Accra, Ghana
Shirikisho la soka ulimwenguni (FIFA) limeongeza muda wa adhabu na marufuku kwa raisi wa chama cha soka nchini Ghana, (GFA) Kwesi Nyantakyi, kwa siku arobaini na tano zaidi.
Kwesi, alipigwa marufuku hiyo na mahakama ya Kamati ya Maadili ya FIFA Juni, 8 mwaka huu na nyongeza ya adhabu hiyo itaanza kutekelezwa Septemba 6.
Kamati hiyo inafanya uchunguzi rasmi dhidi ya Nyantakyi, baada ya kupigwa picha za video aliyorekodiwa kwa siri na mwandishi wa habari nchini Ghana, Anas Aremeyaw, akipokea kitita cha dola 65000 sawa na shilingi million 148.2 kutoka kwa mwandishi mwingine wa habari aliyejifanya ni mfanyabiashara.
Baada ya kuadhibiwa na (FIFA), Nyantakyi, alichukua uamuzi wa kujiuzulu nyadhifa zake kama mjumbe wa bodi ya shirikisho la kimataifa, (FIFA), na nafasi nyingine katika Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).
Licha ya kashfa hiyo aliyoipata na ushahidi wa picha za video, Nyantakyi, amekuwa akikana makosa yake.