Ferdnanda Mbamila, Dar es Salaam
Uongozi wa Soko la Samaki Feri jijini Dar es Salaam, umesema fedha zilizotolewa juzi na Rais John Magufuli, kwa soko hilo, zitatumika kujenga ofisi za umoja wa soko hilo (Wawaki) na Sh milioni tano alizotoa mkewe, Mama Janeth Magufuli, zitawekwa kwenye mfuko wa akiba wa mama ntilie kwa ajili ya maendeleo ya shughuli zao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo Alhamisi Oktoba 4, Diwani wa Kata ya Kivukoni na Mwenyekiti wa Bodi ya soko hilo, Henry Masaba, amesema anamshukuru Rais Magufuli kwa kutimiza ahadi hiyo ya kiasi cha Sh milioni 20 ambapo fedha hiyo ilikabidhiwa juzi kwa katibu wa soko hilo.
Amesema Rais Magufuli alitoa ahadi hiyo alipowatembelea wafanyabiashara na uongozi wa soko hilo, Desemba mwaka jana siku aliyoaliapishwa na kukutana na wadau mbalimbali na kufanya usafi na wafanyabiashara hao.
“Rais alikuja kwa kushtukiza katika zoni namba nane ambapo alifanya mazoezi katika eneo hilo, aliahidi fedha hizo na juzi alitimiza ahadi hiyo kwa kutoa kiasi chote alichoahidi ambapo alimuagiza Katibu wa Ikulu na kuikabidhi katika uongozi wa soko.
“Kwa kuwa, Rais ametimiza ahadi hiyo kama alivyoahidi kwa umoja wa wafanyabiashara wa soko, uongozi wa soko kwa unatoa shukrani kwake,” amesema Masaba.