25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Fidel Castro ni gofu, kriketi na vidosho

Fidel Castro kwenye Baseball
Fidel Castro kwenye Baseball

NA MARKUS MPANGALA

ABEID Karume na Julius Nyerere wanafahamika kama marais waliopendelea kucheza mchezo wa bao. Nelson Mandela alipendelea mchezo wa masumbwi, na alihusudu kukutanisha wanandondi kama Mike Tyson, Evander Holyfield na Lennox Lewis.

Kwa maana hiyo, kila kiongozi anakuwa na mchezo mmoja au miwili na pengine zaidi wanayopendelea kuicheza katika muda wao wa mapumziko.

Nyerere hakuonekana kupenda mchezo wa soka kama Jakaya Kikwete, ambaye pia alipendelea mchezo wa kikapu, soka na muziki wa zamani na Bongofleva. Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa hakuwa  mpenzi wa michezo, ingawa nina hakika alipendelea mchezo fulani.

Ama namna Rais Vladimir Putin wa Urusi anavyopendelea mchezo wa judo na kareti, pamoja na Barrack Obama anavyopenda mchezo wa kikapu, gofu na muziki.

Novemba 25, mwaka huu, dunia nzima ilipigwa butwaa baada ya kutangaziwa kifo cha jabali la mapinduzi na rais wa zamani wa Cuba, Fidel Castro.

Castro alikuwa swahiba mkubwa wa serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Nyerere na Cuba ilikuwa rafiki mzuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kifo cha Fidel Castro kimesikitisha wengi, lakini kwa umri wake wa miaka 90, uzee ulikuwa ukimtesa zaidi. Naamini kifo chake ni mapumziko.

Wengi tunafahamu Fidel alikuwa bingwa wa mapigano, urushaji risasi au matumizi ya bunduki pamoja na silaha nyingine za kivita sambamba na uongozi mahiri.

Pamoja na nyakati hizo ngumu, kama binadamu, alihitaji burudani, ambapo watu wa karibu wanasema alikuwa akihusudu pia vidosho alioshirikiana nao kimapenzi.

Katika simulizi mbalimbali za viongozi huwa ninapendelea kujua kiongozi wa nchi yoyote anapendelea mchezo gani. Vivyo hivyo ndivyo nilivyojiuliza kwa Fidel Castro kwamba wakati wa uhai wake alipendelea mchezo gani?

Baada ya kudurusu huku na huko imeonekana wazi Fidel kuna michezo aliipenda mno, mbali ya kupendelea kuvuta sigara. Mojawapo wa michezo hiyo ni mchezo wa baseball, ambao ni maarufu mno Marekani na baadhi ya mataifa ya Amerika.

Picha ya Agosti mwaka 1964 inamwonesha Fidel Castro akicheza mchezo wa baseball  mjini Havana, nchini mwake Cuba.

Picha nyingine ya mwaka 2002 inamwonesha akimzuia rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, asirushe mpira wa baseball katika viwanja vilivyopo Havana.

Picha nyingine inamwonesha Fidel Castro akicheza mchezo wa gofu. Huu ni mchezo maarufu mno nchini Marekani, na miongoni mwa miamba ya mchezo huo ni Tiger Woods.

Kwenye picha hiyo inamwonyesha Castro akimwangalia Mwanampinduzi Ernesto Che Guevara wakati akipiga mpira wa mchezo huo walioshiriki katika kitongoji cha Colina Villareal, jijini Havana.

Matukio hayo yanadhihirisha kuwa Castro hakuwa kamanda wa vita pekee, bali alipenda michezo na alimudu kuicheza kwa ufasaha.

Mara baada ya kuingia katika uongozi mwaka 1959, Fidel Castro alifanya kitu kimoja muhimu; kurejesha mafunzo ya elimu ya michezo na viungo na kutengeneza mikakati na sera ya kuinua michezo. Katika hilo alifanikiwa kuibua wanamichezo, walimu, wakufunzi wa kila daraja ambao walileta mafanikio makubwa.

Historia inaeleza kuwa, Cuba ni nchi ya kwanza kutoka Latini Amerika kuwa na medali nyingi za michezo ya Olimpiki. Cuba ina jumla ya medali 209; dhahabu (79) fedha (67) na shaba (70). Kwenye michuano ya Olimpiki mwaka huu pekee iliyofanyika nchini Brazil, Cuba ilijipatia medali 197 kwa ujumla.

Kwamba Fidel Castro alipendelea michezo, lakini yeye binafsi alikuwa na michezo fulani aliyomudu kucheza ambayo ni kriketi, gofu na baseball.

Kwenye mchezo wa soka zipo picha kadhaa zinamwonyesha Fidel akipiga mpira, lakini hakuonekani kama alikuwa anahusudu mchezo huo kama ulivyo wa gofu, kriketi na baseball, ambayo ni dhahiri ilikuwa starehe kwake.

Vilevile anajulikana kama kiongozi aliyependa sana kuvuta sigara. Lakini sifa nyingine ilikuwa ni kupenda vidosho. Anatajwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na vidosho mbalimbali na kwamba ilikuwa rahisi kwake kuachana na mama yake Fidelito (Fidelito yaani Fidel mdogo).

Castro amejihusisha na vidosho kadhaa kabla ya kuamua kufunga pingu za maisha kimya kimya mwaka 1980 na mkewe, Dalia Soto del Valle na kuzaa naye watoto watano wa kiume.

Baadhi ya vidosho hao ni Mirta Diaz-Balart, Dalia Soto del Valle, Natalia Revuelta Celia Sanchez (komredi mwenzake, sekretari na msiri wake kwa miaka 30), Juana Vera (mwalimu  na mkalimani), Gladys (mfanyakazi wa ndege), Pilar (mkalimani), Líder Máximo kwa kuwataja wachache. Huo ni ukurasa mwingine wa Fidel Castro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles