisema Mbowe.
Mbowe aliendelea kwa kumlaumu Rais Dk. John Magufuli kwamba ameanzisha utamaduni wa kuuwa demokrasia na kwamba analiletea taifa madhara makubwa.
Alisema Serikali inaendeshwa kwa hila kwani licha ya uchaguzi kufanyika siku ambayo si ya kazi mkurugenzi huyo alikataa barua iliyoandikwa na madiwani Jumamosi Oktoba 22 kuzuia uchaguzi huo kwa kudai kuwa si siku ya kazi.
WAANDISHI WAZUIWA
Katika hali ya kushangaza uchaguzi huo ulifanyika mbele ya waandishi wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali na CCM baada ya waandishi wa vyombo binafsi kuzuiliwa kuingia ndani ya geti la halmashauri hiyo.
Mapema asubuhi waandishi wakiwa wanataka kuingia ghafla walizuiliwa na askari na baada ya muda alifika mmoja wa maafisa habari wa halamashauri hiyo akiwa na karatasi ambayo alimkabidhi askari aliyekuwa getini.
Askari huyo alianza kuita vyombo vya habari vilivyoorodheshwa katika karatasi hiyo vikiwemo, Gazeti la Uhuru, Habari Leo, Daily News, na Televisheni ya Taifa (TBC).
Baada ya kusoma orodha hiyo askari huyo aliawaamuru waandishi wengine kubaki nje kwani hawatambuliki katika mkutano huo.
ASKARI WATANDA
Wakati wote wa zoezi la uchaguzi likiendelea askari wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliovalia sare na wasiovalia sare walitanda maeneo yote yanayozunguka ofisi hizo.
Hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia ndani ya uzio huo wakiwemo waandishi wa habari huku wafuasi wa vyama vya CCM na Chadema wakifurika katika eneo la uchaguzi.
MEYA ATANGAZWA
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya mkutano huo uchaguzi ulifanyika ambapo wajumbe 18 wa CCM walipiga kura na kumchagua kwa kura zote Diwani wa Kata ya Msasani, Benjamin Sitta kuwa Meya huku Diwani wa Kata ya Kigogo, Mangulu Manyama akichaguliwa kuwa Naibu Meya.
Baada ya uchaguzi huo Mkurugenzi aliwatangaza Meya na Naibu wake huku akisisistiza kuwa kutokuwepo kwa madiwani wa upinzani hukujaathiri uchaguzi huo.
MASHINJI
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, muda mchache baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, alisema hawamtambui Meya huyo kwani hajachaguliwa na kikao halali.
“Hatuwezi kusema uchaguzi umefanyika na meya amechaguliwa kwasababu hakuna kikao kilichofanyika na madiwani wa Ukawa wametoka bila kusaini hivyo si kikao halali,” alisema Dk. Mashinji.
MKURUGENZI AJITETEA
Akitoa ufafanuzi kuhusu uchaguzi huo Mkurugenzi wa Manispaa ya hiyo, Aron Kagurumjuli, alisema taarifa ya kufanyika kwa uchaguzi huo ilitolewa kwa mujibu wa sheria kwa wahusika kupokea barua za kufahamishwa.
Alisema kwa sababu hiyo, kujitoa kwa madiwani wa Ukawa, hakutaathiri kuendelea kwa uchaguzi huo kwani unafanyika kihalali.
“Wajumbe wote walipata barua ya wito na kuzipokea kupitia “dispatch” lakini baadhi yao, wamefika na kugoma kuingia ndani.
“Kukaa kwao nje hakutuzuii kuendelea na uchaguzi kwa sababu taratibu zote zimefuatwa,” alisema Kagurumjuli.
Alisema madai kuwa, Mbunge wa Viti Maalum, Susan Lyimo (Chadema) kuwa ni mkazi wa Kinondoni hayana ukweli kwani mbunge huyo anaishi eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivyo ni mkazi wa Ubungo na anapaswa kushiriki kwenye vikao vya baraza la madiwani kwenye wilaya hiyo mpya.
Akizungumzia uamuzi huo ambao pia umemgusa Mbunge wa Viti Maalumu, Salma Mwasa (CUF), alisema yeye ni mkazi wa Kimara na kwa sababu hiyo alipaswa kushiriki vikao hivyo kupitia Manispaa ya Ubungo na si Kinondoni.
Pamoja na hali hiyo pia alitoa ufafanuzi kuhusu wabunge wateule wa Rais ambao wanaitumikia manispaa hiyo kama madiwani huku akishindwa kueleza kwamba tayari wengine walishakula kiapo Manispaa ya Ilala.
Kagurumjuli alisema wabunge hao wanateuliwa na Rais kwa majukumu maalumu na hawana mchakato.
Licha ya hali hiyo alionya kuwa endapo madiwani wa Ukawa wasipohudhuria vikao vitatu mfululizo vya Baraza hilo, watakuwa wamejiondoa kwenye nafasi hizo na kwa mamlaka aliyokuwa nayo ataitisha uchaguzi mwingine kwenye kata zao.
Aliagiza kusomwa barua iliyoandikwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala, ikifafanua kuhusu makazi ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Barua hiyo ilieleza kuwa, Profesa Ndalichako ni mkazi wa Manispaa ya Kinondoni na anawajibu wa kuitumikia manispaa hiyo.
Baada ya maelezo hayo Katibu Tawala wa manispaa hiyo, Gift Msuya, alitoa nafasi ya kula kiapo kwa Profesa Ndalichako, kuitumikia Manispaa hiyo kama diwani.
UBUNGO WAKWAMA
Kwa upande wa Manispaa mpya ya Ubungo uchaguzi hakujafanyika baada ya madiwani na wabunge wa Chadema kudai Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, John Kayombo kutofuata utaratibu unaotakiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Diwani wa Ubungo ambaye pia ni mgombea wa umeya, Bonface Jacob alidai wamefikia uamuzi wa kutokupiga kura kwani uchaguzi huo unaonyesha wazi kuwa umejaa figisu nyingi.
“Madiwani walipewa barua za kufanyika kwa kikao usiku wa Oktoba 20, mwaka huu, walikuwa wanapiga simu na kuwapelekea majumbani lakini cha kushangaza baadhi ya wajumbe akiwamo Mbunge wa Ubungo, Saed kubenea hajapewa barua ya kikao hicho,” alidai.
Alidai barua hiyo haikufuata utaratibu unaotakiwa na kwamba ilieleza kuwa utakuwa mkutano wa baraza la madiwani na si uchaguzi wa meya.
“Sasa kwa kawaida uchaguzi wa meya huwa ni open ‘wa wazi’ lakini baraza huwa si la wazi ndiyo maana hata ninyi waandishi mmezuiliwa nje, lakini barua ile haijaeleza pia madiwani wa wapi ni wa Ubungo na wapi ni wa kinondoni.
“Kwa hiyo haieleweki idadi ya wajumbe watakaopiga kura hiyo, kiutaratibu viongozi walipaswa kuitwa na kuelezwa ili wajue wapiga kura wao lakini wakurugenzi hawakuita viongozi badala yake walijipa kazi ya ‘ku-point’ orodha ya wapiga kura.
“Yaani CCM wanajua kabisa tunashinda ila wanataka tugawane uongozi kama vile tunagawana chapati, kwamba wewe chukua hii mimi nichukue hiyo jambo ambalo haliwezekani,” alidai.
Akitolea mfano alidai wanashangaa kuona jina la Calorine Kazinza aliyekuwa Diwani Viti Maalumu Chadema ambaye alifukuzwa uanachama lakini jina lake limeorodheshwa kama mpiga kura wa Manispaa ya Ubungo.
“Suzan Lyimo, Diwani wa Viti Maalumu (Chadema) Kinondoni jina lake limeandikishwa kupiga kura Ubungo, Salma Maswa (CUF) viti maalumu Kawe badala ya jina lake kuwapo Kinondoni, limewekwa Ubungo na Leila Madibi katolewa Kinondoni kaletwa Ubungo jambo ambalo ni kinyume na utaratibu,” alidai.
Pamoja na hali Jacob alisema kuwa Diwani wa Viti Maalumu Saranga Florence Masunga (CCM), amepelekwa Kinondoni wakati anapaswa kupiga kura Ubungo.
Alidai zipo ishara za wazi kuwa wakurugenzi wamepokea maagizo kutoka juu yanayowataka kuhakikisha Manispaa ya Ubungo na Kinondoni zinakuwa chini ya CCM.
Naye Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) alisema kutokana na hali hiyo, ni vema Rais Dk. John Magufuli akajitokeza hadharani na kutoa kauli juu ya chaguzi hizo.
“Ujumbe wangu kwa Rais Magufuli vita hii ya umeya Kinondoni, Ubungo hawezi kuishinda kama ambavyo nilimwambia kuwa Jiji hawezi na akajitokeza hadharani na kusema Demokrasia ichukue mkondo wake afanye hivyo kwa chaguzi hizi,” alisema.
“Huyu Florence aliomba kuwa mjumbe wa kamati ya Mfuko wa Jimbo la Kibamba lakini leo (jana) jina lake limeorodheshwa kupiga kura Kinondoni, haiwezekani, tutafanya kila juhudi kuhakikisha hila hizi hazifanikiwi,” alisema.
DC AJIFUNGIA
Baada ya wajumbe kutoka ndani ya kikao hicho , waandishi walimfuata Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humfrey Polepole ili azungumze sakata hilo, lakini hata hivyo alikataa.
“Jamani leo siwezi kueleza lolote,” alisema na kuingia ofisini.
DED AGOMA
Naye Kayombo ambaye ndiye Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, alipotakiwa kuzungumza alikataa huku akiwataka waandishi kuwatafuta maofisa habari.
“Mimi nimeshamaliza kila kitu, nina ma Pr wengi wameajiriwa kwa kazi hiyo, watafuteni mzungumze nao,” alisema.